Thursday, September 1, 2022

Kwanini ni muhimu kuondoa kodi kwenye taulo za kike?

 

Kwanini ni muhimu kuondoa kodi kwenye taulo za kike?

Uchambuzi umefanywa na Deogratius Temba

Mnamo mwezi Julai 2018, Serikali ya Tanzania ilipotoa msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa Taulo za Kike ilitoa ujumbe wa wazi kwamba bidhaa hizi ni hitaji la Msingi la Haki za binadamu nani la lazima kwa wasichana na wanawake.

Katika Hotuba ya Bajeti ya mwaka wa fedha 2018/2019, Waziri wa Fedha wakati huo, Dkt Philipo Mpango akasisitiza kwamba wanawake na hasa wasichana wa shule wanaotoka katika familia masikini wanahitaji kupata taulo za kike kwa bei nafuu na rafiki ili waweze kujisitiri  na kuhsiirki kwenye masomo au shughuli za uzalishaji wakiwa salama.

 Ilikuwa ni hatua kubwa muhimu kuelekea usawa wa kijinsia, na kupunguza ‘Umasikini wa Hedhi’. Hatua hii ilisherehekewa katika jukwaa la kitaifa na kimataifa. Tanzania ni kati ya nchi chache vinara kutekeleza mpango huu, ikiiipiku nchi ya Australia (ambayo imeondoa kodi Januari 2019), na nchi nyingine za ukanda na duniani.  


Picha hii imepatikana kwa hisani ya Mtandao

 

Hatua hii ni muafaka kwa uchumi, na ingechangia viwango wa ukuaji wa Taifa. Hata hivyo, Benki ya Dunia inakadiria kwamba, kwa kila uwiano wa ongezeko la asilimia moja ya idadi ya wanawake wenye elimu ya sekondari,  pato la nchi la mwaka hukua kwa  asilimia 0.3.            

Kwa nini Msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ni muhimu na Ubaki

Msamaha wa kodi ya ongezeko la Kodi ya Thamani (VAT) kwenye taulo za kike ni muhimu kwa sababu kuu mbili, ikihusianishwa na usawa wa kijinsia na pia unafuu wa Taulo za Kike. Kuhusu usawa wa jinsia, wanawake na wasichana hawana hiari juu ya Hedhi. Kuanzia umri wa miaka 13 – 55 wataingia kwenye Hedhi kwa kadiri ya wiki nzima, kila mwezi.

Kulipa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika bidhaa za hedhi kunawafanya wanawake kulipa kodi ya ziada wakilinganishwa na wanaume kiuhalisia kutokana na hali yao ya kibaiolojia, kodi iko kwa watu wa jinsi moja.   Kuhusu unafuu, msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani una uwezo wa kupunguza gharama ya taulo  za kike kwa asilimia 18, ambalo linaweza kuchangia bidhaa kupatikana kirahisi kwa wanawake na wasichana nchini kote. Ni muhimu bidhaa hizi zikawa nafuu ili kuwasaidia wanawake na wasichana kudhibiti Hedhi kwa usafi na utu.    

Hedhi isichukuliwe kama njia ya kuongeza mapato, badala yake upatikanaji wa bidhaa za hedhi uchukuliwe kama suala la haki za binadamu na uswa wakijinsia, na iwe hivyo.  Serikali kuondoa VAT si tu inatambua bidhaa za hedhi kwamba ni bidhaa ‘muhimu’, lakini pia inawasaidia wanawake na wasichana kuzipata kwa unafuu na hivyo kupunguza vikwazo wanavyokutana navyo kielimu na kiajira.


Athari ya Kuondolewa kwa VAT kwenye Soko

Uchunguzi wa awali unaonyesha matokeo mbali mbali juu ya kuondolewa kwa VAT.  Kuna tatizo kwenye msimamo wa bei unosababishwa na mnyororo wa usambazaji, ambao humwacha muuzaji wa rejareja kuamua bei ya mwisho. Changamoto kubwa ikiwa ni uzingativu wa bei kwenye bidhaa zinazonunulika haraka kutokana na mfumo uliozoeleka. Hata hivyo kutokana na kuondolewa na kwa VAT bidhaa za pedi zenye majina makubwa kama Always na HC walithibitisha kushuka kwa bei kwa asilimia 20. Bidhaa nyingine pia zilionyesha kupunguza bei kwa viwango tofauti, japo kwa kiasi kidogo.

 

Kwa kawaida wauzaji wa rejareja ndio huchukua kiwango kikubwa cha faida kwenye mnyororo wa usambazaji, na wao ndio wanabeba hatari na dhamana ya biashara na ndio wenye ushawishi mkubwa juu ya bei ya mwisho (bei ya mlaji). Hatimaye, pamoja na msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani, kunatakiwa pia kuwepo na kanuni na njia madhubuti za ufuatiliaji kuhakikisha wauzaji wa rejareja  wanazingatia  bei elekezi. Ushawishi wa bei ya rejareja ni jambo linalohitaji mbinu, muda na uwekezaji na wadau kwa ajili ya kupeana taarifa.

