Sunday, August 14, 2022

KITINI CHA UENDESHAJI WA URAGHIBISHI

 

MTANDAO WA JINSIA (TGNP}

KITINI CHA UENDESHAJI WA URAGHIBISHI

GUIDELINE FOR CONDUCTING PARTICIPATORY ACTION RESEARCH (PAR)

 SEHEMU YA KWANZA.

Maana ya urgahbishi.

Uraghbishi hutegemea imani kubwa kuhusu uwezo na uelewa wa watu. Uraghbishi unajengwa katika mtazamo alionao mraghbishi juu ya watu wengine kwa kuwaona na kuamini kwamba wana maarifa ya kutosha, uelewa kuhusu hali zao na uwezo hivyo wanahitaji kuchokozwa waweze kutafakari zaidi, kuchambua na kuchukua hatua. Mraghbishi anawawezesha watu kujifahamu wenyewe na kujiamini kwamba wanao uwezo mkubwa na ‘raghba’ yao hutokana na hali ya kujifahamu na kujiamini.

 

Misingi ya uraghbishi na sifa za mraghbishi.

§  Kiu ya haki kwa wote, hasa wale ambao wamenyanyaswa, au kukandamizwa au kunyonywa au kupuuzwa au kusahauliwa na kutengewa na mfumo

§  Imani kwamba binadamu wote wana uzoefu na ubunifu wao na hamu ya kuona kwamba uwezo na ubunifu huu unapewa uzito unaostahili

§  Kupenda kutumia ushiriki wa hali ya juu

§  Uwezo wa kuwachokoza watu ili waweze kuchambua hali halisi inayowakabili na mbinu za kuibadili hadi wachuke hatua wenyewe

§  Uwezo wa kuwasiliana na watu na kuwawezesha kama mwenzao

§  Uwezo wa kujenga muafaka na maisha na kazi ya wale anaofanya kazi nao

§  Uwezo wa kukabili hali ya migogoro na hata ugomvi

 

Aina za uraghbishi.

Kwa kuzingatia kwamba uraghbishi kweli ni mchakato kuliko tendo, yafaa kukumbuka kwamba shughuli nyingine zinaweza kutumia falsafa na mbinu za uraghbishi, lakini si uraghbishi kamili.

 

Uraghbishi kamili (mraghbishi wa ndani)

Katika uraghbishi kamili, mtu (mtumishi wa ugani, mwanaharakati, au mgeni yeyote anaenda kuishi katika jamii ambapo anataka kufanya uraghbishi. Huu ni uraghbishi kamili kwa sababu unapotembelea jamii, au hata kuendesha mafunzo huwezi kuelewa hali halisi ya jamii na wanajamii kwa muda mfupi hivyo. Aidha, inachukua muda kwa jamii kumwelewa mraghbishi, kumpima na kumwamini ili wajisikie huru kujadiliana naye.


Uraghbishi wa kutembelea (mraghbishi wan je).

Hapo mwanaharakati, mtumishi wa ugani au mgeni yeyote anaingia na kutoka katika jamii, mara nyingi kwa sababu hana muda. Hivyo hakai pale bali anaenda mara kwa mara (na mara nyingine anaishi karibu pia). Huu si uraghbishi kamili na kwa sababu mtu hana muda wa kutosha kuelewa na kueleweka, ni rahisi sana kurudia tena mbinu za uhamasishaji na kutoa ushauri bila kuelewa kwa undani. Au kwa sababu muda ni mfupi, ni rahisi kufikia kwenye maelezo badala ya maulizo, hasa kama mraghbishi hana subira.

Uraghbishi wa mafunzo/warsha

Huu nao hauwezi kuitwa uraghbishi kamili lakini mwezeshaji anaweza kutumia mbinu shirikishi na za kiraghbishi zaidi katika kuendesha warsha. Hivyo daima hataanza na mihadhara n.k. bali atajaribu kuwachokoza washiriki waseme walicho nacho wao na kujenga juu ya wanavyoona wao.

Katika uraghbishi wa aina zote, lengo kuu ni kuwahuisha, kuwazindua watu waweze kushika usukani wa maendeleo yao na maisha yao, waweze kuchambua na kuelewa kwa undani.

 

Hatua za uraghbishi.

Ili uraghbishi uweze kutimia kwa ukamilifu, inatakiwa hatua kuu tatu muhimu lazima zipitiwe. Hatua hizi zinamwezesha mraghbishi na wanajamii kuyapitia kwa makini masuala yote muhimu yanayojadiliwa kiundani kwa lengo la kuyaelewa na pia kuyapatia ufumbuzi. Hatua hizi zinafahamika kama U3 (U Tatu) ambapo ni:

 

Upimaji (Utambuzi/Uibuaji) -------------------- Uchambuzi------------ Utekelezaji

 

Lengo la uraghbishi huwa linatimia vema pale ambapo mambo yaliyoibuliwa yanaweza kuchukuliwa hatua. Wakati wa uraghbishi wanajamii wataweza kufahamu masuala kadhaa, kisha kuyachambua lakin pia watataka kucukua hatua kukabiliana na hali kadhaa. Hii ni muhimu kwa sababu inazingatia uwezo wa jamii kuleta mabadiliko na maendeleo badala ya kusubiri kufanyiwa kila kitu.


