Vijana wataka umri wa kwenda unyago na Jando uongezwe

Na Deogratius Koyanga, Ruangwa
VIJANA katika kata ya Mandawa, Halmashauri
ya wilaya ya Ruangwa, Mkoani Lindi wamependekeza umri wa vijana wa kike na
kiume kupelekwa jando na unyago uongezwe kutoka miaka 4 ya sasa iwe miaka 8 hadi 10 ili kuwa na kundi la vijana
waliokomaa wanaoweza kunufaika na mafundisho ya nyango na jando.
Hayo yalisemwa na vijana wakati
wa mdahalo wa jamii kutoka katika makundi mbalimbali ya kijamii yaliyoshiriki
katika kufanya tathimini ya mafanikio ya midahalo ya nyuma katika mradi wa
uwezeshaji wanawake kushiriki kwenye nafasi za uongozi na haki ya uchumi,
unaotekelezwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa kushirikiana na shirika
la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya wanawake (UNwomen).
Unwomen na TGNP, na wadau wengine
ikiwepo serikali wanashirikiana katika kujenga uwezo kwa jamii, kubadilisha
mila na desturi hasi pamoja na kuboresha mila nzuri zilizopo ili kuwezesha
jamii kujikwamua kiuchumi sambamba na wanawake kushiriki kwenye uongozi na kufikia usawa wa kijinsia katika Nyanja zote
Akitoa mandekezo ya Vijana kwa
niaba ya wengine,Mwenyekiti wa Vijana Kata ya Mandawa, Zamki Said, alisema
kwamba, vijana wanapendekeza kwamba kuwepo na mwongozo unaobainisha umri rasmi
wa watoto kwenda jando na unyago, ambao utaanzia angalau miaka 8 hadi 10, ambao
watakuwa wameshaanza kukomaa kiakili, na wanaweza kuelewa mafundisho husika na
kuyafanyia kazi.
“ …kwa sasa waoto wanaopelekwa
jando ni wadogo , ni kuanzia miaka
mitatu (3) hadi mitano (5) hawa hawawezi hata kuelewa kitu, kila wanachofundishwa
kambini wanasahau, wakishatoka kwenye ile sherehe za kutolewa nje, wanakuja
kuendelea na maisha huku kijijini, hata hawasalimii tena, utii hakuna, sasa
unajiuliza wamejifunza nini? Mbona kijana hana mabadiliko? Jando au unyago
imemsaidia nini?, Lakini pia mafundisho baadhi ni ya umri mkubwa lakini
wanafundishwa na wakija huku mitaaani wanajaribu yale waliofundishwa ikiwepo
ngono katika umri mdogo”alisema
Pia walipendekeza kwamba kuwepo
na elimu ya kujitambua, kujitolea , uzalendo, usawa kijinsia, ukatili wa
kijinsia ili kuwa na wazazi wazuri wa siku zijazo.
Vijana hao walipendekeza kwamba
kuwepo na Makungwi na Manyakanga rasmi wanaotambulika na watambuliwe na viongozi na serikali ili
kuwepo na mfumo mzuri wa elimu inayotolewa na itakayoijenga jamii hasa dhana ya
kujitolea kwaajili ya jamii na taifa
Aidha walipendekeza kwamba,
kuwepo na warombo au wasimamizi wa
watoto walioko kambinini kwaajili ya unyago na jando ambao watatambuliwa rasmi,
na wawe na maadili mazuri na wasiwe ni
watu wanaopatikana kwa utaratibu usio rasmi kwenye jamii.
Akifunga kikao kazi hicho Mtendaji
kata wa kata ya Mandawa, halmasahuri ya wilaya ya Ruangwa, Said Ng’itu, alisema kwamba, uwepo wa TGNP kwenye kata
hiyo kumeongeza kwa kiasi kikubwa uelewa wa masuala ya Kijinsia kwani katika
kata hiyo kulianzishwa kituo cha Taarifa
na Maarifa ambacho kimeendelea kuchachua masuala ya harakati za usawa wa
Kijinsia na kupeleka elimu hiyo katika taasisi mbalimbali ikiwepo kwenye
mikutano ya Vijiji.
“ hapa, tulikuwa na changamoto ya
Choo cha wasindikizaji wa wazazi wanaojifungua katika Kituo cha Afya, lakini
hawa KC waliona hilo kuwa ni tatizo, wameliibua, na wamejitahidi kuhamasisha,
sasa choo kinajengwa, ni mafanikio makubwa sisi tumeona nguvu ya jamii wakiamua
kuchukua hatua kuboresha mambo yao” alisema
mtendaji.