Thursday, November 17, 2022

Kilwa DC yatenga bajeti kuwezesha wasichana kupata taulo za kike shuleni

Na Deogratius Temba, Kilwa
HALMASHAURI ya Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi, imetenga bajeti kwa ajili ya kuwezesha wasichana wa shule za sekondari na msingi kupata taulo za kike ili waweze kushiriki kikamilifu masomo wanapokuwa kwenye hedhi.

Kwa mwaka wa fedha 2021/22 Halmashauri imefanikiwa kutenga na kutumia kiasi cha shilingi 2,385,000 na kununua taulo za kike ambazo zimewanufaisha wasichana wapatao 1,590, zikiwa ni mapato ya ndani na mchango wa wadau mbalimbali wa elimu.

Aidha, kwa mwaka wa fedha 2022/2023, Halmashauri imetenga kiasi cha sh. 4,500,000 kwaajili ya ununuzi wa taulo za kike kwa wasichana wa shule za sekondari na msingi, ambazo zinatarajia kuwanufaisha wasichana Zaidi ya 3,000.

Akizugumza wakati wa warsha ya kutathimini mradi wa uwezeshaji wasichana kupata elimu, unaotekelezwa na shirika la HakiElimu, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Bi. Farida Kikoleka, amesema kuwa Halmashauri hiyo inatambua umuhimu wa mtoto wa kike kupta elimu bora, ndio maana baada ya madiwani na wakuu wa idara kujengewa uwezo na HakiElimu, juu ya uandaaji wa Bajeti kwa mrengo wa Kijinsia, Halmashauri iliweka mkazo katika kuhakikisha mazingira ya kutoa elimu yanakuwa bora na salama kwa mtoto wa kike.

“mwaka jana wa fedha, tuliweza kutenga kiasi hicho cha bajeti baada ya HAKIELIMU kuwajengea uwezo waheshimiwa madiwani wetu pamoja na wataalamu kutoka idara mbalimbali. Pia Mimba zimepungua kutokana na elimu mbalimbali zinazotolewa kwa wazazi na wananachi kupitia mikutano ya vijiji na vitongoji. Kwa Mwaka 2020 kabla ya kujengewa uwezo na HAKIELIMU kulikuwa na mimba 42 na kupungua hadi mimba 16 mwaka 2021, “ alisema Mwenyekiti wa Halmashauri.
Aliongeza kwamba; utoaji wa taarifa za uwepo kwa mimba umekuwa mkubwa kutokana na mafunzo mbalimbali yanayotolewa na HAKIELIMU, marafiki wa elimu kupitia club za elimu au wasichana na wavulana vinara.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa marafiki wa Elimu Wilaya ya Kilwa, Godfrey Kamota, alisema kwamba, kupitia elimu inayotolewa na HAKIELIMU kupitia klabu za elimu na vinara wa elimu, inawapa uwezo wa watoto wenyewe kujieleza kwa kujiamini na ushirikiano wa jamii pia umeongezeka katika kuripoti matukio ya mimba.

“hawa vinara wa elimu wamekuwa chachu, wanafanya vizuri sana kwa kuwaelimisha wenzao, na hata wazazi juu ya vitendo vya Ukatili wa Kijinsia. Pia hawa wamejifunza kuzalisha sodo ambazo hawagawia wasichana wenzao wanaotoka katika kaya masikini ili waweze kushiriki kikamilifu kwenye za masomo” alisema Mwalimu Kamota.
Naye Kaimu Afisa elimu msingi, Abdallah Namakonja, alisema kwamba utoro umepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na ujenzi wa miundombinu rafiki hasa kwa wanafunzi wa kike, Upatikanaji wa chakula katika baadhi ya shule,ugawaji wa sodo kwa wanafunzi wa kike, pamoja na uwepo wa vyumba maalumu cha kujisitiri wakati wa hedhi.

No comments:

Post a Comment