 

Upimaji:         Hali ikoje?

Uchambuzi.  Mambo gani yanasababisha hali hii?

Utekelezaji:  Hatua zinazochukuliwa kwa misingi ya upimaji na uchambuzi.

 

Upimaji

Mbinu za kuibua: Jambo la kwanza kwa mraghbishi ni kujua wanajamii wako wapi kimtazamo na kiufahamu. Hali yao ikoje, maisha wanayaonaje? kwanini wanafanya wanavyofanya, ndoto zao ni zipi, je ndoto zao zinatimilizwa na maisha wanayoishi sasa? Zinakwamishwa na nini? Katika kuibua tunaweza pia kujua mtazamo ya wanajamii na uelewa wao kuhusu masuala husika. Hivyo ni bora kutumia mbinu shirikishi zinazoibua na wakati huohuo kuongeza uchambuzi.

 

Uchambuzi

Hatua ya pili ni kuchambua yale yote yaliyojitokeza katika hatu ya kwanza. Hata tunahitaji kujua zaidi kuhusu hali na masuala husika. Mathalani mara nyingi tunapata sababu zilizo wazi, kwa mfabo tunaweza kuambiwa sababu ya wasichana wadogo kupata mimba kwenye jamii inatokana na ‘tamaa’ ama mkundi rika yanayopotosha. Lakini waraghbishi hatukomei hapo. Tunataka kuuliza zaidi na kuwaongoza wanajamii kuchambua sababu hizi za wazi ili kupata sababu za ndani na za kina, na ia kuchambua sababu za kimfumo. Vivyo hivyo, bila kuwa na dhana ya uchambuzi kijinsia inawezekana masuala ya jinsia hayataonekana.

 

Utekelezaji

Katika hali ya kawaida, kila mtu anatambua tatizo, analichambua kisha anachukua hatua. Utekelezaji utafanyika kulingana na upimaji na uchambuzi sahihi. Kuendeleza duara hili la u- tatu. Baada ya kuchukua hatua, inabidi kutambua au kupima na kuchambua tena kama hatua zilizochukuliwa zimetatua tatizo, au kubadili tatizo au kushindwa kabisa kukabili tatizo lenyewe.

 

Hata hivyo, ili U- Tatu ifanikiwe, lazima kila hatua ichukuliwe kwa usahihi.

 

Lakini hii ni duara kwa sababu baada ya kuchukua hatua, inabidi kupima na kuchambua matokeo ya hatua ili kuweza kuchukua hatua nyingine tena.

 

 

 

 

 

SEHEMU YA PILI.


 

Hatua muhimu za uraghbishi:

Mraghibishi anatakiwa kufuata hatua zifuatazo wakati anapoanza kutekeleza majukumu yake ya kiuraghibishi. Hatua pia zinahusisha mbinu anazotakiwa kutumia anapokuwa katika jamii.

 

Kujitambulisha

Mraghibishi anatakiwa kujitambulisha kwa uongozi wa jamii kabla hata ya kuanza kazi na makundi ambayo yatashiriki katika uraghbishi. Hatua muhimu inahusu kuripoti katika ofisi ya Halmashauri, kisha ofisi ya Kata ama ofisi ya kijiji husika na kukutana na viongozi akiwemo Mtendaji kata/kijiji, mwenyekiti wa kijiji/kitongoji ama ni muhimu kukutana na viongozi wote wa serikali ya kijiji.

 

Mraghbishi anajitambulisha na kuelezea kuhusu malengo ya shughuli yake na namna atakavyofanya kazi katika jamii.

 

Ni vema kuwaomba wenyeviti wa serikali za mitaa/vitongoji kukupatia makundi ya watu watakaoshiriki katika katika kazi ya uraghbishi. Kwa kuwa inaweza kuwa vigumu kuita mkutano mmoja wa kikijiji na watu wote. Mraghibishi anaweza kuomba ruhusa ya kupita mitaani/kijiji akiambatana na mwenyeji ambaye ni kiongozi wa eneo hilo. Huko ataweza kuwaomba wale walio tayari ili kukaa pamoja naye katika kikundi chenye watu kati ya sita na kumi na mbili.

 

Ni vema kuendelea kuwaomba wale walio tayari kukutana nao siku inayofuata ikiwa hamkuweza kumaliza mazoezi yote ya uraghbishi katika siku ya kwanza.

 

Ugawaji wa makundi

§  Vijana wa kike – miaka 15 – 24

§  Vijana wa kiume – miaka 15 – 24

§  Wanawake watu wazima

§  Wanaume watu wazima

§  Watu wenye ulemavu

§  Viongozi wa serikali ya kijiji

 

Unaweza kupanga makundi kulingana na mahitaji ya uraghbishi, kwa mfano:

§  Vijana wa kike – miaka 13 – 17

§  Vijana wa kiume – miaka 13 – 17

§  Vijana wa kike – miaka 18 – 24

§  Vijana wa kiume – miaka 18 – 24


Baada ya kuwapata waeleze madhumuni ya mazoezi ya uraghbishi mnayokwenda kuyafanya na hakikisha wanaelewa dhamira yako na jinsi wao watakavyonufaika na masuala yatakayoibuliwa.

