Tuesday, August 23, 2022

Sensa 2022: Takwimu za Kijinsia kwa ajili ya maendeleo shirikishi

 UCHAMBUZI: 

Takwimu za Kijinsia  kwaajili ya maendeleo shirikishi

 

Mara kadhaa wachambuzi na wadau wa Haki za wanawake, Usawa wa Kijinsia na Haki za Binadamu wamekuwa wakisisitiza serikali kutenga bajeti kwa mrfengo wa Kijinsia ili kukidhi mahitaji ya makundi yote.

Suala kubwa katika usawa wa Kijinsia na Bajeti ni mgawanyo wa rasilimali zote zilizoko katika nchi kwa kuzingatia mahitaji ya watu wote yaani (wanawake, wanaume, watoto wa kike na kiume, wazee, watu wenye ulamavu na watu wanaoishi pembezoni kwa kuokota matunda na kuwinda).

Wakati huu wa zoezi la kuhesabu sense ya watu na makazi, ni muhimu kila mtu kutambua kwamba, ushiriki kamilifu kwenye zoezi hili, kwa kutoa taarifa sahihi za makundi haya kutawasaidia watunga sera, waandaji wa bajeti kupanga kwa kuzingatia idadi ya watu waliopo.

Takwimu za kijinsia ni muhimu katika kuwaongoza waandaaji wa mipango na wafanya maamuzi kufahamu hali halisi ya kijinsia na hivyo kuweza kuandaa majibu sahihi ya changamoto zilizopo.

 Takwimu hizi zinapatikana kutoka katika vyanzo mbalimbali na vilevile zimesambaa na hivyo kuwa vigumu kupatikana kwa taarifa kutoka katika vyanzo vyote. Serikali pamoja na Asasi za Kiraia (AZAKI) na wadau wengine hukusanya takwimu zilizochambuliwa kijinsia, zikihusisha idadi ya watu, masuala ya afya, maendeleo ya jamii, kilimo, uchumi, elimu, huduma za jamii, mazingira, na taarifa kuhusu ajira.

Takwimu hizi hukusanywa kupitia sensa ya watu na makazi, tafiti na takwimu za kiutendaji. Nyaraka nyingine nyingi zimebainika kuwa na taarifa muhimu za kijinsia kwa ajili ya uandaaji wa sera na programu.

Aidha, nyaraka nyingine zimeonekana kutokuwa na taarifa toshelevu za kijinsia na hazijumuishi masuala mapya kuhusu hali ya wanawake na usawa wa kijinsia.

Katika muktadha huu, upo umuhimu wa kujenga uelewa wa masuala ya takwimu kwa sekta zote kuanza kukusanya na kuchakata takwimu kwa kuzingatia masuala ya kijinsia kutekeleza mpango wa ufuatiliaji na tathmini wenye mtazamo wa kijinsia.

Serikali yetu ipo kwenye mchakato wa kupitia sera ya   Jinsia na Maendeleo ya Wanawake ya mwaka 2000 ambayo sasa takwimu za sense ya mwaka 2022 zitawezesha sera kukamilika vizuri ikiwa na takwimu sahihi.

Ni jukumu la kutambua kuwa Hii itasaidia kuhamasisha ufuatiliaji wa mara kwa mara wa sera za kisekta, miradi, programu na mipango kwa ufanyaji wa maamuzi yenye tija



Pata Elimu juu Ubakaji- SMAUJATA

 *UBAKAJI*

*ELIMIKA NA SMAUJATA*πŸ‡ΉπŸ‡ΏπŸ’ͺ

   Ubakaji ni Tendo la kutumia Nguvu Katika Ngono ambapo mbakaji anatumia Nguvu kutekeleza kitendo hicho. Ama ubakaji  ni Ngono isiyo ya hiari.Kama mtu hayupo hiari na analazimishwa kufanya Hivyo hii inahesabiwa kama ubakaji hata kama anaekulazimisha ni rafiki, ndugu, jirani, mume au mtu usiyefahamiana nae.


    Ingawa Kwa kawaida ubakaji unafanyika dhidi ya wanawake lakini unatokea pia dhidi ya wanaume mbali ya watoto na watu wenye Ulemavu wa akili wasio elewa kinachoendelea.

 Ubakaji unaweza kutumiwa Nguvu ya mwili lakini pia mamlaka,vitisho na nitukio baya kabisa la kikatili Kwa nafsi ya mhanga na pengine Kwa afya yake linaloweza kumuathiri maisha yake yote kama si kusababisha kifo chake hasa likifanywa na watu kadhaa Kwa pamoja.


Matukio ya namna hiyo yanazidi kutokea hata ndani ya ukoo na mengi hayaripotiwi Kwa polisi,yakiwemo yanayotokea Magerezani kati ya watu wa jinsia Ile Ile.

Kwa vyovyote mara nyingi watu wanaobaka ni watu wanaojulikana sana na mhanga.Ubakaji hautokani na tamaa.


Matendo haya hayakubaliki iwe Serikalini,Magereza,Majumbani, kwenye jamii hata vitani,sheria za kimataifa haziruhusu matendo hayo ya kinyama na kikatili Vitani.


