Tuesday, October 18, 2022

Mambo ya kuzingatia kabla na wakati wa kuandika wosia

 Mambo ya kuzingatia kabla na wakati wa kuandika wosia

Hapo awali nilikuwa nikiamini kuacha wosia ni uchuro yaani kujitakia au kujitabiria kifo chako mwenyewe. Hii ilipelekea nikaogopa mnoo inapotokea nikisikia habari zinazohusu masuala ya wosia. Hali kadhalika ninaamini pia wapo watu wengi wanaoogopa kuacha wosia kwa dhana hii hii kwamba ni uchuro wa kujitabiria kifo.

Wengine nao huamini ya kwamba wosia unaachwa na watu wasomi au wazee au wanaume au wanaokaribia kufa au wenye uwezo mkubwa kwenye kumiliki mali kama vile nyumba, viwanja, hisa kwenye makampuni au pesa katika akaunti za Benki na kadhalika.

Yote hayo yatajibiwa na makala hii hatua kwa hatua ambapo nitaangazia kwa ufasaha ni nini maana ya wosia kwa jicho la kisheria zaidi, aina zake, sifa, pamoja pia na faida. Tutaweza pia kuangalia japo kwa uchache wosia unatakiwa uweje.

Nini basi maana ya wosia?

Wosia ni tamko lenye nguvu kisheria ambapo mtoa wosia anakusudia ni namna gani mali yake au zake zitasimamiwa baada ya kifo chake. Katika wosia mtoa wosia anaweza kuelezea ni kwa namna gani mali yake au zake zitagawanywa kwa warithi wake, kiwango ambacho watagawiwa, orodha ya mali anazomiliki, orodha ya wadai na wadaiwa, namna gani atazikwa na kadhalika.

 Hiyo ni baadhi tu ya orodha ya mambo yanayotakiwa yawepo katika wosia na ni vyema kila jambo ambalo ni muhimu kuandikwa katika wosia ili kuondoa utata. Ikumbukwe kuwa mwacha wosia hatakuwa hai ili aweze kuulizwa kuhusiana na wosia wake wakati utakapoanza kutumika hivyo basi ni vyema uandikwe kwa lugha iliyo wazi na yenye kueleweka vizuri. Utata wowote utakaojitokeza unaweza kupelekea wosia kubatilishwa na wosia huo utakuwa batili automatiki.

Ikumbukwe ya kuwa kutokuacha wosia au kuacha wosia wenye dosari itapelekea mali utakazoacha kugawanywa kwa utaratibu wa wasioacha wosia. Utaratibu huu unaweza ukawa sio rafiki sana kwani wakati mwingine unaweza kwenda kinyume kabisa na matakwa ya mtoa wosia.

Aina za wosia

Wosia wa mdomo

Huu ni wosia unaotolewa kwa maneno ya mdomo yaani ‘Oral will’. Japokuwa aina hii ya wosia ni ngumu wakati mwingine kuthibitishwa  lakini sharia inautambua kuwa ni wosia kama vile ulivyo ule wa maandishi. Kwa mfano, Local Customary Law (Declaration) (No. 4) Order, 1963 inataka wosia huu ni lazima utolewe wakiwepo mashahidi wanne (4) yaani wawili wawe ni ndugu na wawili wasiokuwa ndugu. Mke au wake za marehemu, kama anaye au anao, ni lazima awe nyongeza  ya mashahidi hao. Kigezo hiki kisipofuatwa basi wosia huo utabatilishwa kweupee.

Wosia wa maandishi

Huu ni wosia unaotolewa kwa njia ya maandishi. Wakati mwingine unajulikana kama wosia rasmi. Lengo lake ni sawa tu kama lilivyo la wosia wa mdomo kama nilivyoeleza hapo juu. Umakini wa hali ya juu sana unatakiwa uzingatiwe katika kuandika wosia huu.

Ni lazima ‘legal formality’ yaani matakwa ya kisheria yafuatwe wosia wa aina hii unaopoandikwa. Baadhi ya matakwa hayo ni kama vile ni lazima uwe kwa maandishi na kusainiwa na mtoa wosia huo mbele ya mashahidi, ushuhudiwe angalau na mashahidi wawili na ni vizuri mmoja kati yao akawa ni nduguye mtoa wosia; mashahidi hao wanaweza kuzidi wawili ila tu wasipungue.

Wosia wa maandishi unaweza ukabatilisha wosia uliotolewa awali kwa mdomo, isipokuwa wosia wa mdomo hauwezi kubatilisha ule wa maandishi.  Na anayeweza kufanya hivyo ni mtoa wosia peke yake na si mtu mwingine.

Wosia uliotolewa na watu wawili kwa lengo la pamoja

Huu unaitwa kwa lugha ya kitaalamu ‘a mutual will’. Wosia huu unatolewa na watu wawili wenye malengo ya pamoja kama nilivyodokeza hapo juu kwa maana ya kwamba wote wanakubaliana jambo au mambo yanayofanana.

