Friday, September 30, 2022

Wazazi NABA wahimizwa kuwalinda watoto dhidi ya Ukatili wa Kijinsia

 

Na Mwandishi Wetu

KUTOKANA na kuongezeka kwa vitendo vya Ukatili wa Kijinsia katika Jamii, hasa kwa watoto wanapokuwa nje ya shule, Jamii imeashwa kuwalinda watoto wa kike na kiume wanaotarajiwa kuahitimu darasa la saba mapema mwezi Oktoba mwaka huu.

Pia wazazi wameaswa kuhakikisha wakati wahitimu wa darasa la saba wakisubiria kuijunga na kidato cha kwanza mwakani, wanawaandalia watoto sehemu salama ya kuendelea kujifunza  na kuongeza maarifa ya kitaaluma au kuboresha vipawa na vipaji vyao Zaidi.

Akizungumza wakati wa mahafali ya nane ya shule ya awali na msingi ya NABA iliyopo Kata ya Saranga, manispaa ya Ubungo, jijini Dar es salaam, Diwani wa kata ya Saranga Edward Laizer ambaye alikuwa mgeni rasmi, alisema kwamba, wanafunziz wanaohitimu wamekuwa salama na kufikia kuhitimu darasa la saba akwa sababu waalimu walikuwa  makini, na walishirikiana vizuri na wazazi.

“Nina waasa sasa kuendeela kuwa karibu na hawa watoto, bado hawajawa watu wazima, wanatakiwa kuendelea kulelewa kimaadili, wanahitakiwa kuwa chini ya uangalizi, kuhitimu kwao leo tusiwache waka anza kuzurura mitaani, wakajiunga na vikundi vya uhalifu”.alisema Laizer katika hotuba yake.

 Aliongeza kwamba, Vijana wakikosa uangalizi, ndio tunapata changamoto ya watoto wa mitaani, panya road na makundi mengine ambayo yanaibuka katika jamii.

“Tunawasihi sana miezi hii ya kusubiria matokeo, tuwatafutie hawa vijana sehemu ya kukaa, vitu vya kufanya, kujifunza, ili wawe bize badala ya kuzurura mitaani. Zipo fursa za kujifunza computer, ufundi wa muda mfupi, kujifunza stadi za maisha, ambavyo pia vitawafanya watambue vipaji vyao” aliongeza

Laizer aliongeza kwamba, Watoto wa kike wengi wanapata ujauzito wakati wa kusbiria matokeo ya shule, au hata wengine kuolewa kabla ya kujiunga na kidato cha kwanza, wakati ni  kosa la jinai, kwa mujibu wa Sheria ya Elimu ya mwaka 1978 pamoja na kanuni zake.

Pia alipongeza uongozi wa shule hiyo kwa kuifanya kata ya Saranga kupaa kielimu kutokana na Shule hiyo kufanya vizuri kitaaluma, katika mitihani ya Kitaifa, kimkoa na kiwilaya.

Awali akisoma taarifa ya maendeleo ya shule hiyo, Mwalimu Mkuu, Mariam Mbaya, alisema kwamba, shule imewekaza kwenye kumjenga mtoto kukua kinidhamu, kitaaluma na kujitambua.
“Mheshimiwa Mgeni rasmi, kama unavyowaona watoto hawa , wamejengwa kwenye misingi ya nidhamu, kujiamini, na kujitambua. Wanafunzi waliohitimu NABA wanajiamini, wanauwezo mkubwa wa kujieleza, na wanafaulu vizuri. Matokeo yetu kitaaluma ni mazuri sana. Na tunaendelea kujitahidi kufanya vizuri Zaidi” alisema Mwalimu Mkuu.

Shule ya awali na msingi NABA ipo katika manispaa ya Ubungo, kata ya Saranga.  

Tuesday, September 27, 2022

CHAUMMA WAANDAA SERA YA USAWA WA JINSIA

 

CHAUMMA WAANDAA SERA YA USAWA WA JINSIA

Na Mwandishi Wetu,Dar

CHAMA cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), kimeanza mchakato wa kuandaa sera ya Jinsia ya chama hicho kwaajili ya kuzingatia usawa wa Kijinsia na kuongeza ushiriki wa wanawake, vijana  na watu wenye ulemavu katika nafasi za uongozi na maamuzi.

Azkiungumza wakati wa kikao kazi cha kuandaa rasimu ya Serya ya Jinsia ya Chama hicho,  Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) Tanzania bara Bw. Eugen  Kabendera wakati wa Mafunzo Maalum ya namna ya kuandaa Sera yalitotolewa na  Shirika la Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa kushirikiana na shirika la Wanawake na Sheria Katika Maendeleo Afrika (WiLDAF) alisema kwamba, imefika mahali ambapo haiepukiki kuwa na sera za usawa wa kijinsia kila nyanja za taifa letu.


Bw. Kabendera amesema kuwa Sera ya Jinsia ni muhimu katika Taifa letu kwa kuwa inakwenda kulinda Haki za wanawake, vijana, wazee na watu wenye ulemavu katika kufanya Siasa.

“ sisi kama CHAUMMA tunatamani kufanya siasa inayomshirikisha mwanamke moja kwa moja. Ushiriki wa makundi yote, watu wenye ulemavu, vijana, wazee, wajisikie sehemu ya siasa,wanufaike na siasa na mgawanyo wa nafasi za uongozi uzingatie usawa” alisema.

