Thursday, September 8, 2022

Hali ya Upatikanaji na Umiliki wa Ardhi kwa wanawake

 

Hali ya Upatikanaji na Umiliki wa Ardhi kwa wanawake

 

Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia (2000) ilitoa kipaumbele katika eneo la upatikanaji, umiliki na utumiaji wa ardhi kwa usawa baina ya wanawake na wanaume. Umiliki na utumiaji wa ardhi ni nguzo muhimu katika suala zima la maendeleo ya wanawake kiuchumi.

 Hivyo, umiliki wa ardhi kwa wanawake ni muhimu katika kufikia fursa nyingine za kiuchumi nchini. nchini Tanzania, ni wanawake 26% wanamiliki ardhi ya kilimo (SIGI, 2020). Hali hii inatokana na kuendelea kuwepo kwa mila na desturi zinazowapendelea wanaume kurithi na kumiliki ardhi ya familia ambapo wanawake hupata fursa hiyo kupitia wanaume ndani ya familia.

Serikali imeendelea na jitihada za kisera ili kuhakikisha kuwa umiliki wa ardhi unazingatia usawa wa kijinsia. Sera hizo ni pamoja na Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Makazi (2000), Sera ya Taifa ya Ardhi (1995), Ibara mbalimbali za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) na Dira ya Maendeleo 2025. Jitihada nyingine ni pamoja na Marekebisho ya Sheria ya Ardhi ya Vijiji Na. 5 ya mwaka 1999 kifungu cha 3 (2) ambayo inatoa fursa kwa kila mwanamke kumiliki na kutumia ardhi na kuanzisha Kamati za kuhamasisha haki za wanawake kumiliki ardhi mwaka 2017. Kutokana na jitihada hizi, mwaka 2018 jumla ya hati 80,000 za umiliki wa ardhi zilisajiliwa.

Jitihada hizi zimewezesha kuongezeka kwa idadi ya wanawake wanaomiliki ardhi kutoka asilimia 9 hadi asilimia 25 na kuongezeka kwa umiliki wa pamoja kutoka asilimia 6 hadi asilimia 16; kuongezeka kwa watu wenye hati miliki zinazotambulika kisheria kutoka asilimia 50 mwaka 2016 hadi asilimia 59 mwaka 2018; kuongezeka kwa idadi ya hati za kimila za umiliki wa ardhi mfano, katika Mkoa wa Iringa pekee jumla ya hati za kimila 3,208 zilitolewa (1,970 Wilaya ya Kilolo na 1,238 Wilaya ya Mufindi). Hii ni matokeo ya uwezeshaji wa Shirika Lisilo la Kiserikali la Haki Ardhi linalohamasisha uandaaji wa mipango ya matumizi bora ya ardhi katika vijiji 7 katika Wilaya ya Mufindi na 11 katika Wilaya ya Kilolo.



Pamoja na mafanikio yaliyopatikana, suala ya umiliki wa ardhi na rasilimali nyingine za uzalishaji limeendelea kuathiri maendeleo ya wanawake ambapo licha ya kuwa na sheria zinazowalinda wanawake katika kumiliki rasilimali bado mila na desturi kandamizi ni kikwazo. Umiliki wa rasilimali za kiuchumi kwa wanawake kama vile pato la familia, ardhi, vitendea kazi na mikopo umeendelea kuwa mdogo ukilinganisha na wanaume. Pamoja na ukweli kwamba wanawake wanachangia Katika sekta ya kilimo uvuvi na misitu, wanawake wamachangia asilimia takribani asilimia 67 (ILFS, 2014).

Kiwango cha uzalishaji kwa wanawake katika sekta ya kilimo ni kidogo ikilinganishwa na wanaume. Hii ni kutokana na matumizi ya zana duni kama vile jembe la mkono. Sheria ya Mirathi ya Kimila (1963) inazuia wanawake, wajane na wasichana kurithi ardhi na hivyo kuwakosesha fursa za kumiliki rasilimali za kiuchumi na uwekezaji. Hivyo, maboresho katika sheria ni muhimu katika kuwawezesha wanawake kuboresha hali zao za kiuchumi na kijamii. Kwa msingi huo, ni muhimu kuiwezesha jamii kushiriki na kuwa na uelewa wa haki za wanawake kurithi mali ikiwemo ardhi.

No comments:

Post a Comment