Wosia huu unapendelewa sana na walio katika mahusiano ya kimapenzi kama vile wanandoa. Kwa mfano kwenye wosia huu wanaweza wakakubaliana katika wosia huo ya kwamba yeyote atakayetangulia kufariki kati yao basi mali zitaenda kwa yule aliyebakia hai, kama vile mume akitangulia kufariki basi mali walizonazo zitamilikiwa na mke na kinyume chake, halafu wanaweza pia kukubalia namna gani watoto wao watapata urithi baada ya wote kufariki.

Hii ijulikane ya kwamba makubaliano haya kama yalikwisha kuwekwa hakuna namna yanaweza kubadilishwa kama mmoja wapo wa watoa wosia huo kashafariki.

Wosia wa masharti fulani

Unaweza ukauitwa ‘Conditional will’ ambapo masharti fulani aliyoyaweka mtoa wosia na ni lazima yatimizwe kwanza ndipo tunaweza kusema wosia una nguvu kisheria. Msharti haya yanatakiwa yawe ni yale yanayotekelezeka.

Kwa mfano mtoa wosia anaweza kusema nyumba hii apewe Comfort pindi atakapooa au atakapoweza kupata Shahada yake ya kwanza ya Sheria, hivyo basi ikiwa mtoa wosia huo amefariki  nyumba hiyo haitokwenda kwa Comfort mpaka atakapokuwa ameoa au kupata Shahada yake ya kwanza ya Sheria.

Mambo ya msingi yanayotakiwa kuzingatiwa wakati wa kuandaa wosia

Wosia ni lazima uwe na mambo yafuatayo vinginevyo inaweza kupelekea ukabatilishwa na mpango wa kugawanya mali bila wosia ukachukua nafasi. Mambo hayo ni kama vile:

1. Mtoa wosia ni lazima kisheria awe na uwezo wa kuacha wosia. Hapa nina maana ya kwamba sharia inahitaji mtu anayetoa wosia awe na umri wa miaka isiyopungua kumi na minane (18). Pia anatakiwa awe na akili timamu wakati wa kuacha wosia huo. Hali kadhalika mtu mwenye matatizo ya akili anaweza kuandika wosia pindi tatizo hilo limemwondoka kwa mfano endapo atakuwa anasumbuliwa na tatizo la ukichaa wa muda ‘temporary insanity’. Mtu akiwa na akili timamu na akaandika wosia lakini baadae akapata ukichaa wosia ule hautokuwa batili kwani wakati anauandika alikuwa na utimamu wa akili.

2. Mtoa wosia ni lazima afahamu yale yaliyoandikwa katika wosia. Kwa mfano mwacha wosia kaandikiwa wosia eidha na wakili au mtu yeyote ni lazima afahamu yale yaliyoandikwa ndani kabla hajaweka saini.

3. Wosia ni lazima utaje majina ya mtoa wosia.

4. Wosia unatakiwa utaje atakaye simamia mirathi.

5. Wosia ni lazima uwe na tarehe ya siku wosia huo ulipoandaliwa.

6. Wosia ni lazima utaje aina na kiwango cha thamani ya mali zinazotolewa katika wosia. Kama kuna kitu kinamilikiwa na watu wawili au zaidi basi ni sharti hilo libainishwe katika wosia.

7. Wosia unatakiwa utaje idadi ya warithi na wanufaika wa mirathi hiyo.

8. Wosia unatakiwa utilie maanani vipi itakapotokea mrithi au warithi na mnufaika au wanufaika watakapofariki kabla ya mtoa wosia.

9. Wosia unatakiwa utilie maanani ndoa inayoweza kufungwa baada ya wosia kuandaliwa. Ndoa itakayofungwa baada ya wosia kuandikwa inaweza kuathiri wosia huo.

10.         Wosia ni lazima usainiwe na mtoa wosia mbele ya mashahidi.

11.         Wosia ni lazima uthibitishwe na mashahidi.

12.         Mtoa wosia ni lazima aonyeshe ya kuwa ameandika wosia huo akiwa na akili timama pia bila kushurutishwa.

13.         Lazima katika wosia kuwe na kipengele kinachoonyesha ya kuwa mtoa wosia akibatilisha wosia wowote alioutoa awali.

14.         Endapo mtu ambaye kwa kawaida alitakiwa kupewa sehemu ya mirathi lakini hakutajwa katika wosia basi ni vyema sababu zikatolewa.

15.         Endapo mambo haya yatazingatiwa itapunguza kwa kiasi kikubwa matatizo yanayoweza kutokea baadae mtoa wosia atakapokuwa amekwisha fariki, mfano, wosia huo kukataliwa au kubatilishwa kwa kutokufuata taratibu kama nilivyokwisha kuelezea kwa uchache hapo awali.