 

Kila kikundi kitafanya mazoezi kama yalivyoainishwa kulingana na utaratibu wao. Kwa mfano kuna mazoezi maalum kwa kikundi cha vijana na mazoezi maalum kwa vikundi vya watu wazima. Japokuwa makundi haya yanaweza kutumia mbinu zote lakini ni muhimu kuangalia muktadha na utayari wa makundi hayo kabla ya kujaribu ama kutumia mbinu hizi.

 

Kabla ya kuanza waombe wanajamii kupanga muda gani ni mzuri kwao kwa ajili ya kufanya kazi hii. Wekeni makubaliano kuhusu muda na jinsi mtakavyoifanya. Waambie kwamba ‘hili ni zoezi la hiyari kwa ajili ya maendeleo ya jamii yao, hivyo kila mmoja ana nafasi ya kuamua kama atapenda kushiriki au lah’

 

Baada ya kupitia mazoezi yote kwa pamoja. Waambie kwamba watahitajika kwa ajili ya kufanya mrejesho katika kikao kitakachohusisha viongozi wa kijamii.

 

Katika kila kundi mraghbishi awaongoze wanakikundi kuchagua kiongozi wao. Kiongozi atakabidhiwa fimbo kama ishara ya kuwaongoza wengine na si kuwatawala. Kwa kuwa yeye ndiye amekubalika miongoni mwa wengine, atakuwa na jukumu la kuhakikisha kuwa mjadala unafuata taratibu na kila mmoja anapata nafasi ya kuchangia. Haitakuwa tena kazi ya mraghbishi kuwaamsha wanajamii wachangie bali anatakiwa kuwa na jicho la kuona nani anaweza kuchangia huku akiwasiliana na kiongozi.

 

 

MBINU ZA URAGHBISHI. UPIMAJI.

Zoezi la kwanza: NANI MWENYE NGUVU (Power Walk)

Zoezi hili litumike kwanza ili kutambua watu wenye uwezo ama wenye nguvu na uhusiano wao na makundi mbalimbali katika jamii na kuchambua kwa nini wengine wako mbele na wengine wanabaki nyuma. HATUA hii ni muhimu katika kuibua mambo ya msingi kama ya kuanza kuyachambua. Zoezi hili linaweza kuwa na mantiki zaidi iwapo wanajamii kwa pamoja wakiwemo viongozi wao pia wanaweza kushiriki ili kutambua hali halisi ya jamii yao. Wachache kulingana na namna mraghbishi atakavyopanga wanaweza kushiriki moja kwa moja na wengine wakibaki kwa ajili ya mjadala.

 

Hatua za mraghbishi:


·         Tafuta eneo la wazi lenye nafasi ya kutosha kwa watu kupiga hatua mbele angalao hatua ishirini.

·         Mgawie kila mwanajamii karatasi yenye mhusika mmoja.

·         Wahusika wawe mchanganyiko wa watu wenye uwezo, viongozi wa kijamii, watu wenye ushawishi na hata wananchi wa kawaida (diwani, mtendaji kata/kijiji, mwalimu mkuu, mfanyabiashara wa mazao n.k.) na wale wasio na uwezo (mtoto yatima wa kike na kiume, mfanyakazi wa baa, kijana wa kijiweni, msichana wa kazi wa mtendaji, msichana mwenye mtoto, n.k.) na wengine wa uwezo wa kati.

·         Wapange katika mstari mmoja wakitazame mbele mahali uliposimama.

·         Kisha waambie kwamba utasoma kauli moja baada ya nyingine. Kama jibu la mhusika ni ndiyo atapiga hatua moja kwenda mbele. Kama ni hapana na haimhusu basi atabaki palepale.

·         Zoezi litaendelea namna hiyo mpaka masuala yote ambayo yameandaliwa na mraghibishi yawe yameshasomwa yote.

·         Baada ya kumaliza kusoma na wakati tayari watu kadhaa watakuwa wamepiga, anza kuwauliza wale walio mbele wajitaje wao ni wakina nani.

·         Wahoji mmoja mmoja kulingana na uwakilishi wao. Wageukie walio nyuma na kuwaomba nao waeleze ni wakina nani.

 

Unaweza kutumia maswali haya kiujumla.

·         Kwa wale waliopo mbele, mlijisikiaje wakati mnapiga hatua zaidi ya wengine?

·         Je mlifurahi kuona wengine wakiwakaribia? Kwanini?

·         Kuna wakati wowote uligeuka nyuma kuwatazama wengine? Ulijisikiaje?

·         Kwa waliobaki nyuma; ulijisikiaje ulipoona wengine wanasonga mbele na wewe unazidi kuachwa?

·         Hali hii inalingana vipi na maisha halisi ya kijiji/kitongoji ama jamii yenu?

·         Nani anaachwa nyuma? Kwanini?

·         Ikiwa hali hii inatokea, tunaweza kuizungumziaje?

 

Mifano ya wahusika:

·         Mtendaji kata.

