Sunday, June 30, 2024

Vijana wataka umri wa unyago,Jando uongezwe

 Vijana wataka umri wa kwenda unyago na Jando uongezwe






Na Deogratius Koyanga, Ruangwa

VIJANA katika kata ya Mandawa, Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa, Mkoani Lindi wamependekeza umri wa vijana wa kike na kiume kupelekwa jando na unyago uongezwe kutoka miaka 4 ya sasa iwe  miaka 8 hadi 10 ili kuwa na kundi la vijana waliokomaa wanaoweza kunufaika na mafundisho ya nyango na jando.

Hayo yalisemwa na vijana wakati wa mdahalo wa jamii kutoka katika makundi mbalimbali ya kijamii yaliyoshiriki katika kufanya tathimini ya mafanikio ya midahalo ya nyuma katika mradi wa uwezeshaji wanawake kushiriki kwenye nafasi za uongozi na haki ya uchumi, unaotekelezwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa kushirikiana na shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya wanawake (UNwomen).

Unwomen na TGNP, na wadau wengine ikiwepo serikali wanashirikiana katika kujenga uwezo kwa jamii, kubadilisha mila na desturi hasi pamoja na kuboresha mila nzuri zilizopo ili kuwezesha jamii kujikwamua kiuchumi sambamba na  wanawake kushiriki kwenye uongozi na  kufikia usawa wa kijinsia katika Nyanja zote

Akitoa mandekezo ya Vijana kwa niaba ya wengine,Mwenyekiti wa Vijana Kata ya Mandawa, Zamki Said, alisema kwamba, vijana wanapendekeza kwamba kuwepo na mwongozo unaobainisha umri rasmi wa watoto kwenda jando na unyago, ambao utaanzia angalau miaka 8 hadi 10, ambao watakuwa wameshaanza kukomaa kiakili, na wanaweza kuelewa mafundisho husika na kuyafanyia kazi.

“ …kwa sasa waoto wanaopelekwa jando ni wadogo ,  ni kuanzia miaka mitatu (3) hadi mitano (5) hawa hawawezi hata kuelewa kitu, kila wanachofundishwa kambini wanasahau, wakishatoka kwenye ile sherehe za kutolewa nje, wanakuja kuendelea na maisha huku kijijini, hata hawasalimii tena, utii hakuna, sasa unajiuliza wamejifunza nini? Mbona kijana hana mabadiliko? Jando au unyago imemsaidia nini?, Lakini pia mafundisho baadhi ni ya umri mkubwa lakini wanafundishwa na wakija huku mitaaani wanajaribu yale waliofundishwa ikiwepo ngono katika umri mdogo”alisema

Pia walipendekeza kwamba kuwepo na elimu ya kujitambua, kujitolea , uzalendo, usawa kijinsia, ukatili wa kijinsia ili kuwa na wazazi wazuri wa siku zijazo.

Vijana hao walipendekeza kwamba kuwepo na Makungwi na Manyakanga rasmi wanaotambulika  na watambuliwe na viongozi na serikali ili kuwepo na mfumo mzuri wa elimu inayotolewa na itakayoijenga jamii hasa dhana ya kujitolea kwaajili ya jamii na taifa

Aidha walipendekeza kwamba, kuwepo na  warombo au wasimamizi wa watoto walioko kambinini kwaajili ya unyago na jando ambao watatambuliwa rasmi, na wawe na maadili mazuri  na wasiwe ni watu wanaopatikana kwa utaratibu usio rasmi kwenye jamii.

Akifunga kikao kazi hicho Mtendaji kata wa kata ya Mandawa, halmasahuri ya wilaya ya Ruangwa, Said Ng’itu,  alisema kwamba, uwepo wa TGNP kwenye kata hiyo kumeongeza kwa kiasi kikubwa uelewa wa masuala ya Kijinsia kwani katika kata hiyo  kulianzishwa kituo cha Taarifa na Maarifa ambacho kimeendelea kuchachua masuala ya harakati za usawa wa Kijinsia na kupeleka elimu hiyo katika taasisi mbalimbali ikiwepo kwenye mikutano ya Vijiji.

“ hapa, tulikuwa na changamoto ya Choo cha wasindikizaji wa wazazi wanaojifungua katika Kituo cha Afya, lakini hawa KC waliona hilo kuwa ni tatizo, wameliibua, na wamejitahidi kuhamasisha, sasa choo kinajengwa, ni mafanikio makubwa sisi tumeona nguvu ya jamii wakiamua kuchukua hatua kuboresha mambo yao” alisema  mtendaji.

No comments:

Post a Comment