** Hedhi Salama: Muheza Yaendelea Kufanikiwa Baada ya Utekelezaji wa
WASH**
Na Deogratius Koyanga
Upatikanaji wa huduma za hedhi salama umeleta mabadiliko makubwa kwa
wasichana shuleni, ukirejesha tabasamu na kuwapa fursa ya kushiriki kikamilifu
katika masomo yao.
Mwongozo wa serikali juu ya Maji, Afya na Usafi wa Mazingira wa mwaka 2016
unatoa maelekezo kwa wadau mbalimbali kuhakikisha ujenzi wa miundombinu ya
hedhi salama mashuleni ili kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa watoto wa
kike. Kupitia mwongozo huu, kila Halmashauri inapaswa kutenga bajeti kila mwaka
wa fedha ili kuhakikisha changamoto zinazotokana na ukosefu wa huduma bora za
Maji, Afya na Usafi wa Mazingira (SWASH) zinatatuliwa na hivyo kuimarisha
kiwango cha elimu.
Serikali ya Tanzania kupitia hotuba mbalimbali za viongozi wake imekuwa
ikisisitiza umuhimu wa bajeti kwa ajili ya huduma za hedhi salama. Rais Samia
Suluhu Hassan katika moja ya hotuba zake aliwahi kusema, "Tunahitaji
kuhakikisha kuwa hakuna msichana anayekosa shule kwa sababu ya hedhi. Serikali
itaendelea kuweka mkazo katika bajeti ya elimu na afya ili kuboresha mazingira
ya watoto wa kike." Aliyekuwa Waziri wa Afya Ummy Mwalimu, pia alisisitiza kuwa mpango wa bajeti ya taifa
unahakikisha kuwa shule zinatengewa fedha za kuboresha miundombinu ya afya na
usafi wa mazingira.
Katika utekelezaji wa mwongozo huu, Mtandao wa Jinsia (TGNP) kwa
kushirikiana na Shirika la ONGAWA na Halmashauri ya Wilaya ya Muheza
walitekeleza mradi wa Maji, Afya na Usafi wa Mazingira (WASH) mwaka 2022 katika
ngazi ya kaya na shuleni, huku suala la hedhi salama likipewa kipaumbele ili
kuwawezesha wasichana kuhudhuria masomo yao bila kikwazo. Ingawa mradi huo
umekamilika, ufuatiliaji wa hivi karibuni umebaini mafanikio makubwa
yanayoendelea kuwanufaisha wasichana na jamii kwa ujumla.
Utafiti wa awali wa serikali wa mwaka 2009 kuhusu hali ya SWASH ulionyesha
kuwa hali ya Maji, Usafi wa Mazingira mashuleni ilikuwa duni, ambapo ni
asilimia 11 tu ya shule zilizofanyiwa utafiti zilikuwa na uwiano wa matundu ya
vyoo unaokidhi viwango vya kisera. Zaidi ya asilimia 20 ya shule zilikuwa na
uwiano wa wanafunzi 100 au zaidi kwa tundu moja la choo, huku asilimia 6 ya
shule zikiwa hazina kabisa matundu ya vyoo. Hali hii iliathiri mahudhurio ya
wasichana shuleni, hususan wakiwa kwenye hedhi, kutokana na ukosefu wa vifaa
vya hedhi salama na mazingira yasiyokuwa na faragha.
Katika Shule ya Sekondari ya Zirai, wilayani Muheza, wasichana wamepata
unafuu mkubwa baada ya kujengewa chumba maalum cha kujisitiri wanapokuwa kwenye
hedhi, kupatiwa pedi za bure shuleni, maji safi na salama kwenye vyoo, pamoja
na elimu na malezi bora kutoka kwa walimu wa kike. Wasichana wanasema sasa
wanaweza kuhudhuria masomo bila wasiwasi, tofauti na awali ambapo wengi
walikuwa wakikosa vipindi wanapokuwa kwenye hedhi. Afisa Elimu Kata ya Zirai,
Mwalimu Mohamed Mmole, anasema kuwa mafanikio haya yamechangiwa na uamuzi wa
shule kutoa kipaumbele kwa hedhi salama. Hata kwa changamoto ya upatikanaji wa
rasilimali za kununua pedi, shule imeweza kutumia sehemu ya ruzuku ya elimu kwa
wanafunzi (capitation) ili kuhakikisha huduma hizi zinapatikana.