·         Mtendaji wa kijiji.

·         Mwenyekiti wa kijiji.

·         Mwalimu mkuu.

·         Daktari wa zahanati ya kijiji.

·         Mgambo wa kijiji.

·         Mfanyabiashara wa mazao.


·         Bibi mlezi wa yatima.

·         Msichana yatima umri wa miaka 14.

·         Mvulana yatima umri wa miaka 17.

·         Msichana mfanyakazi wa baa.

·         Mtoto wa Mtendaji kata.

·         Kijana wa kijiweni.

·         Mkulima mwanaume

·         Mama mjane mwenye watoto 6.

·         Mfanyabashara wa madini.

·         Mfugaji ndugu wa mbunge.

·         Kijana dereva wa bodaboda.

·         Mganga wa jadi.

·         Kibarua wa mashambani.

 

Mifano ya kauli

·         Nina umri wa zaidi ya miaka 30.

·         Napata angalao milo mitatu kwa siku.

·         Ninaweza kupata mkopo.

·         Sijawahi na sio rahisi kunyanyaswa kijinsia.

·         Naweza kumudu gharama katika hospitali binafsi.

·         Sina haja ya kutafuta maji.

·         Ninaweza kwenda sekondari au nimekwenda sekondari.

·         Nina mradi wa uchumi.

·         Wakija wageni maarufu kijiji napata nafasi ya kukutana nao.

·         Ninaongea kwenye mikutano ya kijiji.

·         Nashiriki katika vikao vya bajeti ya kijiji.

·         Nina uwezo wa kulipa ada ya shule.

·         Nina uwezo wa kumiliki radio na kupata taarifa mbalimbali.

·         Ninaweza kukutana na mbunge kila ninapohitaji.

 

Katika mjadala unaweza pia kuibua masuala ya kiraghbishi mliyolenga kuyatazama, mathalani masuala kuhusu mila, desturi kwa kuangalia ni nani kati ya wahusika mliowaona ambao wana nguvu na ushawishi. Vilevile inaweza kuwa masuala kuhusu maji, rasilimali, jinsia na hata ukatili wa kijinsia.

 

Zoezi la pili: UCHORAJI WA RAMANI


Baada ya kumaliza zoezi la kwanza la kuchambua watu wenye nguvu na namna utofauti wake unavyoathiri mahusiano katika jamii, mraghbishi ataanza kukaa na wanajamii kwa ajili ya zoezi la kutambua hali halisi ya jamii, kuhusu masuala yanayohitaji kufanyiwa uraghbishi mathalani mila na desturi zinazochochea ukatili kijinsia na nafasi ya mwanamke katika jamii. Uchoraji wa ramani pia utatoa mwanga mzuri wa kujua jamii ianzie wapi katika kutafuta suluhu ya matatizo yao na pia itakuwa ni chanzo cha kuweza kukusanya taarifa ndani ya kijiji na kuzitafutia ufumbuzi kwa kushirikiana. Katika ramani wanajamii wataweza kuainisha ni mazingira gani yanasababisha ama kuchochea vitendo vya ukatili kijinsia, wapi matukio haya yanatokea, nani anahusika na pia ni aina gani ya vitendo vya ukatili vinavyofahamika kwa wanajamii halikadhalika mila na desturi zilizopo.

 

Vilevile uchoraji wa ramani unawezesha kutambua mifumo mbalimbali ya kijamii inayoweza kutumika kushughulikia masuala ya mila na ukatili wa kijinsia. Wanajamii wanatakiwa kuchora ramani kwa kuonyesha mifumo na miundombinu muhimu kama majengo ya serikali, ya kijamii, nyumba za ibada, kituo cha polisi, ofisi ya asasi isiyo ya kiserikali nk.

 

Hatua za mraghbishi:

·         Tafuta eneo lenye kufaa kwa ajili ya kuchora ramani ya kijiji.

·         Wanaweza kuchora ramani chini kwenye udongo iwapo hakuna karatasi kubwa na kalamu kwa ajili ya kufanya hivyo.

·         Waambie wanajamii wachore ramani ya kijiji/kitongoji chao kwa kuonyesha mipaka ya kijiji na maeneo muhimu kama vile, barabara ‘kuu’, ofisi za serikali ya kijiji, shule, zahanati, soko, mto, kituo cha polisi nk.

·         Pia waonyeshe mahali ambapo vijana wanakutana ama hupenda kushinda kwa kuyawekea alama maeneo hayo. Wanaweza kutumia alama fulani kuonyesha mahali ambapo vijana hukutana; alama kama vile jani ama kokwa ya tunda nk.

·         Vilevile waonyeshe ni mahali gani ambapo mikutano ya kijiji ama mikutano kwa ajili ya kufanya maamuzi huwa inafanyika. Wakati wa kuonyesha waseme pia iwapo vijana wanahudhuria katika maeneo hayo ama wanashiriki vipi?

·         Wataonyesha pia mahali na huduma tofauti za kijamii zinapopatikana.

 

Mraghbishi anaweza kutumia maswali haya kuchokoza zaidi.