Aidha ameongeza kuwa takwaimu zinaonyesha kuwa Wanawake katika nchi hii ni wengi kuliko makundi yote lakini wamekuwa wakitumiwa vibaya na kuwa kama njia ya kuwapitisha wanasiasa kupata uongozi, na  CHAUMMA kimejipanga  kuhakikisha kuwa sera ya jinsia itatoa mweleko mzuri wa kuzingatia usawa wa Kijinsia katika nafasi za maamuzi na uongozi.

Kwa upande wake Katibu wa jumuiya ya wanawake CHAUMMA Bi. Marry Mpangala ameshukuru sana TGNP pamoja na WILDAF  kwa kuweza kuwaletea mafunzo hayo na kusema kuwa katika vyama vingi vya siasa ngazi za maamuzi zimekuwa zikishikiliwa na wanaume na wanawake wamekuwa wakiachiwa nafasi ndogo ndogo.

Ameongeza kwa kuwataka wanawake waje kwa wingi ndani ya CHAUMMA ili waweze kusogeza mbele Ajenda yao ya ‘Ubwabwa na Maharage’ kuhakikisha inawafikia wangonjwa Mahosptalini na Watoto Mashuleni, na kuongeza kuwa wanawake wakati wa kujifungua wanapoteza damu nyingi hivyo wanahitaji chakula cha kutosha ambacho ni Ubwabwa na Maharage.

Deogratius Temba, ambaye ni mwezeshaji wa mchakato huo kwaniaba ya TGNP na WILDAF alisema kwamba, mchakato huo unafanywa na chama, mashirika hayo yanawezesha kuweka sawa masuala ya Kijinsia ili sera hizo ziweze kukamilika zikiwa zimeweka vizuri misingi ya usawa wa Kijinsia na ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi.

“Hii ni sehemu ya utekelezaji wa maazimio ya viongozi wakuu wa vyama vya siasa, baada ya kupatiwa mafunzo na TGNP na WILDAF na vikao kadhaa vya mashauriano vilifanyika chini ya uratibu wa Ofisi ya msajili wa vyama vya siasa, baadaye walikubaliana kwamba ili kufikia usawa wa Kijinsia ndani ya vyama vya siasa na kuzuia vitendo vya Ukatili na udhalilishaji wa Kijinsia ndani ya vyama ni muhimu kuwa na sera ya Jinsia” a;isema Temba

CHAUMMA kinakuwa miongoni mwa vyama vinane vya siasa nchini Tanzania ambavyo vipo kwenye mchakato wa kuandaa sera ya Jinsia, kwaajili ya kuweka mazingira salama kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kushiriki kwenye nafasi za uongozi na maamuzi.

Thursday, September 15, 2022

CUF yatengeneza sera ya usawa wa Kijinsia

 

Na Mwandishi wetu, Unguja

Chama cha wananci (CUF) kimeanza mchakato wa kuandaa sera ya Jinsia ya Chama itakayotumika kurasimisha masuala ya kujinsia ndani ya chama kwa kipindi chote

Mchakato huu ni sehemu ya utekelezaji wa maazimio ya Mkutano wa Baraza la Vyama vya siasa nchini lilolomwagiza Msajili wa Vyama vya Siasa kushirikiana na wadau ili kuviwezesha vyama vya siasa kuwa na sera ya Jinsia ili kuzingatia usawa wa kijinsia na kuongeza ushiriki wa wanawake, vijana, watu wenye ulemavu katika nafasi za uongozi na maamuzi ndani ya chama.

Mchakato huu unawezesha na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) na shirika la Wanawake, Sheria katika Maendeleo Afrika (WilDAF), kwa kutoa wataalamu ambao wanajenga uwezo kwa watendaji wa CUF kuandaa rasimu ya sera hiyo.




Akizungumza wakati wa maandalizi ya rasimu hiyo, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Mbarouk Seif Salim, wakati wa kukaribisha wajumbe wa kikao kazi hicho kuanza kazi,  alisema kwamba, chama kimefurahi kwamba kimekuwa miongoni mwa vyama vya awali ambavyo vitatengeneza sera hiyo, na ana matumaini kuwa kazi hiyo itamalizika kwa wakati na kuleta tija ndani ya chama.

“sisi CUF ni chama cha siasa ambacho tumekuwa tukizingatia  usawa wa kijinsia, kwenye ushiriki wa wanawake tumejitahidi, bado hatujafikia 50:50 lakini tuna matumaini kuwa tutafanya vizuri sana baada ya sera hii kukamilika” alisema Naibu Katibu Mkuu.

Aidha Katibu wa Kikosi kazi, Ally Juma Khamis, alisema kwamba kwa niaba ya kikosi kazi hiyo, wameamua kujituma, kuhakikisha kazi hiyo ya kuandaa sera inakamilika kwa wakati na inawasilishwa kwenye vikao vya juu kwaajili ya kupata baraka na kuanza kutekelezwa.

“sisi tunashukuru Chama kwa kutuamini, kututeua tuwe sehemu ya maandalizi ya sera hii. Tumeaminiwa kuwawakilisha wenzetu, hatuta wangusha, tutahakikisha tunatoka na sera nzuri ya Kijinsia ambayo italeta mabadiliko makubwa ya usawa wa kijinsia ndani ya chama chetu” amesema Ally.


Upande wake, Mwezeshaji kutoka TGNP, Deogratius Temba, alisema kwamba yeye amefkia  CUF kwaajili ya kuwezesha watendaji wa chama kutengeneza sera hiyo, na kwamba mchakato huu unafanywa na chama chenyewe sio TGNP au WiLDAF.

