RC BABU “MWENYE HAMU YA KUPIGA MWANAMKE AJE ANIPIGE MIMI”
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro,Nurdini Babu amesema hatawavumilia wanaume wanaoendeleza vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wanawake ikiwemo unyanyasaji pamoja na vipigo kwenye Mkoa huo.
Babu ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa tamasha la jinsia la kanda ya kaskazini lililoandaliwa na Mtandao wa Jinsia tanzania (TGNP),kwa kushirikiana na wadau wanaotetea haki za wanawake na usawa wa jinsia na wanaharakati binafsi linalofanyika kwa siku tatu kuanzia October 5-7, kwenye viwanja vya kwasakwasa Wilayani Same, huku akiwataka wanamke wanaofanyiwa vitendo hivyo vya ukatili wa vipigo, kufika ofisini kwake kuripoti kutokana na kuwa miongoni mwa watu wanaochukizwa na unyanyasaji wa kijinsia.
“Wanaume wanapaswa kujua kwamba mwanamke hatakiwi kupigwa bali anapaswa kuonyesha upendo kwani vipigo havina faida katika mahusino na endapo mwanaume anayepiga mwanamke ana hamu ya kupiga basi nipo tayari aje anipige mimi”Alisema Babu
Akizungumzia kuhusu tamasha hilo la jinsia, lilobebwa na mada kuu isemayo ‘Haki ya Uchumi, Rasilimali ziwanufaishe walioko pembezoni kwa maisha endelevu' amesema ni mada nzuri kama washiriki watayazingatia yatakayozungumzwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TGNP Mtandao, Gemma Akilimali, akaeleza mambo yanayochangia kukwamisha wanawake na makundi ya pembezoni kushiriki na kunufaika na maendeleo ya kiuchumi ni pamoja na mila potofu na kandamizi, ukatili wa kijinsia, kukosa fursa za kiuchumi kama kumiliki ardhi, kukosa mikopo wezeshi na kukosa taarifa sahihi.
Awali Mkurugezni wa TGNP,Liliani Liundi,akielezea kuhusu tamasha hilo alisema ni utaratibu wao wa kufanya hivyo kila mwaka na kubainisha kuwa kwa mara ya kwanza TGNP iliratibu Tamasha la kwanza la Jinsia ngazi ya taifa mwaka 1996 na mpaka sasa matamasha 14 yamefanyika na yameweza kuleta pamoja zaidi ya washiriki 25,000 kati yao asilimia 70 ni wanawake na asilimia 30 ni wanaume.
No comments:
Post a Comment