·         Kwa upande wa maeneo hatarishi:

o   Je ni maeneo gani ya hatari zaidi katika jamii?

o   Ni hatari zipi zinapatikana maeneo hayo?

o   Nani yupo kwenye hatari zaii katika maeneo hayo? Wanawake? Wanaume? Vijana wa kike/kiume?

o   Nani anasababisha hatari hizo?


 

·         Kwa upande wa huduma:

o   Ni huduma gani zinapatikana katika jamii?

o   Wanawake wanapata huduma zipi?

o   Vijana wa kike na wa kiume wanapata huduma hizi?

o   Nani anatoa huduma na kwa kiwango gani? Km. afya, elimu, ulinzi, ushiriki nk.

 

·         Kwa upande wa ulinzi:

o   Kuna mifumo gani katika jamii ambayo inamhakikishia mwanamke, msichana ama kijana/wanaume ulinzi dhidi ya ukatili kijinsia?

o   Nani anasimamia mifumo hiyo? Kwa kiasi gani?

o   Mifumo inaaminika? Kwa kiwango gani?

o   Changamoto zipi zinapatikana katika masuala ya ulinzi dhidi ya vitendo vya ukatili kijinsia?

 

·         Kwa upande wa utawala bora:

o   Wanasemaje kuhusu uwajibikaji wa viongozi?

o   Wanaheshimu mawazo ya wananchi?

o   Kuna uwazi? Kwa kiasi gani?

o   Kuna njia gani za kuwawajibisha viongozi wanapokiuka misingi ya utawala bora?

o   Njia hizo zinafanya kazi? Kwa kiasi gani?

 

Tanbihi:

Si lazima mraghbishi afanye yote bali kwa yale muhimu ambayo yanahitajika kwa kutegemea muktadha. Mazoezi hayapaswi kuwa marefu sana kiasi cha kuchukua muda na kuwachosha wanajamii. Vinginevyo kama kuna mjadala mkali basi mraghbishi anaweza kuendelea kwa dakika kadhaa. Muda mzuri zaidi kwa kila zoezi ni dakika arobaini ama saa moja.

 

Zoezi la tatu: MSTARI WA KALENDA (Timeline).

Hii ni mbinu kwa ajili ya kuibua kutoka katika kundi la watu wazima. Mraghbishi ahakikishe kuwa anapata kundi la watu wazima ambao wameishi katika jamii ama kijiji husika kwa muda wa kutosha kuelewa kiundani ‘historia’ ya mahali hapo. Bila shaka watakuwa wameshuhudia mabadiliko mengi katika mifumo ya maisha, uhusiano, mila na tamaduni za mahali hapo.

 

Lengo ni kuwachokoza ili waweze kuorodhesha hali halisi ya jamii yao kwa sasa kulinganisha na zamani. Mwishoni wataweza kuona ni wapi mambo yalibadilika na sababu za mabadiliko hayo.

 

Hatua za mraghbishi:


·         Waulize wanajamii ni kwa muda gani wameishi katika eneo/kijiji ama jamii hii.

·         Wanaweza kutoa mifano mmoja mmoja na utagundua kuwa pengine idadi kubwa wameishi mahali hapa kwa zaidi ya miaka 20 ama 30 nk.

·         Sasa waambie kwamba utataka kujua historia ya mahali hapa katika masuala yanayohusu uhusiano wao katika jamii na hapa mtaibua namna mila na desturi zilivyobadilika ama kutekelezwa.

·         Waambie kwamba hamtaweza kuangalia kila kitu kuhusu historia bali mambo fulani machache ili nawe ujifunze kutoka katika masimulizi yao.

 

·         Sasa waombe wachore mstari mmoja mnyoofu chini ya ardhi. Wataanza na kuweka tarehe (mwaka) ya mwanzo wanayotaka kuanza nayo km. 1973 mwanzo wa mstari. Kisha wataanza kuorodhesha matukio kadhaa yaliyojitokeza tangu wakati huo hadi kufikia sasa.

(matukio yawe yanayohusu namna uhusiano katika jamii ulivyobadilika, matukio gani yaliathiri mila na desturi zao nk)

·         Wahimize waendelee kuchora na kukukumbuka, kwa mfano ‘Vita ya Kagera’, ‘Kipindi ambacho jamii yao ilikubwa na ukame, njaa, magonjwa, vifo nk na kwamba haya yote yalibadili vipi desturi zao na kuathiri mila zao kwa namna gani.’

 

Baada ya kumaliza unaweza kupitia mstari wao na kuuliza maswali:

·         Mabadiliko haya yaliathiri vipi uhusiano kati ya wanajamii?

·         Kulikuwa na mila ama taratibu gani za kumlinda mwanamke ama kijana dhidi ya ukatili wa kijinsia?

·         Ni mila zipi zilitelekezwa? Nani alizitelekeza? Kwanini?

·         Je ni vijana ama wazee ndio walioacha mila hizi?

·         Ni wakati gani vitendo vya ukatili kijinsia vilionekana kushamiri? Kwanini?

·         Kulikuwa na utaratibu gani wa kushughulikia masuala ya ukatili kijinsia?

