Tuesday, September 27, 2022

CHAUMMA WAANDAA SERA YA USAWA WA JINSIA

 

CHAUMMA WAANDAA SERA YA USAWA WA JINSIA

Na Mwandishi Wetu,Dar

CHAMA cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), kimeanza mchakato wa kuandaa sera ya Jinsia ya chama hicho kwaajili ya kuzingatia usawa wa Kijinsia na kuongeza ushiriki wa wanawake, vijana  na watu wenye ulemavu katika nafasi za uongozi na maamuzi.

Azkiungumza wakati wa kikao kazi cha kuandaa rasimu ya Serya ya Jinsia ya Chama hicho,  Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) Tanzania bara Bw. Eugen  Kabendera wakati wa Mafunzo Maalum ya namna ya kuandaa Sera yalitotolewa na  Shirika la Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa kushirikiana na shirika la Wanawake na Sheria Katika Maendeleo Afrika (WiLDAF) alisema kwamba, imefika mahali ambapo haiepukiki kuwa na sera za usawa wa kijinsia kila nyanja za taifa letu.


Bw. Kabendera amesema kuwa Sera ya Jinsia ni muhimu katika Taifa letu kwa kuwa inakwenda kulinda Haki za wanawake, vijana, wazee na watu wenye ulemavu katika kufanya Siasa.

“ sisi kama CHAUMMA tunatamani kufanya siasa inayomshirikisha mwanamke moja kwa moja. Ushiriki wa makundi yote, watu wenye ulemavu, vijana, wazee, wajisikie sehemu ya siasa,wanufaike na siasa na mgawanyo wa nafasi za uongozi uzingatie usawa” alisema.

Aidha ameongeza kuwa takwaimu zinaonyesha kuwa Wanawake katika nchi hii ni wengi kuliko makundi yote lakini wamekuwa wakitumiwa vibaya na kuwa kama njia ya kuwapitisha wanasiasa kupata uongozi, na  CHAUMMA kimejipanga  kuhakikisha kuwa sera ya jinsia itatoa mweleko mzuri wa kuzingatia usawa wa Kijinsia katika nafasi za maamuzi na uongozi.

Kwa upande wake Katibu wa jumuiya ya wanawake CHAUMMA Bi. Marry Mpangala ameshukuru sana TGNP pamoja na WILDAF  kwa kuweza kuwaletea mafunzo hayo na kusema kuwa katika vyama vingi vya siasa ngazi za maamuzi zimekuwa zikishikiliwa na wanaume na wanawake wamekuwa wakiachiwa nafasi ndogo ndogo.

Ameongeza kwa kuwataka wanawake waje kwa wingi ndani ya CHAUMMA ili waweze kusogeza mbele Ajenda yao ya ‘Ubwabwa na Maharage’ kuhakikisha inawafikia wangonjwa Mahosptalini na Watoto Mashuleni, na kuongeza kuwa wanawake wakati wa kujifungua wanapoteza damu nyingi hivyo wanahitaji chakula cha kutosha ambacho ni Ubwabwa na Maharage.

Deogratius Temba, ambaye ni mwezeshaji wa mchakato huo kwaniaba ya TGNP na WILDAF alisema kwamba, mchakato huo unafanywa na chama, mashirika hayo yanawezesha kuweka sawa masuala ya Kijinsia ili sera hizo ziweze kukamilika zikiwa zimeweka vizuri misingi ya usawa wa Kijinsia na ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi.

“Hii ni sehemu ya utekelezaji wa maazimio ya viongozi wakuu wa vyama vya siasa, baada ya kupatiwa mafunzo na TGNP na WILDAF na vikao kadhaa vya mashauriano vilifanyika chini ya uratibu wa Ofisi ya msajili wa vyama vya siasa, baadaye walikubaliana kwamba ili kufikia usawa wa Kijinsia ndani ya vyama vya siasa na kuzuia vitendo vya Ukatili na udhalilishaji wa Kijinsia ndani ya vyama ni muhimu kuwa na sera ya Jinsia” a;isema Temba

CHAUMMA kinakuwa miongoni mwa vyama vinane vya siasa nchini Tanzania ambavyo vipo kwenye mchakato wa kuandaa sera ya Jinsia, kwaajili ya kuweka mazingira salama kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kushiriki kwenye nafasi za uongozi na maamuzi.

No comments:

Post a Comment