Muhimu: Ifahamike ya kwamba hakuna fomula maalumu ya kuandika wosia lakini endapo utazingatia mambo niliyoyataja hapo juu basi wosia wako utakuwa una nguvu kama wosia mwingine wowote.

Faida za kuacha wosia

·         Humsaidia mtoa wosia kupanga ni namna gani mali yake itakavyosimamiwa baada yakufariki kwake. Endapo atafanya hivyo basi itamzuia mtu asiyehusika kuingilia mali zake pindi atakapofariki.

·         Kuepuka mali alizoacha kugawanywa kwa utaratibu wa asiyeacha wosia. Upoutaratibu ambapo mtu asiyeacha wosia mali zake kugawanywa kinyume cha matakwa yake kama nilivyoeleza hapo awali hivyo basi ili kuepusha jambo kama hili kutokea ni vyema kabisa ukajiwekea utaratibu wako ambao utaheshimiwa na kila mtu.

·         Kuepusha watu wadanganyifu wenye nia ya kutaka kunufaika na mali alizokuwa amechuma marehemu.

·         Wosia utamwezesha mtoa wosia kumweka mtu mwaminifu atakayesimamia mali zake baada ya yeye kufariki. Pia utamsaidia kuandaa walezi wa mtoto au watoto wake. Jaribu kufikiri mazingira ambayo baba mwenye mtoto au watoto kafariki na pengine mkewe nae kafariki au hawaishi wote na pengine mtoa wosia huyo ndugu zake wa kuzaliwa walimtangulia auhana kabisa, katika mazingira haya marehemu asipoandaa utaratibu mzuri wa kusimamia mirathi basi mali na watoto alioacha watakuwa katika mazingira magumu sana. Wosia tu ndio utakaookoa hilo lisitokee.

·         Wosia utasaidia kufahamu mali za marehemu na nani apewe nini na kipi.

·         Wosia pia utaweza kueleza utaratibu wa namna mtoa wosia atakavyozikwa. Hapa ataweza kuelezea azikweje, wapi na kwa gharama zipi kutoka wapi. Unaweza hata kuamua uchomwe moto badala ya kufukiwa na waliobakia watahakikisha hilo linatokea.

Je ni wakati gani sahihi kwa mtu kuandika wosia?

Lengo kuu la wosia ni kutaka mambo fulani fulani yafanyike pindi mtu atakapokuwa umefariki. Tusikariri ya kuwa ni lazima tuwe na vitu vingi ndio tuweze kuacha wosia kwani unaweza hata kuacha wosia kuutoa mwili wako pindi utakapofariki utumike katika kufanyia majaribio kwa wanafunzi wa udaktari katika chuo cha udaktari cha Muhimbili.

Ukizingatia vigezo vingine kama vile umri na kadhalika, mtu yeyote anaweza kuacha wosia. Hata kama unayo mali yenye thamani ndogo bado ni muhimu kwa wewe kuacha wosia kama nilivyoweza kuelezea hapo juu.

Unaweza ukaacha wosia kwenye mambo mengine ukiacha mali na vitu kama nilivyokwisha kudokeza hapo juu. Hivyo basi wosia unaweza kuachwa wakati wowote mtu anapokuwa hai na sio kusubiria mtu yupo mahututi ndio anatoa wosia.

Ni nani anapaswa kuandika wosia?

Mtu yeyote, awe mwanaume au mwanamke, kijana au mzee, mwenye mali nyingi au chache, mwenye umri wa miaka kumi na minane (18) na kuendelea akiwa na akili timamu wakati wa kuacha wosia basi anakidhi vigezo vya kuacha wosia.

Muhimu

Ni muhimu pia kufahamu ya kuwa wosia unakusudiwa kuwa na nguvu pale mtoa wosia huo atakapofariki. Watu wafahamu wosia ni tamko au karatasi tu kama aliyeandika wosia huo bado yupo hai. Itambulike pia mali zitakazopatikana baada ya wosia kuachwa zinaweza kuwa sehemu ya wosia bila hata kuorodheshwa katika wosia huo.

Lakini pia wosia wa mwanzo unaweza kufutwa au kubadilishwa na wosia mwingine. Hii inaweza kutokea hata kama kuna kipengele katika wosia kinachosema wosia huo hautabadilishwa kamwe. Jambo hili linaweza kufanywa na aliyetoa wosia kipindi cha uhai wake na sio mtu mwingine yeyote.

Mwisho naendelea kukusisitiza ndugu msomaji wangu usikose mwendelezo wa Makala hizi. Endelea kuutembelea ukurasa huu ili kujipatia makala mbali mbali kuhusiana na sheria. Kumbuka ‘learning is a process’ kwa maana ya kwamba kujifunza ni mchakato hivyo usichoke kujifunza. MAKALA HII NI KWA MUJIBU WA: https://ijuesheriatz.wordpress.com/2017/09/04/mambo-ya-kuzingatia-kabla-na-wakati-wa-kuandika-wosia/

No comments:

Post a Comment