 

UCHAMBUZI:

 

Hatua ya pili baada ya UPIMAJI (uibuaji) ni UCHAMBUZI. Hapa mraghibishi atawaongoza wanajamii kuweza kuchambua na kujua sababu za kina kwa masuala ambayo yaliibuliwa katika hatua iliyopita ili kupata kiini cha jambo na kuweza kulishughulikia.


Zoezi la kwanza: UPANGAJI WA VIPAUMBELE 1 (Ranking)

Kupiga kura.

Zoezi hili linaweza kutumika kama zoezi la mwanzo la kujenga msingi kwa ajili ya kupata mambo ya muhimu kabisa. Itampa nafasi kila mwanajamii kupiga kura na kutaja jambo moja ambalo yeye anaamini kuwa ndilo la msingi zaidi linalohitaji kushughulikiwa kutokana na athari zake kwa jamii. Baada ya kuwa wanajamii wote wameorodhesha mambo yaliyotokana na sehemu ya kwanza ya uraghbishi, wakumbushe kuwa mtaanza kufanya tathmini ya kila mmoja. Itakuwa rahisi kwao kuyataja kwa sababu watakuwa wameshaanza kuyaibua kwenye mstari wa kalenda, na uchoraji wa ramani.

 

Hapa wanajamii watapiga kura ili kupata jambo moja la mwisho kwa kila mmoja ambalo ndilo litawekwa katika orodha ya upangaji mawe. Inategemewa kwamba kwa kuwa mawazo ya wanajamii yatatofautiana basi yale ambayo yamebaki kwa kila mmoja yatajumuishwa kati hatua inayofuata.

 

Hatua za mraghbishi:

·         Waambie wanajamii wafikiria kuhusu mila na desturi ambazo wanazifahamu na ambazo hutekelezwa mara kwa mara katika jamii.

·         Kisha wagawie kila mmoja vikaratasi vitano.

·         Kila mmoja aandike aina tano za mila na desturi katika vipande vidogo vya karatasi (ikiwa wote wanaweza kuandika). Ama wanaweza kutumia vijiti na alama tofauti.

·         Baada ya kila mmoja kuwa na vikaratasi vitano ambapo kila kimoja kimeandikwa aina ya ukatili kijinsia, sasa waambie kuwa watapaswa kufanya maamuzi magumu.

·         Waambie kuwa kila mmoja ajifikirie kwamba yupo ndani ya mtumbwi na anasafiri majini akiwa na masuala hayo matano anayotaka kuyashughulikia.

·         Lakini kwa kuwa hali ya bahari imechafuka, analazimika kuondoa baadhi ya mizigo na kuitosa baharini ili kupunguza uzito wa chombo. Hapo utamtaka kila mmoja kuondoa karatasi moja yenye aina mojawapo ya mila na desturi ambayo anahisi haina athari sana kulinganisha na nyingine.

·         Endelea kuwaambia wapunguze karatasi moja kila mara na kubaki na zile ambazo wanaona ni lazima kufika nazo pwani ili ziweze kushughulikiwa. Wataendelea  kupunguza mpaka pale watakapobaki na karatasi moja tu. Hii itamaanisha kuwa kila mmoja amebaki na suala moja ama aina moja ya mila na desturi ambayo inamkera zaidi.

·         Watake kila mmoja asome ya kwake na kisha ziandike.

·         Pitia orodha pamoja na wafahamishe kwamba haya ndio masuala ama aina za mila ambazo zina umuhimu sana kushughulikiwa. Km kurithi wajane, ukeketaji, utakasaji wa wajane wanapofiwa na waume zao, jando na unyago yenye mafunzo yasiyofaa kwa watoto, marufuku kutojadili masuala ya ukatili kijinsia, nk.


·         Yachukue masuala hayo kwa ajili ya zoezi linalofuata.

 

Zoezi la pili: UPANGAJI WA VIPAUMBELE 2

Upangaji wa mawe.

Hii ni mbinu inayotumika kwa ajili ya kuchagua mambo ambayo yana athari zaidi ya mengine katika jamii husika kutokana na mitazamo wa wanajamii. Orodha hiyo ya vitendo vya ukatili kijinsia itaweza kutokana na zoezi lililopita. Ikiwa masuala ni mengi mnaweza kupiga kura na kupata masuala matano ama sita tu ambayo itakuwa rahisi kuyapitia.

 

Hatua za mraghbishi:

·         Kwa kushirikiana na wanajamii, anza kutaja masuala yote yaliyoorodheshwa kutoka katika hatua ya kwanza ya uibuaji.

·         Waonyeshe jinsi ya kupanga mawe. Angalia mfano hapa chini

·         Baada ya kupata orodha, waambie kwamba sasa watapiga kura ili kujua athari za kila jambo na kuangalia ni nani anaathirika zaidi.

·         Wakusanye mawe madogo ishirini kwa ajili ya kuyapanga. Kisha wachore jedwali na

kuweka chumba cha kwanza ‘masuala’, halafu ‘wanaume’ na mwisho ‘wanawake’

·         Waorodheshe masuala yote kisha waanze kugawa mawe kwa kutoa idadi kubwa kwa yale yaliyo na uzito zaidi. Kama wanaona suala la kurithi wajane linahitaji uzito zaidi wanaweza kuweka mawe matano au sita, kisha kama suala la ukeketaji linafuata wanaweka mawe matatu au manne na kuzidi kufanya hivyo kwa kila jambo.