SABABU YA UBAKAJI

1.Ushirikina 

Mara nyingi ubakaji unafanywa na mtu anaeambiwa na Waganga wa jadi Kwa lengo la Fulani,mfano Kubaka mtoto kama Njia ya kupona ukimwi,Kubaka mtu mwenye Ulemavu Kwa lengo la kupata Mali na Utajiri nk jambo ambalo si kweli na niukatili mkubwa sana.

2.Ulevi

Ulevi kupindukia hupelekea Mwanaume au mwanamke kufanya kitendo Cha ubakaji Kwa mfano baba kumbaka mtoto wake,ama mama kumbaka mtoto wake wakiume, yote hii nikutokana na kunywa pombe kupindukia na kutokujizuia mihemko iliyotokana na ulevi.

3.Mila zisizo faa

Baadhi ya makabila  huamini kua mwanamke Hana kauli mbele za wanaume jambo ambalo kumpelekea mwanamke kulazimishwa kufanya kitendo Cha Ngono bila kuridhia kwani pale ambapo mwanaume anamuhitaji kiunyumba Naye bila ya kujiandaa nakujikuta alishaingiliwa pasi na kuridhia.

4.Maadili

Mmomonyoko wa maadili Kwa baadhi ya watoto wa kike na wakiume hupelekea mbakaji kufanya vitendo vya kibakaji ambapo,

Baadhi ya watoto wa kike kuvaa nguo zisizo kua za heshima Kisha kukatiza mbele ya wanaume hupelekea wanaume kupata mihemko na kumfanyia ubakaji binti alovaa vazi ilo lisilo na maadili.Pia wanaume kuvaa Nguo zisizo faa (mlegezo)jambo ambalo hupelekea kufanyiwa ubakaji.hata hivyo uvaaji wa nguo hizo Haina maana ya Moja kwa moja kua ndio chanzo Cha kufanyiwa ubakaji.

5:Wazazi kutosimamia malezi.

Hii huchangia kiasi Kikubwa Cha mtoto kufanyiwa ubakaji kwani wazazi siku izi wamekua wakiacha watoto muda mrefu Kwa madai yakua wanatafuta ridhki bila ya Kujua huku nyuma mtoto anafanyiwa Ukatili wa ubakaji na kupelekea mtoto kupata madhara makubwa sana.


MADHARA YA UBAKAJI

1:Kifo.

Ubakaji humfanya mhanga ajiuwe kwani huathirika kisaikolojia na Kuona Kwamba Hana Tena thamani kutokana na kitendo alicho fanyiwa

2:dharau Kwa wanawake

Mwanamke aliebakwa kudharauriwa na kushushwa uthamani wake hata baadae anapoitaji kuolewa Inapelekea kuonekana kwamba Hana thamani Kwa kubakwa kwake.

3:magonjwa ya zinaa,kama ukimwi,kaswende nk kwani mhanga hupata michubuko kutokana na kuingiliwa bila ridhaa yake Kwa Nguvu.

4:mimba zisizo Tarajiwa,


NINI KIFANYIKE KUKOMESHA UBAKAJI 

1:Elimisha kizazi

Iwe Jukumu letu kuhamasisha wanawake wanaotetea haki za wanawake wa siku zijazo.pinga mitindo iliyokaririwa ya Kijinsia na maoni ya vurugu ambayo watoto kupatana nayo kwenye vyombo vya Habari,barabarani na mashuleni, watoto wako wajue kwamba familia yako ni nafasi salaama kwao kujielezea walivyo,sisitiza uamuzi wao uwafundishe umuhimu wa ridhaa ktk umri mdogo.

2:Anzisha mazungumzo na familia yako na marafiki kuhusu jinsi mnavyoweza kufanya kazi pamoja kumaliza utamaduni wa ubakaji Katika jamii zenu.

3:Usifurahie ubakaji

Ubakaji sio jambo la kuchekesha ,utani hivyo Jitahidi kutoharirisha unyanyasaji wa kijinsia hivyo kua ngumu Kwa waathirika kusema wakati idhini Yao inakiukwa.utani unaohalalisha dhuluma ya Kijinsia Haikubaliki kashifu.

 4:Ubakaji unaoendelezwa na kutokuwepo au ukosefu wa utekelezaji wa sheria zinazoshughulikia Ukatili dhidi ya wanawake na sheria za kibaguzi ya umiliki Mali,ndoa,talaka na utunzaji wa watoto.

5.Wazazi tutenge muda wa kuwalea watoto wetu kwani Kwa kufanya Ivyo tutakua nao karibu na kuweza kuwapa elimu zaidi kwani mwalimu wakwanza Kwa mtoto nimzazi hivyo tupate muda wa kukaa na watoto wetu 

 

KWA MSAADA ZAIDI YA WAHANGA WA UKATILI

Piga simu namba 116 Bure 

Toa taarifa kwa Maafisa Ustawi,Dawati la jinsia, police,ofisi za Serikali ya mtaa,

Toa taarifa kwa Mashujaa wa maendeleo SMAUJATA

Mhanga akimbizwe hospital mara moja kwa ajili ya matibabu na Vipimo.