Mwalimu Mmole anaeleza kuwa shule yao imeamua kuunga mkono juhudi za wadau
kwa kuhakikisha pedi na dawa za kutuliza maumivu kwa wasichana zinapatikana
muda wote. Anasisitiza kuwa utekelezaji wa mwongozo wa serikali wa mwaka 2016
unaweza kuleta mafanikio makubwa iwapo wadau wote wataendelea kushirikiana. Kwa
upande wake, Mwalimu Rehema Matuga, mlezi wa wasichana shuleni hapo, anasema
kuwa mazingira ya shule sasa ni salama kwa wasichana na yameongeza mahudhurio
yao darasani. Anabainisha kuwa awali suala la hedhi lilipuuzwa, na wasichana
walikuwa wakikosa shule kwa hofu ya kukosa vifaa na faragha, lakini kwa sasa
hali imebadilika na shule yao imekuwa mfano wa kuigwa.
Laya Christopher, mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule hiyo, anaeleza
kuwa tangu huduma za hedhi salama zimeboreshwa, wasichana wamekuwa na uhuru wa
kuhudhuria masomo bila wasiwasi. Anaeleza kuwa uwepo wa pedi shuleni umeondoa
aibu na hofu waliyoipata awali, na sasa wanaweza kuendelea na masomo yao kwa
utulivu. Naye Amina Ayubu, mwanafunzi wa kidato cha kwanza, anaeleza kuwa
tofauti na alivyokuwa shuleni msingi ambako suala la hedhi halikuwa likipewa
kipaumbele, sasa anajisikia huru na salama kutokana na elimu anayopata na
upatikanaji wa vifaa vya hedhi shuleni.
Aliyekuwa Afisa Programu wa ONGAWA katika mradi huo Bi. Leonia Andrew,
anasema kuwa lengo lao ni kuboresha mazingira ya utoaji elimu kwa watoto wa
kike ili waweze kumaliza elimu yao ya sekondari bila vikwazo vya hedhi.
Anasisitiza kuwa viongozi wa serikali waliopata mafunzo kuhusu hedhi salama
wanapaswa kuhakikisha suala hilo linapewa kipaumbele katika bajeti za
maendeleo. Kaimu Afisa Mtendaji wa Kata ya Zirai, Florence Mosha, anasisitiza
kuwa kila kijiji kinapaswa kuchukua hatua za dhati katika kutekeleza mpango
kazi wa kuhakikisha huduma za hedhi salama zinaboreshwa mashuleni.
Shule ya Sekondari ya Zirai ina zaidi ya wasichana 150 ambao kwa sasa
wanatumia boksi 10 za pedi kila mwezi. Pedi hizo zinapatikana kwa michango ya
wadau mbalimbali, shule kupitia bajeti yake ya capitation, na Kituo cha Taarifa
na Maarifa Zirai ambacho kinashirikiana na wadau wa maendeleo. Katika mafunzo
ya uandaaji wa bajeti zenye mrengo wa kijinsia yaliyofanywa na TGNP na ONGAWA,
viongozi wa vijiji vya Kwalumbizi, Zirai na Kizerui walikubaliana kuhakikisha
shule za msingi katika vijiji vyao zinajengewa vyumba maalum vya kujisitiri kwa
wasichana na kutenga bajeti kwa ajili ya ununuzi wa pedi. Pia wameweka kipaumbele
katika ujenzi wa maeneo ya kuchomea taka (incinerators) kwa ajili ya kuteketeza
pedi zilizotumika, ili kuhakikisha usafi unazingatiwa.
Hatua hizi zinathibitisha kuwa upatikanaji wa huduma za hedhi salama umeleta
mabadiliko makubwa katika maisha ya wasichana shuleni, kuimarisha mahudhurio
yao, na kuwafanya kushiriki masomo kwa kujiamini. Ushirikiano wa serikali,
wadau wa maendeleo, walimu na jamii kwa ujumla ni msingi muhimu katika
kuhakikisha kila mtoto wa kike anapata fursa sawa ya elimu bila vikwazo vya hedhi.
No comments:
Post a Comment