·         Waambie kwamba wanaruhusiwa kubadilisha ikiwa wamefika mwisho na hawaridhiki.

Mfano wa jedwali

Masuala

Wanawake

Wanaume

kurithi wajane

5

3

marufuku kutojadili masuala ya ukatili kijinsia

2

5

jando na unyago yenye mafunzo yasiyofaa kwa watoto

3

6

utakasaji wa wajane wanapofiwa na waume zao

4

3

ukeketaji

6

3

 

 

 

 

 

 

 

Angalizo: Epuka kumpa kila mwanajamii mawe kadhaa ili apige kura kwenye jambo analoona ni muhimu sana. Japo kwa kufanya hivi kazi itaisha haraka lakini hakutakuwa na mjadala. Wakati wa kupanga mawe wanajamii wanatakiwa kujadili, kubishana na kukubaliana. Wakati wanafanya hivi watatoa hoja ambazo ndizo msingi wa zoezi.


Hapa hoja nyingi zitaibuka na mraghbishi ataweza kuendelea kuchokoza na kuandika yatokanayo na mjadala.

 

Zoezi la tatu: MADUARA YA UCHAMBUZI (Venn Diagram).

Zoezi hili linalenga katika kuchambua namna masuala mbalimbali mathalani ya mila, desturi, ukatili kijinsia yanavyomuathiri hususani mwanamke. Mraghbishi atawachoza wanajamii ili waweze kujadili na kueleza ni nani anayeathiriwa zaidi na mila na desturi zilizotajwa. Katika makundi yatakayotajwa inaweza kujitokezwa kwamba wanawake ana vijana hasa wasichana ndio waathirika zaidi wa mila na desturi zinazotajwa. Mraghbishi ataandaa kadi za duara zenye ukubwa tofauti kulingana na orodha ya masuala ama mila na desturi zilizoorodheshwa.

 

Hatua za mraghbishi:

§  Waulize wanajamii ni mila na desturi zipi zinazotekelezwa kwa kiasi kikubwa. Kisha ile ambao inatekelezwa kwa kiasi kikubwa itapewa duara kubwa na kuandikwa humo. Hii itafuatiwa na mila ama desturi ambayo haitekelezwi sana kwa kupewa duara ndogo mpaka kufikia ile ndogo zaidi kwa mila na desturi ambazo hazitokei mara kwa mara.

§  Waambie washiriki wazunguke wakisimama kwenye duara.

§  Mwombe kiongozi aweke duara moja ndogo ambayo inamwakilisha mwanamke/mwanajamii katikati.

§  Kisha mpe mwanajamii yeyote katika kundi aweke kadi mojawapo jirani na ilipo kadi ya mwanamke. Anaweza kuweka kadi hii karibu kabisa ama mbali zaidi.

§  Bila kujali ukubwa wa kadi, kwa kadiri inavyokuwa karibu inamaanisha kwamba jambo hilo lina athari kubwa zaidi.

§  Na kwa kadiri kadi inavyokuwa mbali inamaanisha jambo hilo halina athari sana. Kwa mfano, kurithi wajane si mila inayotekelezwa kwa kiasi kikubwa hivyo ni kadi ndogo lakini inapotokea athari zake huwa ni kubwa sana. Kwa vyovyote kadi hii italetwa karibu zaidi na ilipo kadi inayomwakilisha mwanamke/mwanajamii.

§  Waruhusu wanajamii wapange kadi huku wakijadili sababu za wao kufanya hivyo, wakibishana na kueleza zaidi mpaka watakaporidhika.

 

UTEKELEZAJI.

 

Sehemu hii inahusu mbinu mbalimbali za kutumia kwa ajili ya kuweka mikakati kuhusu yale ambayo tayari makundi yamepitia. Utekelezaji utafanyika katika mkutano wa mrejesho ambapo makundi yote yatakutana pamoja na uongozi wa kijiji.

 

Mara baada ya mazoezi ya uraghbishi kwa kila kikundi, panga kuhusu mkutano wa mrejesho kwenye ngazi ya kijiji. Kila kikundi kitajiandaa kufanya mrejesho wa yale waliyoyajadili, kuyaibua


na kuyachambua. Ikiwa washiriki ni wengi basi kila kikundi kitachagua wawakilishi wawili wa kuhudhuria mrejesho wa kijiji.

 

Zoezi la kwanza: NDOTO ZETU

Baada ya kila kikundi kufanya mrejesho wake, waraghbishi wataandika yale yote ambayo yameonekana kupewa kipaumbele. Hapa lazima kuangalia ni masuala gani ambayo yanajirudia kutoka katika vikundi vyote.

 

Kwa kutegemea na muda na nafasi, inaweza kufanyika kwa kutumia makundi manne ambapo viongozi wa kijamii wanaweza kuchanganyika katika vikundi vya wanaume au kama ni viongozi wanawake katika kikundi cha wanawake na pia vijana wa kiume na wa kike.