“Sisi hapa ni wawezeshaji tu, kazi hii inafanywa na chama chenyewe, tunawawezesha kutambua masuala ya Kujinsia na namna ya kuyaweka ili yaeleweke, tunawawezesha pia kuwa na uwezo wa jicho la kijinsia , baadaye wanayaweka kwenye sera, hapa mimi nimekuwa nikijibu maswali yao zaidi, ninaamini hiki kikosi kazi kitamaliza kazi kwa wakati na kuanza utekelezaji wa sera hii”alisema Temba

Mchakato huu umehusisha kupitia nyaraka za chama zikiwemo Ilani, Katiba, Kanuni, sera, program na nyaraka nyingine za kiuendeshaji ili kuangali kwa namna zilivyozingatia usawa wa Kijinsia.

Washiriki wa kikosi kazi cha kaundaa sera ya Jinsia ya CUF wakiwa katika Picha ya pamoja
washiriki wa kikosi kazi cha kuandaa sera ya Jinsia ya CUF wakiwa katika Picha ya Pamoja
washiriki wa kikosi kazi cha kuandaa sera ya Jinsia ya CUF wakiwa katika Picha ya Pamoja

washiriki wa kikosi kazi cha kuandaa sera ya Jinsia ya CUF wakiwa katika Picha ya Pamoja

 

Saturday, September 10, 2022

Vyama vinane vya Siasa vyaanza mchakato wa 
kuandaa sera ya Jinsia

Na Deogratius Temba

VYAMA vinane (8) vya siasa nchini Tanzania vimekutana na kujadiliana namna ya kuanza mchakato wa kuandaa sera ya Jinsia ndani ya vyama vyao ili kuweka misingi ya kuwezesha ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi wa kisiasa.

Vyama hivyo ni Chama cha Kijamii (CCK), Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Chama cha Wananchi (CUF), Chama cha ACT-Wazalendo, Chama cha Mapinduzi (CCM), ADA-TADEA, Chama cha Wakulima (AAFP), Alliance for Democratic Change (ADC), ambavyo vinaanza zoezi hili kwa awamu kama sehemu ya akutekeleza maazimio ya Baraza la Vyama vya Siasa nchini Tanzania.

Mchakato huu unaendeshwa kwa kuwezeshwa na wataalam wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) na Shirika la Sheria na Maendeleo Afrika (WiLDAF), ambao wanatekeleza mradi wa uwezeshaaji Wanawake kushiriki katika vyombo vya maamuzi na uongozi na siasa.

Kwa mujibu wa Baraza la Vyama vya siasa, Mpango wa awamu ya kwanza ya mchakato huu utavihusu vyama hivyo vinane vilivyoteuliwa kwa kufuata orodha ya Mpangilio wa kiherufi (A-Z) na baadaye vitafuata vyama vilivyobaki.

Tayari timu za wawezeshaji zimeshapangwa kwaajili ya kushiriki mchakato huo ndani ya vyama ambao unatarajiwa kuanza mapema wiki ijayo, na baadaye rasimu za sera za Jinsia kwa vyama hivyo vinane zitawasilishwa katika Baraza la Vyama vya siasa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya siasa kwaajili ya utekelezaji na ufuatiliaji.

Mwisho






MWANACHUO AJIKATA TUMBO BAADA YA KUMUUA MWANAFUNZI MWENZAKE DODOMA


Changamoto kubwa inayowasumbua vijana na jamii kwa ujumla ni kukosekana kwa uelewa juu ya umuhimu wa maisha ya mtu binafsi katika ulimwengu huu na wakati mwingine kupelekea watu wengine kuweka maisha yao rehani kwa watu wengine. 

matukio ya kujiua, kuua, kujeruhi, kuumiza, au kufanya vitendo vya Ukatili wa Kijinsia katika jamii vinashamiri sana na kwa kasi ya hali ya juu. Hii inatokana na kwamba, kuna ukosefu mkubwa wa maadili.  

Mwanafunzi wa Chuo cha St John, Winfrida Michael (24) amefariki dunia baada ya kuchomwa kisu na mpenzi wake Julius Gervas (26) ambaye pia ni mwanafunzi wa chuo hicho sababu ikitajwa kuwa wivu wa mapenzi.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Martin Otieno amesema tukio hilo limetokea Septemba 7,2022 baada ya Julius kufanya mauaji hayo alijaribu kujiua kwa kujikata tumbo na sasa anapatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa Mkoa wa Dodoma.

Ofisa muuguzi wa hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Ester Ngoloki amesema walimpokea Julius akiwa na jeraha la kuc

AKATWA PANGA BAADA YA KUWEKA PESA MEZANI AKIMWAGILIA MOYO SHINYANGA MJINI

Na  Mapuli Misalaba, Shinyanga


Mkazi wa mtaa wa Mwabundu kata ya Ndala Manispaa ya Shinyanga Charles Mayunga (38) amelazwa katika Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Shinyanga baada ya kujeruhiwa na kitu chenye makali kichwani na usoni akiwa kwenye klabu cha Pombe kata ya Ngokolo.

Tukio hilo limetokea Septemba 4,2022 majira ya saa sita mchana kata ya Ngokolo mjini Shinyanga.

Misalaba Blog imefika katika Hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga na kuzungumza na majeruhi huyo ambaye ameeleza kuwa alifika kwenye klabu cha Pombe akaweka fedha mezani shilingi elfu kumi na nane akaendelea kunywa ambapo inasadikika watuhumiwa hao walizitamani fedha hizo baada ya kukataa kuwanunulia Pombe.

Mayunga amesema kuwa aliendelea kunywa Pombe baada ya muda mfupi akaanza kushambuliwa hali iliyopelekea kupata majeraha kichwani na usoni.