Imetayarishwa na

Mwamini Samaje

Idara ya Habari mawasiliano na Hamasa SMAUJATA Taifa



*KATAA UKATILI WEWE NI SHUJAA*πŸ’ͺπŸ‡ΉπŸ‡Ώ

Saturday, August 20, 2022

Yajue Malengo Makuu ya SMAUJATA

 πŸ‡ΉπŸ‡Ώ


MALENGO MAKUU YA SMAUJATA* 


1. Kushirikisha Jamii katika kuainisha fursa na changamoto 

zinazoikabili ili kulijiletea Maendeleo


2. Kuelimisha Jamii kuondokana na Fikra, Imani, Mila, Desturi 

na Tamaduni Zinazokinzana na Maendeleo


3. Kushirikisha Jamii katika Kuiunganisha na Kuiwezesha katika Mchakato wa Maendeleo ili 

kuinua ustawi wake.


4. Kuratibu Utekelezaji na Uzingatiaji wa Masuala ya Jinsia 

Katika Programu na Mipango ya Maendeleo Katika Sekta

Mbalimbali


5. Kuwezesha Jamii Kutumia Fursa ya Sera za Kisekta na 

Mikakati yake katika Kujiletea Maendeleo.


6. Kutoa Elimu Kwa Jamii Kupitia Semina, sanaa, Warsha , Makongamano, Vyombo vya Habari, Matembezi ya Amani , Vipeperushi Kuhusu Haki,  usawa, Fursa na Sera  mbadala kwa Maendeleo Endelevu na Kuiwezesha Jamii Kutekeleza Haki na Malezi ya Mtoto


7. Kuibua, Kuendeleza na Kukuza Vipaji Mbalimbali katika Ujuzi, Utaalamu na Ubunifu ili Kujenga Kizazi chenye Uwezo wa Kujitegemea.


8. Kushirikiana na Serikali, Wananchi,  Wadau mbalimbali Kutoka Ndani na nje ya Nchi katika Shughuli za  Utoaji wa Elimu na Fursa za Maendeleo. 


9. Kupokea Mbinu wezeshi, Maoni na Mawazo Mapya kutoka Makundi mbalimbali ya Wadau na Kuishauri Jamii na Serikali  katika Kuboresha na Kufanikisha Vipaumbele vya Ustawi na Maendeleo ya Jamii.


10. Kufanya Shughuli zingine Zozote zinazohusu Maendeleo na Ustawi wa Jamii.

Thursday, August 18, 2022

Mchakato wa Mabadiliko Binafsi katika uongozi wa kifeminia

 

Mchakato wa Mabadiliko Binafsi katika uongozi wa kifeminia 

na deogratius Koyanga 

Makala ya Valerie Miller na VeneKlasen (2012) Imebainisha kanuni nne za kuzingatia kwenye mchakato wa mabadiliko binafsi kwa wanaharakati watetezi wa haki za wanawake. Katika harakati kuna uongozi, uongozi ili uwe na ufanisi na ulete mabadiliko, unahitaji mabadiliko binafsi ya kiongozi. Kiongozi awe na mtazamo chanya, abadilishe mtazamo wake wa awali kabla ya kuwa mwanaharakati, na pia aweke misingi ya kutaka kuona mabadiliko chanya yatakayosababishwa na yeye. kwahiyo hapa ni lazima abadilike.  Valerie na veneKlasen, wanandika hizi kanuni ambayo zitatusaidia kubadilika sisi kwanza: 

Kanuni ya Kwanza ni: Ujuzi na Ufahamu muhimu

Waandishi hawa wanadai kwamba elimu na maarifa ya itikadi ya ukombozi wa mwanamke inaanza kwenye maisha halisia ya mwanamke anayopitia kwenye safari ya mabadiliko.

Maarifa haya hayapatikani kwenye darasa rasmi, bali yanatokana na uzoefu unaoanza kwa kujiifunza kuhoji mambo yalivyo “kawaida” Mifano ya maswali ni kama haya

 

Mchakato wa kuanza kuhoji ubaguzi na mifumo kandamizi humjengea mwanamke yoyote ufahamu na hamasa kubwa ya kutamani mabadiliko .

Makala za Valerie Miller na VeneKlasen (2012) zimebainisha viwango vya ufahamu vinavyochochea wanawake na hasa viongozi kuchukua hatua za kudai na kufanya mabadilko wanapopata fursa ya kushika usukani wa uongozi.

 

Kanuni ya 2: Kuhakikisha na Kujenga Juu ya Ufahamu wa Wwanawake na Roho (Validating and building on women’s knowledge and spirit)

Katika safari ya kujenga uelewa na ufahamu binafsi, lazima mwanaharakati afike mahali ambapo anajenga imani na ile ajenda bila wasiwasi au mashaka. Kwenye ngazi hii kunahitajika wingi wa watetezi wenye   uelewa wa muktadha na mifumo kandamizi ili iimarishe uelewa na ufahamu (knowledge and consciousness raising). mambo ambayo yanawezesha kuhakikishia misimamo iliyochukuliwa na mielekeo ni pamoja na kusoma kumbukizi za wapambanaji, mashairi, nyimbo na sanaa zinazoimarisha uelewa kukuza hamasa  na kuhakikisha  misimamo ya binafsi na mielekeo.

Kanuni ya 3. Kuelewa na kutafakari suala la mamlaka (Understanding and navigating power).