 

Hatua za mraghibishi:

·         Waombe wanajamii wachore mstari mrefu unaojulikana kama ‘mstari wa maisha’.

Wanaweza kuugawa mstari huo katika sehemu tatu kuanzia wakati walipo sasa.

·         Sehemu ya kwanza

·         Sasa mpaka miaka mitano ijayo

·         Sehemu ya pili:

·         Miaka mitano hadi kumi

·         Sehemu ya tatu

·         Miaka kumi hadi kumi na tano/ishirini

·         Katika kila sehemu waambie wanajamii wawe huru kuchora ndoto zao kwa kuzingatia masuala yale yaliyoibuliwa katika mijadala ya vikundi na katika mrejesho.

o   Ni jamii ipi wanayoitaka katika kipindi fulani cha maisha? Wanaweza kutafuta

kauli mbiu wakati wa kuchora, km. ‘Jamii yetu bila mila kandamizi.’

o   Mabadiliko gani wanayotarajia kuyaona?

o   Aina gani ya mahusiano ambayo wangependa kuyaona baina ya wanawake, wanaume, vijana wa kiume na wa kike pamoja na watoto.

o   Mifumo gani ya ulinzi dhidi ya ukatili wa kijinsia kwa kuangalia mila na desturi zinazoweza kuongeza ulinzi.

 

·         Wanafanya hivi kwa kuchora lakini wasisitize kwamba uchoraji wao uwe na uhalisia kulingana na hali na matarajio ya jamii yao.

·         Mwishoni fanya mjadala ili kujua

o   Wanatarajia kufanya nini ili kutimiza ndoto zao?

o   Nani anaweza kufanya nini?

o   Mkakati gani wanajiwekea?


Zoezi la pili: UCHAMBUZI WA MAJUKUMU

Baada ya kuchora ndoto zote, waraghibishi wataandika kile ambacho jamii inatarajia. Hapa pia wasisahau kuhusu masuala yaliyoibuka katika mrejesho kama sehemu ya mambo muhimu yanayotakiwa kutekelezwa.

 

Hatua za mraghbishi:

Waambie wanajamii kuwa wanatakiwa kuorodhesha watu wote waliopo kwenye jamii kulingana na vyeo na majukumu yao, kwa mfano:

·         Mwenyekiti wa kijiji.

·         Mtendaji.

·         Mwenyekiti wa ulinzi na usalama.

·         Diwani.

·         Wazee wa mila.

·         Ngariba.

·         Muuguzi

·         Nyakanga/kungwi.

·         Mzee maarufu

·         Mtaalamu wa afya.

·         Asasi inayofanya kazi kijijini nk.

 

Wanajamii watachora jedwali lifuatalo na kuweka kila mmoja na nafasi yake. Kwanza wataandika jina/cheo cha mhusika katika sehemu ya jedwali inayoonyesha mhusika, halafu wataangalia kuhusu ndoto zilizopo na masuala yaliyopendekezwa kufanyika na kisha watasema kuhusu nini anapaswa kufanya ili kufikia ndoto hiyo. Katika sehemu moja wanaweza kuwa watu zaidi ya mmoja. Mwishoni watatoa alama kulingana na uwezo wake. Kwa mfano namba 1 itamaanisha uwezo mdogo na namba 10 itamaanisha uwezo mkubwa kabisa.

 

Angalia mfano

Mhusika

Suala/ndoto husika

Wajibu wake kufikia ndoto

Uwezo

wake

Mtendaji

Kuunda kamati ya ulinzi na

usalama

Kuweka mipango ya wananchi

10

 

 

Kuitisha mkutano wa kijiji kujadili

masuala ya ukatili wa kijinsia

 

Mwenyekiti wa

ulinzi na usalama

Kukomesha vitendo vya ukatili

Kurudisha ulinzi shirikishi

 

Kuhakikisha kuwa kamati ya ulinzi

10


 

 

inafuatilia matukio yote ya ukatili

na kuyaripoti

 

Mzee wa mila

Kuondoa mila zote kandamizi

Kuitisha kikao cha wanamila, mangariba na makungwi ili

kuajdili mila kandamizi nk.

8

 

Baada ya kufanya hivi, makundi yatapitia na kukubaliana kwa pamoja. Ikiwa muda hautoshi waraghibishi watapitia na kuweka majumuisho pamoja na kisha kurudisha nakala kwa uongozi wa kijiji kwa ajili ya utekelezaji.

 

Wakati wa mkutano wa mrejesho kijijini, wanajamii watachagua timu ya wawakilishi kwa ajili ya mrejesho kwnye ngazi ya halmashauri. Wawakilishi watapata nafasi ya kukaa na waraghbishi na kuandaa mrejesho wo kwa kuangalia masuala wanayotaka kuongea na viongozi wa serikali ambayo yanahitaji kushughulikiwa na pia wanaeleza kuhusu hatua wanazopanga kuchukua.

 

Wakati wa mrejesho wa Halmashauri, waraghbishi (wanajamii) wataomba kukutana na Mkurugenzi wa Halmashauri pamoja na wakuu wa idara husika.

No comments:

Post a Comment