“Nilitoka nyumbani nikaenda Ngokolo nikafika kwa muuza Pombe mmoja anaitwa Kofi wakati nimeagiza pale Pombe kumbe wale watu niliokuwa nao pembeni hela zangu wamezitamani mimi nikaendelea kunywa baada ya muda nikashangaa tu napigwa Panga nikaanguka nikapoteza fahamu”.


“Nilikuja nikiwa na hali mbaya sana yaani nilikuwa nikikaa najisikia kizunguzungu halafu na damu zilikuwa zikitoka kwa wingi ila namshukuru sana Dokta alivyokuja alinishughulikia hakuangalia sina hela wala nini mpaka sasa naona hali yangu ni nzuri”. Amesema Mayunga

Kwa upande wake mkuu wa idara ya kitengo cha upasuaji katika Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Shinyanga Dkt. Kambi Athuman Buteta amekiri kumpokea mgonjwa huyo siku ya jana akiwa na hali mbaya na kwamba baada ya kumpa huduma stahiki hali yake inaendelea vizuri.

“Tulimpokea akiwa amepata majeraha kichwani ya kupigwa na kitu chenye ncha kali alikuwa anatokwa na damu nyingi kichwani na tulimpatia huduma ya kwanza pamoja na kumsafisha na kumshona vizuri sasahivi anaendelea na matibabu na hali yake ni nzuri”.amesema Dkt, Kambi

Aidha kamanda wa jeshi la polisi Mkoa wa Shinyanga kamishna msaidizi polisi Janeth Magomi amesema bado hajapokea taarifa za tukio hilo.




CHANZO - Misalaba blog

APIGWA HADI KUFA NA MMEWE KISA KACHELEWA KURUDI NYUMBANI AKITAFUTA MAREJESHO YA KIKOBA

 Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma linamshikilia Peter Mwakiposile kwa tuhuma za kumuua mkewe Aisha Ramadhani mkazi wa Chidachi kwa kupigwa hadi kufa, kwa kosa la kuchelewa kurudi nyumbani akitafuta fedha za Marejesho la kikundi cha kikoba.



Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma ACP Martin Otieno ameeleza kuwa mtuhumiwa yupo chini ya ulinzi wakati akisubiri taratibu za kufikishwa mahakamani huku mwili wa marehemu Aisha Ramadhani ukiwa umehifadhiwa chumba cha kuhifadhia maiti kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kwa taratibu za mazishi.

Marehemu, Asha, wakati wa Uhai wake



Mama wa marehemu Aisha Ramadhani amesimulia kuwa alipigiwa simu na mkwe wake Peter Mwakiposile wakati akitekeleza unyama huo ambapo ilisikika sauti ya marehemu ikiomba msaada kitendo ambacho kilipuuzwa na mumewe huku watoto wa marehemu wakisema mama yao aliondoka nyumbani saa 12 jioni na kurudi saa 2 usiku baada ya kwenda kuomba fedha kwa rafiki yake kwa ajili ya rejesho

RAIS SAMIA ATUMA SALAMU ZA POLE KIFO CHA QUEEN ELIZABETH II

 Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesikitishwa na kifo cha Malikia Elizaberth II wa nchini Uingereza, kilichotokea jana Alhamisi Septemba 8, 2022 katika visiwa vya Balmoral nchini Scotland alipokuwa anapatiwa matibabu.


Hayati, Malkia Elizabeth II. enzi za uhai wake
Katika ukurasa wake wa Twitter, Rais Samia ameandika, “Nimesikitishwa na taarifa za kifo cha Malkia Elizabeth II. Kwa niaba ya Watanzania wote, natuma salamu za pole kwa familia ya Kifalme@RoyalFamily na raia wote wa Uingereza. Malkia atakumbukwa duniani kote kama nguzo ya Amani, Umoja na Utulivu.”

Thursday, September 8, 2022

Hali ya Upatikanaji na Umiliki wa Ardhi kwa wanawake

 

Hali ya Upatikanaji na Umiliki wa Ardhi kwa wanawake

 

Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia (2000) ilitoa kipaumbele katika eneo la upatikanaji, umiliki na utumiaji wa ardhi kwa usawa baina ya wanawake na wanaume. Umiliki na utumiaji wa ardhi ni nguzo muhimu katika suala zima la maendeleo ya wanawake kiuchumi.

 Hivyo, umiliki wa ardhi kwa wanawake ni muhimu katika kufikia fursa nyingine za kiuchumi nchini. nchini Tanzania, ni wanawake 26% wanamiliki ardhi ya kilimo (SIGI, 2020). Hali hii inatokana na kuendelea kuwepo kwa mila na desturi zinazowapendelea wanaume kurithi na kumiliki ardhi ya familia ambapo wanawake hupata fursa hiyo kupitia wanaume ndani ya familia.

Serikali imeendelea na jitihada za kisera ili kuhakikisha kuwa umiliki wa ardhi unazingatia usawa wa kijinsia. Sera hizo ni pamoja na Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Makazi (2000), Sera ya Taifa ya Ardhi (1995), Ibara mbalimbali za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) na Dira ya Maendeleo 2025. Jitihada nyingine ni pamoja na Marekebisho ya Sheria ya Ardhi ya Vijiji Na. 5 ya mwaka 1999 kifungu cha 3 (2) ambayo inatoa fursa kwa kila mwanamke kumiliki na kutumia ardhi na kuanzisha Kamati za kuhamasisha haki za wanawake kumiliki ardhi mwaka 2017. Kutokana na jitihada hizi, mwaka 2018 jumla ya hati 80,000 za umiliki wa ardhi zilisajiliwa.