Utafiti wa awali uliofanywa Morogoro na Mbeya[1] uliohusisha maduka 2,906 yanayouza taulo za kike (yakiwemo ya rejareja, ya jumla, maduka ya dawa), inaonyesha kwamba bei ya bidhaa moja ikitofautiana kwa asilimia 40 kutoka kwenye duka moja na jingine. Asilimia 52 inaonyesha pakiti moja ya pedi ikiuzwa kwa Shilingi 2,000/=, Asilimia 13 zikiuzwa kwa shilingi 1500/= na asilimia 28 zikiuzwa kwa zaidi ya shilingi 2500/=.

Wahamasishaji wa Bei:  Pia, Utafiti huu unaonyesha kwamba wakati mwingine bei inakuwa thabiti zaidi sehemu ambapo duka kuu linauza bidhaa kwa bei ya chini kwa eneo husika. Hii inatoa fursa ya ushirikiano kati sekta ya umma na binafsi na wahamasishaji wa bei katika kushusha bei katika maeneo ya jirani. Hasa, mara watumiaji wanapojua kuna maeneo yanayoshindana wanayoweza kununua bidhaa, wana uwezo wa kuwa nguvu kubwa ya kuleta ushindani katika soko, na kusababisha bei kushuka.

Utafiti wa awali wa soko unaonyesha kuwa msamaha wa kodi ya VAT ulianza kupunguza bei. Hata hivyo, sera ya msamaha wa kodi ya VAT imetekelezwa kwa muda mfupi chini ya mwaka mmoja, na huu sio muda wa kutosha kuelewa na kupima athari zake.

 

Mapendekezo ya wadau ili kurudisha msamaha wa kodi kwa pedi

Ni muhimu msamaha wa VAT kubaki Tanzania. Hii ni hatua ya awali muafaka ya upunguzaji wa gharama za bidhaa za Hedhi. Ikiwa wanawake na wasichana watakuwa na uwezo wa kumudu gharama za pedi, haya yatakuwa ni mapinduzi makubwa yatakayowawezesha kutumia muda wao kwenye kazi za uzalishaji na kielimu, na pia kuboresha afya zao.

 Kwa ujumla wake hayo yote yatachangia kwenye ukuaji wa uchumi wa Taifa, kupunguza mzigo kwenye sekta ya afya, na pia kuhakikisha wanawake na wasichana wanatoa mchango kwenye sera ya viwanda na Dira ya maendele ya Taifa ya 2025.

 

Ili Msamaha wa kodi ya VAT uweze kufanyakazi kama ilivyotarajiwa ni vyema serikali na sekta binafsi kufanyakazi kwa karibu, kuhakisha utekelezwaji wa ushushaji wa bei. Pia usimamizi kwenye serikali za mitaa kunaweza kuleta tofauti katika kuongeza uelewa na utekelezaji. Wauzaji wa rejareja waelimishwe kwamba bidhaa za Hedhi ni bidhaa muhimu kwa akina mama na si anasa.  Pia, Serikali na Sekta binafsi itumie fursa ya kuona matokeo chanya ya kufanyakazi pamoja ili kuleta matokeo mapana, vile vile watumie washawishi kwenye jamii.

 

Kuhamasisha watumiaji na kuwaeleza juu ya msamaha wa VAT na kuwapa bei elekezi, itachagiza bidhaa kushuka bei hasa kwa wauzaji wa rejereje na itaongeza msukumo kwa wauzaji wa rejareja kushusha bei ya bidhaa yenyewe. Kampeni za kitaifa zinaweza kusaidia jitihada hii, ikiambata na kutengeza hitaji kubwa katika soko.

Pamoja na kwamba Serikali imependekeza punguzo la asilimia 5 ya kodi ya Makampuni. Hii ina hatari ya kutoweza kubadilisha bei za pedi ikiwa hakuna kanuni na ufuatiliaji wa bei, wanfanya biashara wa reja reja wanaweza kuendelea kujiongezea faida. Mwaka ujao wa fedha 2023/2024 uwe ni fursa nyingine ya kuendelea kuwa na msamaha wa kodi ya VAT kwa Taulo za Kike, na kufuatilia athari yake kwa karibu ili vikwazo viweze kutatuliwa.  Tanzania inatakiwa kuendelea kuwa kinara wa dunia kwenye jambo hili ili wengine wafuate na wajifunze kwetu.  Uchambuzi umefanywa na Deogratius Temba-0784686575

 



 

No comments:

Post a Comment