Uwezo wa mwanaharakati kujenga uelewa wa jinsi mamlaka(nguvu) ndani ya jamii ya mfumo dume inavyofanya kazi ni nyenzo muhimu ya kumwezesha kuungana na wengine katika kujenga mikakati ya kuvunja hizi nguvu na kujenga njia mbadala ya kutumia nguvu zilizoko kwenye nafsi zao (power within)

Wachambuzi wa jinsi mamlaka (power) inavyofanya kazi ndani ya jamii wamebainisha njia mbili. Kwanza kwa njia inayoonekana (visible power), ikiwa ni pamoja na sheria, sera zinazohalalisha ubaguzi wa jinsia. Mamlaka au nguvu iliyojificha (invisible power) Wenye mamlaka kama viongozi wa dini, matajiri wa dunia na taasisi zinazowalinda kama Benki Kuu ya Kimataifa, Shirika la Biashara la Kmataifa,  vina uwezo wa kuumba? au kujenga ajenda za kisiasa zinazolinda maslahi yao. Kwa mfano sera za kubinafisisha huduma za jamii, sera za soko huria zote hizi zinalinda maslahi ya mabepari, zinawakandamiza maskini na mafukara wa dunia na kuwabebesha wanawake mzigo wa ziada kwenye shughuli za kuendeleza kizazi na nguvu kazi.

Uelewa wa jinsi nguvu hizi zinavyofanya kazi huwezesha mwanamke mmoja mmoja kuona umuhimu wa kuunganisha nguvu zake kujenga mshikamano wa kupambana na hizi nguvu kandamizi.

Kanuni ya 4 - Kujitunza (Moyo, akili-mwili) (Self-care - Heart-mind-body)

Afya ya kiongozi ni rasilimali kwake, kwa familia, kwa shirika au asasi anayoongoza na kwa tapo la utetezi wa haki za wanawake kimapinduzi. Mara nyingi shughuli za uanaharakati ni kazi inayotumia nguvu nyingi ya kimwili, kiakili,  kifikra na hata kiroho. Shughuli hizi ukiunganisha na shughuli nyingine za uzalishaji (productive) na za kuendeleza kizazi (reproductive) zinaweza ziwe na athari kubwa kwenye afya ya hisia (emotional health), afya ya mwili (physical health) na afya ya akili (mental health).Umuhimu wa kujali afya ni sehemu muhimu za uanaharakati  wa mapambano dhidi ya mifumo kandamizi..

 

Misingi Binafsi inayomwongoza kiongozi wa harakati za utetezi wa wanawake kimapinduzi

 

Ø    Hii inamaanisha kwamba, kiongozi wa harakati za ukombozi wa wanawake kimapinduzi ni yule mwenye kuamini na kuongozwa na  misingi ya usawa, na  ukombozi wa wanawake kimapinduzi.

 

Ø    Ni kiongozi anaehamisika na uelewa wa itikadi na mwenye utayari wa kujiimarisha kwenye uelewa huu ili aweze kujenga mazingira wezeshi ya kujifunza pamoja (shared learning).

Ø    Mwenye dhamira ya kuweka mifumo mibadala ya uongozi itakayowezesha ushiriki wa pamoja katika kujenga ajenda ya pamoja, kujadili, kuendeleza na kutetea ajenda ya ukombozi wa wanawake kimapinduzi.

Ø    Ni kiongozi mwenye dhamira, nia na uwezo wa  kuchambua hali halisi ya muktadha wa siasa na uchumi kwa kubainisha fursa na changamoto za kuendeleza harakati za utetezi wa haki za wanawake kimapinduzi.

Ø    Ni kiongozi mwenye uwezo wa kushirikiana na wenzake kubainisha mafanikio ya pamoja na mwenye utayari wa kuwajibika kutokana na makosa au mapungufu yatokanayo na maamzi ya pamoja (celebrate collective achievements and assume individual accountability on behalf of the collective).

Ø    Kiongozi mwenye uwezo na dhamira ya kujenga mahusiaono mbadala ndani ya shirika yenye kujali utu wa kila mmoja, wenye kusaidiana wakati wa shida na mwenye kutabiri viashiria vya kugawa nguvu za pamoja.

Ø    Ni kiongozi mwenye utayari wa kushikamana, kutandaa  na viongozi na mitandao yenye kuongozwa na misingi ya utetezi wa wanawake kimapinduzi kama mkakati wa ujenzi wa tapo la kusambaratisha mfumo dume.

Ø    Ni kiongozi mwenye upeo wa kuona mahusiano kati ya mfumo dume na mifumo mingine kandamizi inayotumia rangi, jinsi, tabaka, hali ya maumbile na ujinsia wa mtu kukandamiza na kuwabagua wanawake na watu waliko pembezoni.

Ø    Kiongozi mwenye dhamira na utayari wa kushirikiana na wengine katika kupambana na mifumo mingine kandamizi bila kupoteza ajenda ya ukobozi wa mwanamke kimapinduzi. 

Ø    Vilevile ni kiongozi mwenye nia na dhamira ya kushirikiana kwa kugawana majukumu na siyo kushindana.

Ø    Ni kiongozi anachukulia  cheo kama dhamana inayompa wajibu na siyo mamlaka ya kutawala na kumrisha.

Ø    Mwisho na siyo kwa daraja ni kiongozi mwenye kujali afya yake na ya wale anaowaongoza kama mkakati wa kujenga afya ya shirika na afya ya tapo.

Ø    Mwezeshaji ajumuishe akizingatia mwongozo wa Mkataba wa Kanini za Ukombozi wa Wanawake wa Kiafrika Kimapinduzi.