Jitihada hizi zimewezesha kuongezeka kwa idadi ya wanawake wanaomiliki ardhi kutoka asilimia 9 hadi asilimia 25 na kuongezeka kwa umiliki wa pamoja kutoka asilimia 6 hadi asilimia 16; kuongezeka kwa watu wenye hati miliki zinazotambulika kisheria kutoka asilimia 50 mwaka 2016 hadi asilimia 59 mwaka 2018; kuongezeka kwa idadi ya hati za kimila za umiliki wa ardhi mfano, katika Mkoa wa Iringa pekee jumla ya hati za kimila 3,208 zilitolewa (1,970 Wilaya ya Kilolo na 1,238 Wilaya ya Mufindi). Hii ni matokeo ya uwezeshaji wa Shirika Lisilo la Kiserikali la Haki Ardhi linalohamasisha uandaaji wa mipango ya matumizi bora ya ardhi katika vijiji 7 katika Wilaya ya Mufindi na 11 katika Wilaya ya Kilolo.



Pamoja na mafanikio yaliyopatikana, suala ya umiliki wa ardhi na rasilimali nyingine za uzalishaji limeendelea kuathiri maendeleo ya wanawake ambapo licha ya kuwa na sheria zinazowalinda wanawake katika kumiliki rasilimali bado mila na desturi kandamizi ni kikwazo. Umiliki wa rasilimali za kiuchumi kwa wanawake kama vile pato la familia, ardhi, vitendea kazi na mikopo umeendelea kuwa mdogo ukilinganisha na wanaume. Pamoja na ukweli kwamba wanawake wanachangia Katika sekta ya kilimo uvuvi na misitu, wanawake wamachangia asilimia takribani asilimia 67 (ILFS, 2014).

Kiwango cha uzalishaji kwa wanawake katika sekta ya kilimo ni kidogo ikilinganishwa na wanaume. Hii ni kutokana na matumizi ya zana duni kama vile jembe la mkono. Sheria ya Mirathi ya Kimila (1963) inazuia wanawake, wajane na wasichana kurithi ardhi na hivyo kuwakosesha fursa za kumiliki rasilimali za kiuchumi na uwekezaji. Hivyo, maboresho katika sheria ni muhimu katika kuwawezesha wanawake kuboresha hali zao za kiuchumi na kijamii. Kwa msingi huo, ni muhimu kuiwezesha jamii kushiriki na kuwa na uelewa wa haki za wanawake kurithi mali ikiwemo ardhi.

Wednesday, September 7, 2022

Wajibu wa Mzazi au mlezi kulinda haki za Mtoto Kisheria

 

Wajibu wa Mzazi au mlezi kulinda haki za  Mtoto Kisheri

Na Mwandishi wetu

Tumeshuhudia matukio mengi katika jamii yetu ya watoto kunyanyaswa na kudhalilishwa na watu wazima wakiwemo walezi na hata baadhi ya wazazi wasio waadilifu.

Imekuwa kawaida kusikia watoto yatima au wanaolelewa na watu wa karibu kama sana  wakitendewa vitendo vya uonevu baada ya wazazi wao kufariki. Ndugu na jamaa, bila haya, wamekuwa wakifanya maamuzi yanayowahusu watoto bila kuzingatia maslahi na haki za watoto.

Unyanyasaji wanaofanyiwa watoto, wakati mwingine unafanyika kwa sababu wazazi, walezi na hata jamii kwa ujumla hawafahamu wajibu walionao kwa mtoto kisheria. Kutokujua namna mtoto anavyolindwa kisheria kunaweza, kwa namna moja au nyingine, kuchochea vitendo hivi.

Katika [blogu] hii kila Alhamisi, tunakusudia kukuletea dondoo muhimu kama zinavyoainishwa kwenye sheria ya Mtoto Na. 21 ya 2009 iliyotungwa kwa minajili ya kulinda maslahi na ustawi wa mtoto.

Sheria hii ilitungwa na serikali yetu kukidhi matakwa ya mikataba ya kimataifa inayomhakikishia mtoto haki zake za msingi. Lakini pia sheria na. 21, inatekelezwa sambamba na sheria Sheria ya kanuni za adhabu  sura ya 16 (SOSPA 1998), Sheria ya ndoa ya mwaka 1971, Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 na Sheria ya Elimu ya Elimu ya mwaka 1978. Kwahiyo watu wasifikiri kwamba watapona endapo sheria zitasimamiwa vizuri. Kuna vifungu na adhabu za kutosha kwa mtu anayefanya Ukatili wa Kijinsia kwa watoto.

Kwa mhutasari, sheria na. 21 ya mwaka 2009, yaani sheria ya mtoto  hii inalenga kumwekea mtoto mazingira ya kukua na kustawi katika nyanja zote za kimaisha bila kudhalilishwa, kuonewa na kunyanywaswa na jamii ikiwemo familia yake. Ingawa msisitizo ni kumlinda mtoto zaidi, sheria hii pia inafafanua wajibu wa mtoto kwa familia na jamii kwa ujumla.

Labda tuanze na tafsiri ya mtoto. Mara nyingi tumetumia neno ‘mtoto’ kumaanisha mambo mengi kwa wakati mmoja. Kwa mfano, unaweza kushangaa mzee wa miaka 55 anajitambulisha kama ‘mtoto’ wa tatu katika familia yake. ‘Mtoto’ huyu wa tatu, naye anaweza kuwa na ‘watoto’ kadhaa wenye umri wa utu uzima.

Hapa mtoto maana yake ni nini? Mtoto, katika mazingira hayo, ni mtu aliyezaliwa na mtu mwingine bila kujali umri wake. Tafsiri hii inazingatia uhusiano wa mzazi na mwanae bila kujali umri.

