Wednesday, August 17, 2022

Hali ya ushiriki wa wanawake kwenye Kilimo Tanzania

 

Ushiriki Katika Kilimo


Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia (2000) iliweka mkazo katika kuongeza ushiriki wa wanawake katika kilimo ambacho ni uti wa mgongo na njia ya kujikimu kimaisha kwa wananchi wengi hususan wanaoishi vijijini. Jitihada mbalimbali zimefanyika katika kuboresha sekta ya kilimo ikiwa ni pamoja na: Kuunganisha kilimo na usalama wa chakula na lishe ili kukabiliana na tatizo la lishe duni kwa kuzingatia programu ya Lishe na Usalama wa Chakula; na utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Lishe; Utekelezaji wa programu ya Feed the Future, Bread Basket Initiative; Programu ya Kuboresha Miundombinu ya Masoko na Kuongeza Thamani na Asasi ya Huduma Ndogo za Kifedha Vijijini (Rural Finance Support Program); Kuboresha Maisha ya wafugaji kupitia programu ya Maendeleo ya Sekta ya Mifugo (2008) na kuandaa Sera ya Masoko ya Bidhaa za Kilimo (Agricultural Marketing Policy). Jitihada nyingine ni pamoja na uanzishwaji wa programu zifuatazo: Ukanda wa Ukuaji wa Kilimo Kusini mwa Tanzania - SAGCOT; MKUKUTA Iⅈ Kilimo Kwanza; Mradi Shirikishi na Uwezeshaji wa Maendeleo ya Kilimo - PADEP; na DADIP ambazo zimeimarisha huduma za ugani kwa wakulima kupitia mashamba darasa na vituo vya kata vya maarifa na taarifa za kilimo; Kuongeza idadi ya zana za kilimo kwa wakulima wadogo mfano trekta za mikono (power tillers); na Kuwajengea uwezo wakulima, Asasi za Wakulima, Sekta Binafsi, watoa huduma na Maafisa Ugani.

 

Sekta ya kilimo bado inakabiliwa na changamoto licha ya juhudi kubwa za serikali na wadau. Changamoto hizo ni pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi, uzalishaji mdogo kutokana na matumizi ya teknolojia duni za kilimo, ujuzi mdogo kwa wakulima na ukosefu wa masoko na taarifa za masoko. Kutokana na kutokuwepo kwa usawa wa kijinsia, wanawake tofauti na wanaume, wana fursa finyu ya kupata mikopo na ujuzi. Hali hii inasababisha wanawake washindwe kuajiri na kuwekeza kwenye kilimo cha mazao yenye thamani kubwa. Aidha, uwezo wa wanawake kumiliki rasilimali za uzalishaji kama vile ardhi ni mdogo. Hivyo, wanawake wakulima humiliki wastani wa ukubwa wa shamba la asilimia 40 tu ambayo inazalisha mazao kidogo. Matokeo ya utafiti wa Sensa ya Kilimo iliyofanyika 2019/20 yanaonesha kuwa kati ya kaya 12,007,839 Tanzania, kaya 7,837,405 (65.3%) zinajihusisha na shughuli za kilimo. Kwa upande wa Tanzania bara, kati ya kaya 7,657,185 (65.7%) zinazojihusisha na kilimo, kaya 4,972,372 (64.9%) zinalima mazao, kaya 2,526,846 (33%) mazao na ufugaji na kaya 157,290 (2%) zinajishughulisha na ufugaji pekee.

 

Serikali ina jukumu la kushirikiana na wadau kuhamasisha masuala ya kijinsia katika sekta ya kilimo ili kuhakikisha kuwa wanawake na wanaume wanapata haki sawa. Uboreshaji wa miundombinu ya kilimo vijijini (barabara, miundombinu ya umwagiliaji na mifumo ya TEHAMA) unapaswa kuimarishwa ili kuongeza tija kwa wakulima wa vijijini na kuboresha usalama wa chakula na lishe. Upatikanaji wa huduma za kifedha (mikopo na ujuzi wa usimamizi wa kifedha) kwa wakulima wanawake wa vijijini ni lazima ziboreshwe ili kutoa fursa zaidi za kupanua uwekezaji wao wa kilimo ili kuongeza kipato zaidi.

No comments:

Post a Comment