Ujenzi wa Mbinu za Uongozi wa Kifeministi (feminist leadership Styles)

 

Ujenzi wa Mbinu za Uongozi wa Kifeministi (feminist leadership Styles)

na deogratius Temba 

Zipo makala nyingi zinazozungumzia jinsi wanawake wanavyotumia mbinu tofauti kwenye uongozi. Inadaiwa kuwa, kutokana na jinsi zao, wanawake huwa na uwezo mkubwa wa kusikiliza, kupokea ushauri, kushawishi, kushirikisha, kusoma alama za nyakati na kutumia ubunifu kwenye kutatua migogoro.

 Baadhi ya mashirika makubwa ya binafsi wamegundua vipaji hivi na kuanza kuwateua wanawake kama wakurugenzi wa makampuni yao, jambo ambalo limewezesha kampuni hizi kuongeza faida kubwa kwenye uzalisaji wa bidha zao ( Tiffany Harper and  Hughey Gorge inapatikana https://womenlovetech.com/7-leadership-skills-ofpsucessful-women) .

 Vilevile Utafiti uliofanywa na Rusimbi M, Meena R na Carolyne I (2018) ulibainisha baadhi ya viwezeshi vinavyosababisha uongozi mbadala wa wanawake. Baadhi ya viwezeshi ilikuwa ni pamoja na vipaji binafsi (personal traits) ikiwa ni pamoja na msukumo na hisia za kutaka kuleta mabadiliko ya mfumo kwa haraka, ubunifu, uwezo wa kusikiliza na kukubali ushauri, uwezo wa kusoma alama za nyakati na urahisi wa kubadili mbinu bila kuyumbisha dira na uwezo wa kushirikiana na kuwa na mitandao wezeshi.

Uongozi wa wanawake unaangalia kwa haraka mahitaji ya watu, au mahitaaji ya msingi ya kijinsia kuliko yale ya jumla. Wakati mwingine, jamii inachukulia kwamba wanaangalia masuala madogo madogo sana, ila hayo ndiyo huchangia ufanisi kwa yale makubwa. Mfano, mahali pa kunyoneshea na kutunzia watoto kwa mfanyakazi anayenyonyesha ili aweze kukaa kazini kwa masaa mengi na kuongeza ufanisi. Ukilitangalia hili kwa haraka unaweza kuona kwamba ni jambo la wanaharakati wa haki za wanawake lisilo na mafanikio.

Swali : Je Mimi kama kiongozi natumia mbinu zipi za uongozi?Kuna fursa zipi za kuleta Mabadiliko ya Mbinu za Uongozi? Na Changamoto zipi?

Wednesday, August 17, 2022

Jinsia na Haki za Binadamu (Gender and Human Right

 

 Jinsia na Haki za Binadamu

Mfumo wa sheria wa Tanzania una jukumu muhimu katika kuhakikisha kwamba kuna utekelezwaji kamili wa haki za binadamu na kwamba kila raia anafurahia haki zake bila kuingiliwa. Serikali ya Tanzania imejitolea kukuza na kulinda haki za binadamu kwa kutekeleza mipango mbalimbali ya ndani na kimataifa. Ndani ya nchi Serikali imejitahidi kuwajengea uwezo maafisa wa mahakama kuhusiana na sheria za kimataifa za haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na haki za wanawake, katika muktadha wa CEDAW, itifaki yake ya hiari na Itifaki ya Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu na Haki ya Wanawake barani Afrika. Katika mwaka wa 2011, majaji 24 na wasajili wa Mahakama Kuu walipata mafunzo katika vyombo vya kimataifa vya haki za binadamu, hasa vinavyohusu wanawake na watoto. Vile vile, Serikali ilihakikisha kuwa haki za binadamu zinafundishwa katika shule zote za msingi na sekondari (kama mada katika uraia) na pia katika Vyuo vya Elimu ya Juu (HLIs), ikilenga kuwajengea kizazi kipya hisia ya kuheshimu haki za binadamu.

 

Serikali pia imeimarisha vifungu vya sheria kwa vitendo vya ubaguzi, ambavyo vinanyima haki za vikundi vingi vya kijamii kulingana na usawa wa kijinsia. Mifumo ya kisheria iliyoanzishwa imegawanyika katika sekta zote, na hivyo kufanya haki za binadamu kuwa suala  mtambuka. Sheria hizi ni pamoja na;  Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009; Sheria ya Kuzuia na Kudhibiti UKIMWI (Na. 28 ya mwaka 2008); Sheria ya Taifa ya Uchaguzi ya mwaka 1985 ambayo inakataza ubaguzi katika chaguzi; Sheria ya Masharti Maalum ya Makosa ya Kujamiiana (SOSPA) ya mwaka  1998 pia imejumuishwa katika Kanuni ya Adhabu; Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999, na Sheria ya Msaada wa Kisheria ya mwaka 2017. Mifumo hiyo kwa ujumla inasaidia ustawi wa wanawake kiuchumi na kijamii; inatoa ulinzi wa wanawake na watoto dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia katika mazingira mbalimbali; inajenga thamani na kuhakikisha wanawake wana haki ya kupata, kumiliki na kutumia ardhi kwa usawa na wanaume.