Kadhalika, unaweza kusikia mtu mwenye miaka 40 akidaiwa kufanya mambo ya kitoto. Utoto, kwa mazingira hayo, ni kufanya vitendo visivyoakisi uwezo wa mtu mzima anayejitegemea. Jamii inakuwa na matarajio fulani kwa mtu anayejitambulisha kama mtu mzima. Anatarajiwa kufikiri kwa namna fulani, kufanya vitu kwa namna fulani na hata kuonekana kwa namna fulani.

  Mchoro huu unao onyesha Ukatili wa watoto ni kwahisani ya TGNP 

Inapotokea mtu mzima huyu anashindwa kukidhi matarajio hayo, watu humtazama kwa jicho la ‘utoto.’ Utoto ni sifa mbaya kwa mtu mzima.

Lakini, kidini tunaambiwa ‘msipokuwa kama watoto wadogo hamuwezi kuurithi uzima wa milele.’ Mtoto, katika mukhtadha huu, si sifa mbaya. Tabia za kitoto kimsingi ni sharti muhimu la kumpa mtu sifa za kuuona ufalme wa mbinguni.

Hata hivyo 'mtoto' huyu anaelekezwa kuendelea kukua na kuongezeka ili awe na sifa ya kujitegemea na kuwategemeza wengine. Haifai kuendelea kuwa 'kama watoto wachanga' wanaoendelea kuwategemea wengine. Jambo hili linaelezwa kisaikolojia pia.

Kisaikolojia mtoto anaweza kuwa mtu yeyote bila kujali umri wake ambaye bado anaendelea kukua kiakili, kimwili, kiroho na kimahusiano. Hata hivyo, mtu mwenye miaka pungufu ya 12 ana nafasi kubwa ya kuwa na sifa hizi.

Sababu kubwa ni kuwa katika umri huo, mtu huyu bado anaendelea kukomaa na kupevuka kiakili, kimwili, kiroho na kimahusiano. Ndio kusema mtu ambaye bado hawezi kujitegemea kimwili, kiakili, kiroho na kijamii, ana sifa za kuitwa mtoto.

Kwa kuwa tafsiri za ‘mtoto’ na ‘utoto’ zinaweza kuwa na mkanganyiko mkubwa kama tulivyouona hapo juu, sheria hii imetumia kigezo kimoja cha umri kumtambua mtu mwenye sifa za kuitwa mtoto.

Mtoto, kwa mujibu wa sheria hii, ni mtu yeyote mwenye umri wa chini ya miaka 18. Haijalishi amepevuka akili kiasi gani, maadam ana umri usiozidi miaka 18 mtu huyo bado ataendelea kutambuliwa na sheria hii kama mtoto. Yapo mashirika yanayofanya kazi ya usaidizi kwa vitendo vya Ukatili ambayo baadhi ni: TWALA, WILDAF, WILAC, TAMWA, CRC, KIWOHEDE, Maafisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri zote, Maafisa maendeleo ya jamii wa halmashauri zote ambao pia wapo kwenye ngazi ya Kata. Kamati za Ulinzi wa mama na mtoto za Wilaya, Kata na Vijiji, Viongozi wa Dini. Zaidi pia simu bure namba. 116.

WAZAZI WASIO WAJALI NA KULINDA WATOTO KUCHUKULIWA HATUA- WAZIRI GWAJIMA

 

WAZAZI WASIO WAJALI NA KULINDA WATOTO KUCHUKULIWA HATUA- WAZIRI GWAJIMA

Na Mwandishi Wetu

SERIKALI imetangaza kuwachukulia hatua kali za kisheria wazazi na walezi watakaoshidnwa kutekeleza wajibu wao wa kisheria wa kuwalea na kuwalinda watoto na kusababisha kufanyiwa vitendo vya Ukatili wa Kijinsia kutokana na kuzurura hovyo mitaani na kufanya shughuli mbalimbali za ajira kinyume na sheria.

ameahidi   kuwachukulia  hatua  kali   za  kisheria   wazazi  na  walezi   wote   watakaobainika  kuwaachia   watoto  kuondoka    nyumbani  na   kuingia   mitaani  na  kufanya   shughuli  mbalimbali .

hayo yamesemwa na, Waziri wa Maendeleo  ya Jamii, Jinsia , Wanawake  na Makundi  maalum  Dkt . Doroth  Gwajima,  jijini  Dar es  Salaam,   wakati  akifungua   mkutano  wa  siku  mbili uliuowakutanisha   wadau  wa  huduma  za Ustawi   wa  Jamii nchini.

Waziri Dorothy Gwajima


Katika  mkutano   huo  Dkt.  Gwajima  amesema  serikali   ya  awamu   ya  Sita  kupitia   wizara   ya  Maendeleo  ya   Jamii, Jinsia,  Wanawake  na  Makundi   Maalum  kwa   kuungana   na  wadau   wote   wa  ustawi  wa   jamii   wanakuja  na   mpango  maalum  utakaofanikisha  kuondoa   mtandao  mzima unaofanikisha  kuzagaa   kwa  watoto  mitaani  katika   miji  mbali mbali  hapa   nchini .

Aidha   waziri   huyo   pia  amesema    wizara   yake  imeona   kuna   umuhimu   wa  kutungwa  kwa  sheria   maalum  itakayo  komesha  vitendo   vya   baadhi   ya  watu  wenye  ulemavu   wanaotuimia   viti   vyenye   magurudumu   kutumia   ulemavu   wao   kwa  kuomba omba   kitendo   alichosema  kinaongeza  kundi   la  Ombaomba  mitaani.

