Thursday, October 27, 2022

TGNP yapongeza Kikosi kazi cha Rais Samia

 TGNP yapongeza Kikosi kazi cha Rais Samia

Na Mwandishi wetu, Dar

Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), imepongeza Kikosi kazi kilichoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa mapendekezo yaliyotolewa, kwa lengo la kuboresha demokrasia ya vyama vingi nchini.

Bi. Lilian Liundi, Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP


Taarifa iliyitolewa Jijini Dar es salaam, na Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Bi. Lilian Liundi imeeleza kwamba:-  “…Kikosi kazi hiki kupitia Mwenyekiti wake, Prof. Rwekaza Mukandala, kimeweza kukabidhi taarifa yake kwa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan yenye mapendekezo 18, ikiwemo mapendekezo yenye lengo la kuongeza ushiriki wa wanawake na makundi yaliyo pembezoni katika uongozi na siasa. Miongoni mwa mapendekezo hayo ni pamoja na

       I.            Pendekezo la. 5: Katika uteuzi wa wajumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi walau wajumbe wawili wawe wanawake, na sifa za kuwa Mwenyekiti, Makamu au Mjumbe ziainishwe.

    II.            Pendekezo la 11: Sharti la uwepo wa Sera ya Jinsia kwenye Chama cha Siasa na ujumuishi wa makundi maalumu. Utararibu wa Viti maalumu uendelee ila sheria ziboreshwe na kuweka ukomo wa miaka 10 na pia, ushiriki wa wanawake katika vyombo vya maamuzi usipungue asilimia 40.

 III.            Pendekezo na. 12: sheria zinazo kwamisha ushiriki wa watu wenye ulemavu kwenye siasa ziangaliwe upya

 IV.            Pendekezo na. 13: juhudi za ushirikishwaji wa vijana kwenye siasa ziongezwe

Ni matumaini yetu kuwa mapendekezo haya yatachukuliwa na kutekelezwa kwa haraka ili kuweza kufikia malengo ya kuwa na demokrasia ya vyama vingi jumuishi na itakayoleta tija katika maendeleo ya taifa letu.

Kipekee, tunatoa pongezi pia kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa kwa kuwa sehemu ya mchakato huu kwenye kikosi kazi na kuweza kubeba na kuhakikisha ajenda ya masuala ya jinsia yanajitokeza katika mapendekezo hayo.

Ikumbukwe kuwa, mnamo mwezi Februari mwaka huu, chini ya mradi wa kuongeza ushiriki wa wanawake katika uongozi unaotekelezwa na TGNP kwa kushirikiana na WiLDAF, tuliweza kufanya kikao cha mashuriano na Baraza la Vyama vya Siasa, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Kikosi Kazi hiki cha Kuratibu maoni ya wadau kwa lengo la kuangalia mapengo ya kijinsia ndani ya vyama vya siasa na kukubaliana namna bora ya kuziba mapengo hayo ili kuongeza ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi na maamuzi ndani na nje ya vyama vya siasa.  Miongoni mwa mapendekezo yaliyotoka katika kikao chicho cha mashauriano ni pamoja na uwepo wa Sera ya Jinsia katika vyama vya siasa.


Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, akipokea taarifa ya mapendekezo ya kikosi kazi kutoka kwa Mwenyekiti wake, Prof. Rwekaza Mkandala, Ikulu Jijini Dar es salaam

TGNP tunaendelea kufanya kazi kwa ukaribu na Baraza la Vyama vya Siasa na Ofisi ya Msajili katika kufuatilia utekelezaji wa mapendekezo hayo yaliyotolewa na kikosi kazi na kuhakikisha kuwa kwa pamoja tunaweka misingi imara ya kuongeza ushiriki wa wanawake katika uongozi wa siasa na ngazi za maamuzi.   Tunatambua mchango wa Kikosi Kazi, Baraza la vyama vya Siasa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa katika kuleta mabadiliko na usawa wa kijinsia nchini.

 

Mhe. Rais, Samia Suluhu Hassan akiwa na wajumbe wa Kikosi kazi Ikulu Dar es saalam

No comments:

Post a Comment