 

Hata hivyo, maendeleo yaliyopatikana, mianya ya kisheria na desturi za kimila mara nyingi hudhoofisha haki za wanawake. Wasichana bado wanaolewa chini ya umri wa miaka 18 na kama matokeo ya kuenea kwa mifumo ya sheria za kimila. Ripoti ya UNICEF (2016), inathibitisha kuwa kiwango cha ndoa za utotoni ni zaidi ya mara mbili ya wastani wa dunia wa  asilimia 13. Takriban asilimia 30 ya wasichana wenye umri wa miaka 15-19 ama wameolewa, wametalikiwa , wajane au wapo katika ndoa za kitamaduni na hawawezi kujihusisha na shughuli za uzalishaji mali. Vikwazo vingine ni pamoja na kushindwa kutekeleza likizo ya uzazi iliyoongezwa na muda wa kunyonyesha katika uchumi usio rasmi na sekta binafsi, pamoja na kuenea kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii nyingi nchini kote.

 

Serikali inapaswa kujitahidi kuimarisha ushirikiano wa sekta mbalimbali na ushirikishwaji wa sekta binafsi katika jitihada za kuboresha ulinzi wa haki za binadamu nchini kote. Jitihada pia zinapaswa kuwekwa katika: kurekebisha Sheria ya Ndoa Na.5 (1971) na sheria nyingine zinazohusiana na urithi, mirathi na haki za watoto pamoja na sheria nyingine za kibaguzi; kutoa mafunzo ya uhamasishaji wa Sheria zinazozingatia masuala ya kijinsia kwa maafisa wa utekelezaji wa sheria, wataalamu wa huduma za sheria na wadau wengine; na maandalizi ya nyenzo za mafunzo na kampeni kuhusu haki za kisheria za wanawake na kuzisambaza ipasavyo.

 


Hali ya ushiriki wa wanawake kwenye Kilimo Tanzania

 

Ushiriki Katika Kilimo


Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia (2000) iliweka mkazo katika kuongeza ushiriki wa wanawake katika kilimo ambacho ni uti wa mgongo na njia ya kujikimu kimaisha kwa wananchi wengi hususan wanaoishi vijijini. Jitihada mbalimbali zimefanyika katika kuboresha sekta ya kilimo ikiwa ni pamoja na: Kuunganisha kilimo na usalama wa chakula na lishe ili kukabiliana na tatizo la lishe duni kwa kuzingatia programu ya Lishe na Usalama wa Chakula; na utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Lishe; Utekelezaji wa programu ya Feed the Future, Bread Basket Initiative; Programu ya Kuboresha Miundombinu ya Masoko na Kuongeza Thamani na Asasi ya Huduma Ndogo za Kifedha Vijijini (Rural Finance Support Program); Kuboresha Maisha ya wafugaji kupitia programu ya Maendeleo ya Sekta ya Mifugo (2008) na kuandaa Sera ya Masoko ya Bidhaa za Kilimo (Agricultural Marketing Policy). Jitihada nyingine ni pamoja na uanzishwaji wa programu zifuatazo: Ukanda wa Ukuaji wa Kilimo Kusini mwa Tanzania - SAGCOT; MKUKUTA Iⅈ Kilimo Kwanza; Mradi Shirikishi na Uwezeshaji wa Maendeleo ya Kilimo - PADEP; na DADIP ambazo zimeimarisha huduma za ugani kwa wakulima kupitia mashamba darasa na vituo vya kata vya maarifa na taarifa za kilimo; Kuongeza idadi ya zana za kilimo kwa wakulima wadogo mfano trekta za mikono (power tillers); na Kuwajengea uwezo wakulima, Asasi za Wakulima, Sekta Binafsi, watoa huduma na Maafisa Ugani.

 

Sekta ya kilimo bado inakabiliwa na changamoto licha ya juhudi kubwa za serikali na wadau. Changamoto hizo ni pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi, uzalishaji mdogo kutokana na matumizi ya teknolojia duni za kilimo, ujuzi mdogo kwa wakulima na ukosefu wa masoko na taarifa za masoko. Kutokana na kutokuwepo kwa usawa wa kijinsia, wanawake tofauti na wanaume, wana fursa finyu ya kupata mikopo na ujuzi. Hali hii inasababisha wanawake washindwe kuajiri na kuwekeza kwenye kilimo cha mazao yenye thamani kubwa. Aidha, uwezo wa wanawake kumiliki rasilimali za uzalishaji kama vile ardhi ni mdogo. Hivyo, wanawake wakulima humiliki wastani wa ukubwa wa shamba la asilimia 40 tu ambayo inazalisha mazao kidogo. Matokeo ya utafiti wa Sensa ya Kilimo iliyofanyika 2019/20 yanaonesha kuwa kati ya kaya 12,007,839 Tanzania, kaya 7,837,405 (65.3%) zinajihusisha na shughuli za kilimo. Kwa upande wa Tanzania bara, kati ya kaya 7,657,185 (65.7%) zinazojihusisha na kilimo, kaya 4,972,372 (64.9%) zinalima mazao, kaya 2,526,846 (33%) mazao na ufugaji na kaya 157,290 (2%) zinajishughulisha na ufugaji pekee.