Kwa  upande  wake  Mkuu   wa   Mkoa  wa  Dar   es Salaam   Amos  Makalla akizungumza  katika  mkutano  huo  amesema   kwa  kushirikiana   na   wizara   ya  Maendeleo   ya  Jamii, Jinsia, wanawake  na  Makundi   Maalum  tayari   wanampango kazi   la  kuwajengea   mazingira  mazuri  ya  kuwatambua watoto  wa  mitaani  na  omba omba  kwa   kuangalia  mahala   watakapopelekwa  mara  baada  ya  kuondolewa  mitaani.

Mhe. Waziri akiwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhe. Zainab Chaula na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, wakizindua vijitabu viwili vya miongozo ya namna ya kulea watoto.


Mkutano  huo  wa   wadau wa huduma   za  Ustawi   wa Jamii umekwenda  sambamba  na  uzinduzi   wa   vitabu   viwili  ikiwemo  kitabu   cha   Kanuni  za  Maadili  ya   kufanya  kazi   na watoto pamoja  na  uzinduzi  wa kitabu  cha  kiongozi  cha  penzi  kitakachosaidia   kutoa   muongozo  katika  vituo vya  kulelea  watoto  mchana .

 

Mhe. Amos Makala, Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mkakati huo.

Kwa mujibu wa sheria ya Mtoto ya mwaka 2009, ni wajibu wa mzazi kuhakikisha mtoto anapata ulinzi, anakuwa salama, anatunzwa na kulelewa katika mazingira salama na asifanyiwe kitendo cha Ukatili au udhalilishwaji hadi atakapotmiza umri unaoatakiwa kisheria kuwa sasa amekuwa mkubwa. Kuhsindwa kutimiza wajibu ho na mengine yaliyoainishwa kwenye sheria hiyo ni kosa.

 

Thursday, September 1, 2022

Kwanini ni muhimu kuondoa kodi kwenye taulo za kike?

 

Kwanini ni muhimu kuondoa kodi kwenye taulo za kike?

Uchambuzi umefanywa na Deogratius Temba

Mnamo mwezi Julai 2018, Serikali ya Tanzania ilipotoa msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa Taulo za Kike ilitoa ujumbe wa wazi kwamba bidhaa hizi ni hitaji la Msingi la Haki za binadamu nani la lazima kwa wasichana na wanawake.

Katika Hotuba ya Bajeti ya mwaka wa fedha 2018/2019, Waziri wa Fedha wakati huo, Dkt Philipo Mpango akasisitiza kwamba wanawake na hasa wasichana wa shule wanaotoka katika familia masikini wanahitaji kupata taulo za kike kwa bei nafuu na rafiki ili waweze kujisitiri  na kuhsiirki kwenye masomo au shughuli za uzalishaji wakiwa salama.

 Ilikuwa ni hatua kubwa muhimu kuelekea usawa wa kijinsia, na kupunguza ‘Umasikini wa Hedhi’. Hatua hii ilisherehekewa katika jukwaa la kitaifa na kimataifa. Tanzania ni kati ya nchi chache vinara kutekeleza mpango huu, ikiiipiku nchi ya Australia (ambayo imeondoa kodi Januari 2019), na nchi nyingine za ukanda na duniani.  


Picha hii imepatikana kwa hisani ya Mtandao

 

Hatua hii ni muafaka kwa uchumi, na ingechangia viwango wa ukuaji wa Taifa. Hata hivyo, Benki ya Dunia inakadiria kwamba, kwa kila uwiano wa ongezeko la asilimia moja ya idadi ya wanawake wenye elimu ya sekondari,  pato la nchi la mwaka hukua kwa  asilimia 0.3.            

Kwa nini Msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ni muhimu na Ubaki

Msamaha wa kodi ya ongezeko la Kodi ya Thamani (VAT) kwenye taulo za kike ni muhimu kwa sababu kuu mbili, ikihusianishwa na usawa wa kijinsia na pia unafuu wa Taulo za Kike. Kuhusu usawa wa jinsia, wanawake na wasichana hawana hiari juu ya Hedhi. Kuanzia umri wa miaka 13 – 55 wataingia kwenye Hedhi kwa kadiri ya wiki nzima, kila mwezi.

Kulipa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika bidhaa za hedhi kunawafanya wanawake kulipa kodi ya ziada wakilinganishwa na wanaume kiuhalisia kutokana na hali yao ya kibaiolojia, kodi iko kwa watu wa jinsi moja.   Kuhusu unafuu, msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani una uwezo wa kupunguza gharama ya taulo  za kike kwa asilimia 18, ambalo linaweza kuchangia bidhaa kupatikana kirahisi kwa wanawake na wasichana nchini kote. Ni muhimu bidhaa hizi zikawa nafuu ili kuwasaidia wanawake na wasichana kudhibiti Hedhi kwa usafi na utu.    

Hedhi isichukuliwe kama njia ya kuongeza mapato, badala yake upatikanaji wa bidhaa za hedhi uchukuliwe kama suala la haki za binadamu na uswa wakijinsia, na iwe hivyo.  Serikali kuondoa VAT si tu inatambua bidhaa za hedhi kwamba ni bidhaa ‘muhimu’, lakini pia inawasaidia wanawake na wasichana kuzipata kwa unafuu na hivyo kupunguza vikwazo wanavyokutana navyo kielimu na kiajira.


