Unyago, jando vyachangia utoro shuleni
Na Deogratius Koyanga, Nachingwea
Vitendo vya kupeleka watoto wa
kiume na kike kwenye shughuli za jando na unyago vinavyofanywa na jamii ya Mkoa wa Lindi na viunga vyake
vinachangia kwa kiasi kikubwa utoro wa wanafunzi wa shule za msingi na
sekondari.
Hayo yamebainishwa katika mdahalo
wa jamii uliowashirikisha wananchi kutoka katika vikundi vya kijamii, wazee wa
mila, mangariba na viongozi wa dini katika kata ya Mtuwa, halmashauri ya wilaya
ya Nachingwea, mkoani Lindi.
Imebainishwa kwamba, vitendo hivyo
vinatokana na jamii kutokufuata ratiba ya kufunga na kufungua shule na
kuwaingiza watoto wadogo wa shule za msingi kwenye shughuli za kimila za jando
na unyago wakati shule zikiendelea na ratiba zake na kupelekea mamia ya
wanafunzi kukosa masomo hadi zitakapofanyika sherehe za kuwatoa ndani,
Mdahalo huo, unawashirikisha
wananchi na wadau mbalimbali kama sehemu
ya kutekeleza mradi wa uwezeshaji wanawake kushiriki kwenye nafasi za
uongozi na maamuzi na haki ya uchumi,
unaotekelezwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa ufadhili wa Unwomen
Tanzania,
Akizungumza wakati wa mjadala huo,
mchungaji wa kanisa la wadiventista wasabato, kata ya Mtuwa,Samwel Mang’ati, alisema
kwamba wao kama viongozi wa dini wanashauri utaratibu wa kuheshimu ratiba za
watoto wa shule ufuatwe ili watoto wote wapate haki ya kupata elimu sambamba na
maadili lakini akaonya kuhusu mila hizo kuzingatia maadili na heshima kwa
kutumia lugha nzuri zenye staha, kuepuka matusi, kuepuka kufundisha vitu
vilivyo nje ya umri wa watoto hao ili kukuza jamii yenye maadili mazuri.
“sisi kama viongozi wa dini
tunashauri kuwepo kwa watu maalum, hawa wanaoitwa “warombo” wawe na elimu, wawe
ni watu wazima, walioandaliwa na wawe na
elimu maalum ya kufanya kazi hiyo” alisema MchungajI Samwel
Kwa upande wake Mwenyekiti wa
Kigango cha Kanisa Katoliki cha Mtuha,Emelius Mkwawa, Alisema kwamba anashauri,
utaratibu wa kundesha unyago na jando, uzingatie ratiba za shule ili
kutokuwakosesha watoto wa kike na kiume haki ya kupata elimu.
“nashauri, mara tu shule
zinapofungwa, hizi shughuli za kimila zianzie hapo hapo, hiyo wiki ya kwanza,
shule zinapofunguliwa tuhakikishe hakuna mtoto anabaki kwenye jando au unyago.
Wote wawe huru waende shule”alisema na kuongeza:-
“Ninashauri wazazi waache hii
tabia kuingia gharama kubwa na kutumia fedha nyingi kwenye sherehe za jando na
unyago lakini kushindwa kuwanunulia
watoto hao sare za shule na vifaa vya shule mara shule zinapofunguliwa, unakuta
mzazi ananunua nguo za gharama kubwa kwaajili ya shughuli ya unyago au jando,
lakini sare za shule hakuna,viatu”
Alisema kwamba, ni vizuri wazazi
kuwekeza kwenye elimu, na wanaotoa zawadi kwa watoto wanunue madaftari ,
kalamu,mabegi ya shule, sare za shule ili kuwafanya watoto walioingia jando
kuipenda elimu.
Kwa upande wake Ngariba wa muda
mrefu mzee Thomas Ndimbo, alismea
kwamba, taratibu za kutoa vibali vya kuendesha
jando na unyago zinajieleza wazi kwamba, watoto waende jando na unyago
wakiwa likizo na wasiwepo kwenye shughuli hizo wakati shule zimefunguliwa na
huu ni utaratibu wa mkoa mzima wa Lindi, lakini jamii imekiuka kwa kupanga
shughuli hizo wakati mwingine.
“Labda sisi mangariba tukutane,
tufanye kikao pamoja na viongozi wa serikali za vijiji vyetu sambamba na jamii
ili tukubaliane tena. Asiwepo ngariba anayekubali kupeleka watoto uwanjani,
wakati wa shule au wengine akiwa sshuleni” alisema Ndimbo.
No comments:
Post a Comment