 

Serikali ina jukumu la kushirikiana na wadau kuhamasisha masuala ya kijinsia katika sekta ya kilimo ili kuhakikisha kuwa wanawake na wanaume wanapata haki sawa. Uboreshaji wa miundombinu ya kilimo vijijini (barabara, miundombinu ya umwagiliaji na mifumo ya TEHAMA) unapaswa kuimarishwa ili kuongeza tija kwa wakulima wa vijijini na kuboresha usalama wa chakula na lishe. Upatikanaji wa huduma za kifedha (mikopo na ujuzi wa usimamizi wa kifedha) kwa wakulima wanawake wa vijijini ni lazima ziboreshwe ili kutoa fursa zaidi za kupanua uwekezaji wao wa kilimo ili kuongeza kipato zaidi.

Nini Maana ya Uwezeshaji wanawake?

Uwezeshaji wa wanawake ni: 

 Mchakato wa kukuza uwezo wa wanawake kuchukua jukumu la maendeleo yao wenyewe, mchakato unahusisha kuwawezesha wanawake kufanya uchaguzi wao, kuwa na sauti katika maamuzi yanayowahusu, uwezo wa kuanzisha hatua za maendeleo, mabadiliko ya mitazamo, na kuongezeka kwa ufahamu wa upatikanaji sawa. na udhibiti wa rasilimali na huduma ili kuchukua jukumu la fursa zao

Nini Maana ya Majukumu ya Kijinsia?

 Majukumu yaliyoandaliwa na kubainishwa kijamii kwa mfano, kulea mtoto ni jukumu la jinsia ya kike badala ya jukumu la jinsi ya kike kwani linaweza kufanywa kwa usawa na wanaume au wanawake. Tofauti na majukumu ya jinsi, majukumu ya kijinsia hayafanani maeneo yote duniani wote na hutofautiana katika maeneo tofauti kwa kuzingatia muda. Pia inaweza zikakubadilika na kubadilishana.



Sunday, August 14, 2022

DHANA YA UONGOZI KATIKA MTAZAMO WA KIJINSIA (Uongozi wa kifeminist)

 

Uongozi 

na deogratius temba

Uongozi ni  dhana inayotumika kuelezea sifa za  wenye mamlaka na maamuzi katika nafasi mbalimbali. Dhana hii inapotumika kueleza sifa   za uongozi uliojikita kwenye misingi ya  mfumo dume, dhana huonesha  tabia ya wenye mamalaka  ya kandamizi, kutawala, kuamirisha na kuhodhi maamuzi ya mwisho.

Uongozi uliojikita kwenye itikadi ya kifeministi  ni dhana yenye kuonesha sifa na tabia za mtu au watu waliokabidhiwa mamlaka wenye kuamini katika haki za wanawake na makundi yalioko pembezoni, ni uongozi ushirikishwaji wa wengi kwenye  kupanga, kutatua matatizo hatimaye  uongozi unabebeshwa wajibu wa kufanya maamuzi na kuwajibika pale kwa matokeo hasi au chanya.

Ø     Uongozi unahusu matumizi ya mamlaka , ni jinsi gani mamlaka inatumiwa aidha kukandamiza au kuwezesha

Ø     Uongozi wa Kifeministi unahusu uwezo wa kuchambua na kuelewa hali halisi, kuwa na maono, na dira ya ukombozi wa wanawake kimapinduzi. Tafsiri zinazojikita kwenye tabia ya uongozi zinabainsiha kiongozi bora kama mtu mwenye uwezo wa kuonyesha njia, kufanya maamuzi, kutafsiri maono na ndoto za shirika, kuhamisisha wengine kuamini kwenye ndoto na kuweka mikakati ya kutekeleza ndoto na maono ya shirika/taasisi

Ø     Uongozi unahusu matendo. yenye kuongozwa na dhima ya maadili na heshima kwa wanawake, watoto na watu wenye changamoto. Tafsiri hii ni ile inayobainisha mchakato na matendo ya pamoja yenye kuwezesha mabadiliko yaliyobuniwa pamoja. Tafsiri hii inabainisha uongozi kama mtu au watu wachache wenye kushirikiana na wengine katika kuleta mabadilko ya mfumo  ( transformational leadership)

Uongozi wa mabadiliko ya kifeministi (Feminist transformational leadership)

 


na deogratius temba

Uongozi wa mabadiliko ya kifeministi ni dhana inayotumika kuelezea vitendo na Imani ya viongozi wenye kuamini kwenye misingi ya usawa wa jinisia na wenye nia ya kuwezesha mabadiliko ya mifumo ya uongozi yanayoweza kujenga msingi ya kulinda haki za wanawake na wasichana na makundi mengine yallioko pembezoni. 

Ni uongozi utakaoleta au kuwezesha mabadiliko ya mifumo na tamaduni za kukandamiza jinsi moja hususan wanawake na wasichana. Mabadiliko hayo yakilenga kwanza watu binafsi kuhusu fikra na vitendo vyao vinavyoashiria kuhalalisha ukiukwaji wa haki za wanawake. Mabadilko ya kitaasisi na mifumo yake ya uwajibikaji ili kujenga misingi ya kuheshimu utu na heshima wa kila mmoja.

 Ni uongozi unaotambua kwamba wanawake na wanaume ni sawa kama binadamu lakini wana mahitaji tofauti kutokana na tofauti za kimaumbile na tofauti zilizojengwa na jamii kuhusu tafsiri ya nini maana ya kuwa mwanamke au mwanaume katika ufikiaji wa huduma, rasilimali, uhuru wa kuamua, umilki wa miili yao na stahi zao za maisha. 