Athari ya Kuondolewa kwa VAT kwenye Soko

Uchunguzi wa awali unaonyesha matokeo mbali mbali juu ya kuondolewa kwa VAT.  Kuna tatizo kwenye msimamo wa bei unosababishwa na mnyororo wa usambazaji, ambao humwacha muuzaji wa rejareja kuamua bei ya mwisho. Changamoto kubwa ikiwa ni uzingativu wa bei kwenye bidhaa zinazonunulika haraka kutokana na mfumo uliozoeleka. Hata hivyo kutokana na kuondolewa na kwa VAT bidhaa za pedi zenye majina makubwa kama Always na HC walithibitisha kushuka kwa bei kwa asilimia 20. Bidhaa nyingine pia zilionyesha kupunguza bei kwa viwango tofauti, japo kwa kiasi kidogo.

 

Kwa kawaida wauzaji wa rejareja ndio huchukua kiwango kikubwa cha faida kwenye mnyororo wa usambazaji, na wao ndio wanabeba hatari na dhamana ya biashara na ndio wenye ushawishi mkubwa juu ya bei ya mwisho (bei ya mlaji). Hatimaye, pamoja na msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani, kunatakiwa pia kuwepo na kanuni na njia madhubuti za ufuatiliaji kuhakikisha wauzaji wa rejareja  wanazingatia  bei elekezi. Ushawishi wa bei ya rejareja ni jambo linalohitaji mbinu, muda na uwekezaji na wadau kwa ajili ya kupeana taarifa.

Utafiti wa awali uliofanywa Morogoro na Mbeya[1] uliohusisha maduka 2,906 yanayouza taulo za kike (yakiwemo ya rejareja, ya jumla, maduka ya dawa), inaonyesha kwamba bei ya bidhaa moja ikitofautiana kwa asilimia 40 kutoka kwenye duka moja na jingine. Asilimia 52 inaonyesha pakiti moja ya pedi ikiuzwa kwa Shilingi 2,000/=, Asilimia 13 zikiuzwa kwa shilingi 1500/= na asilimia 28 zikiuzwa kwa zaidi ya shilingi 2500/=.

Wahamasishaji wa Bei:  Pia, Utafiti huu unaonyesha kwamba wakati mwingine bei inakuwa thabiti zaidi sehemu ambapo duka kuu linauza bidhaa kwa bei ya chini kwa eneo husika. Hii inatoa fursa ya ushirikiano kati sekta ya umma na binafsi na wahamasishaji wa bei katika kushusha bei katika maeneo ya jirani. Hasa, mara watumiaji wanapojua kuna maeneo yanayoshindana wanayoweza kununua bidhaa, wana uwezo wa kuwa nguvu kubwa ya kuleta ushindani katika soko, na kusababisha bei kushuka.

Utafiti wa awali wa soko unaonyesha kuwa msamaha wa kodi ya VAT ulianza kupunguza bei. Hata hivyo, sera ya msamaha wa kodi ya VAT imetekelezwa kwa muda mfupi chini ya mwaka mmoja, na huu sio muda wa kutosha kuelewa na kupima athari zake.

 

Mapendekezo ya wadau ili kurudisha msamaha wa kodi kwa pedi

Ni muhimu msamaha wa VAT kubaki Tanzania. Hii ni hatua ya awali muafaka ya upunguzaji wa gharama za bidhaa za Hedhi. Ikiwa wanawake na wasichana watakuwa na uwezo wa kumudu gharama za pedi, haya yatakuwa ni mapinduzi makubwa yatakayowawezesha kutumia muda wao kwenye kazi za uzalishaji na kielimu, na pia kuboresha afya zao.

 Kwa ujumla wake hayo yote yatachangia kwenye ukuaji wa uchumi wa Taifa, kupunguza mzigo kwenye sekta ya afya, na pia kuhakikisha wanawake na wasichana wanatoa mchango kwenye sera ya viwanda na Dira ya maendele ya Taifa ya 2025.

 

Ili Msamaha wa kodi ya VAT uweze kufanyakazi kama ilivyotarajiwa ni vyema serikali na sekta binafsi kufanyakazi kwa karibu, kuhakisha utekelezwaji wa ushushaji wa bei. Pia usimamizi kwenye serikali za mitaa kunaweza kuleta tofauti katika kuongeza uelewa na utekelezaji. Wauzaji wa rejareja waelimishwe kwamba bidhaa za Hedhi ni bidhaa muhimu kwa akina mama na si anasa.  Pia, Serikali na Sekta binafsi itumie fursa ya kuona matokeo chanya ya kufanyakazi pamoja ili kuleta matokeo mapana, vile vile watumie washawishi kwenye jamii.

 

Kuhamasisha watumiaji na kuwaeleza juu ya msamaha wa VAT na kuwapa bei elekezi, itachagiza bidhaa kushuka bei hasa kwa wauzaji wa rejereje na itaongeza msukumo kwa wauzaji wa rejareja kushusha bei ya bidhaa yenyewe. Kampeni za kitaifa zinaweza kusaidia jitihada hii, ikiambata na kutengeza hitaji kubwa katika soko.

Pamoja na kwamba Serikali imependekeza punguzo la asilimia 5 ya kodi ya Makampuni. Hii ina hatari ya kutoweza kubadilisha bei za pedi ikiwa hakuna kanuni na ufuatiliaji wa bei, wanfanya biashara wa reja reja wanaweza kuendelea kujiongezea faida. Mwaka ujao wa fedha 2023/2024 uwe ni fursa nyingine ya kuendelea kuwa na msamaha wa kodi ya VAT kwa Taulo za Kike, na kufuatilia athari yake kwa karibu ili vikwazo viweze kutatuliwa.  Tanzania inatakiwa kuendelea kuwa kinara wa dunia kwenye jambo hili ili wengine wafuate na wajifunze kwetu.  Uchambuzi umefanywa na Deogratius Temba-0784686575