Ni uongozi wenye kudhamiria kujenga utamaduni wa kitaasisi, kishirika na hata kwa mtu binafsi utakao heshimu utu na haki za mwanawake, wasichana na watu wenye ulemavu. 

Pamoja na kuzingatia misingi ya utawala bora kwa maana kwamba ni uongozi ulio wazi, wenye kuongozwa na uwajibikaji wenye mrengo wa jinsia.  

Kwa kifupi ni uongozi wenye azma ya kuleta mabadiliko ya kimapinduzi katika mifumo kandamizi hususani mfumo dume. 

Uongozi wa kifeministi ni ule unaowezesha mwenye mamlaka kuona, kutambua na kuchukua hatua za kuwezesha watetezi wa haki za wanawake kimapinduzi kuunganisha nguvu ili kuleta mabadiliko ya mifumo kandamizi katika Nyanja mbalimbali za maisha.

Dhana ya Ukombozi wa Mwanamke Kimapinduzi

 


Ukombozi ni mchakato wenye kumwezesha mtu kujinasua kutoka minyororo inayomnyima haki ya kujithamni na kuthaminiwa na wengine, haki ya kuulindwa utu wake, haki ya kusikilizwa na kuzikiliza, haki ya kumiliki mwili wake, haki ya kushiriki katika uongozi wa jamii yake, yaki ya kushiriki na kufaidi matunda yatokanayo na jasho lake, haki ya kufikia na kunufaika rasilimali ya taifa lake. Ukombozi wa mwanamke kimapinduzi ni hali na mchakato uliyomwezesha mwanamke kujinasua kutoka minyororo ya mifumo kandamzi inayombagua na kumsabilishia kukosa haki na stahiki sawa kama mwanaume. Mchakato huu unaanza kwenye ngazi ya kujitambua na kukataa ubaguzi wa aina yoyote, kukataa fikra mgando zinazohalisha ubaguzi wa jinsia, kujiunga na wengine kwenye harakati za kusambaratisha mfumo dume.  

Ufeminist (Ukombozi wa mwanamke Kimapinduzi)

Kuhusu dhana ya Ufeministi

Ufeministi ni dhana inayobeba mambo mengi ikiwa ni pamoja na aina nyingi za misimamo, itikadi na harakati tofauti zinazochangia kwenye azma ya kutetea haki za wanawake dhidi ya ubaguzi wa jinsia katika nyanja za siasa, uchumi na ustawi wa jamii

Ufeministi kama itakavyotumika kwenye nyaraka na machapitisho mengi, ni itikadi inayoongozwa na Imani kuhusu usawa wa wanawake na vitendo vinavyoashiria kutokomeza mifumo inayobagua wanawake kwenye nyanja zote za uchumi, siasa na hata ustawi wa jamii. Ingawaje kuna misimamo na mirengo inayotafautiana kwenye ufafanuzi wa dhana hii ya ufeminist, kuna mambo ya msingi yanayowaunganisha wanaharakati wote watetezi wa haki za wanawake kimapinduzi.

Dhana ya kifeminist ni kutetea haki na usawa kwa wote bila ubaguzi. kuhakikisha mifumo, miundo na rasilimali zinalenga kujenga jamii yenye usawa bila ubaguzi au unyanyasaji.  ufeminia, sio kitu kibaya au sio watu wanaokwenda kinyume na maadili au mila na desturi nzuri isipokuwa Mfeminia hawezi kukubaali kunyamaza akiona mila, desturi, mfumo unamkandamiza mwingine. 

Ubaguzi wa Kijinsia.

 


Ubaguzi wa kijinsia hutokana na hali ya kupendelea jinsi moja na kunyima haki au stahiki jinsi nyingine. Kwa mfano, ubaguzi huu unaweza kuwa katika utoaji wa huduma tofauti, au haki tofauti ambazo hazizingatii misingi imara, ya ujenzi wa usawa kati ya wanawake na wanaume. Katika jamii nyingi nchini, hali hii ya ubaguzi wa kijinsia, hujitokeza kwa mfano katika ubaguzi wa muundo wa kijinsia dhidi ya wanawake kuhusiana na mapato, ufikiaji wa huduma na raslimali na kushiriki katika maamuzi nyeti yanayohusu maisha yao na ya kijamii.

Maana ya Mapengo ya Kijinsia

 


Mapengo ya Kijinsia hutokea pale ambapo tafsiri za jamii kuhusu haki, wajibu na majukumu inaashiria kujenga tabaka au mapengo kati ya mwanamke na mwanaume katika ngazi mbalimbali. Mapengo haya ya kijinsia hupelekea kuwepo kwa tofauti ya ufikiaji wa rasilimali kama vile umiliki wa ardhi, nyumba, biashara, tofauti za mishahara, ufikiaji wa huduma za msingi kama elimu, bima ya afya, nk. Vilevile mapengo ya jinsia huonekana kwenye mgao wa uzito wa kazi, haki na ule wa mapato. Kwa ufupi, mapengo ya kijinsia hutokea pale ambapo kumekosekana haki (social justice) kati ya mwanamke na mwanaume na hivyo kusababisha ubaguzi wa jinsia na uwiano usio sawia kati ya mwanamke na mwanaumme kwenye nyanja zote za maisha.