RC Singida awafunda wanawake viongozi
Washiriki wa mafunzo kutoka Mikoa ya Simiyu na Singida, wakishangilia wakati wa Kumpokea Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego. |
Na Deogratius Koyanga, Singida
MKUU Mkoa wa Singida, Halima Dendego amewataka wanawake viongozi wanaotoka kwenye vikundi vya kijamii vya uzalishaji na wakulima kujitokeza kwenye kugombea uongozi katika ngazi mbalimbali ili kuchangia kuboresha bajeti na mipango ya serikali za mitaa iweze kuzingatia mahitaji ya kijinsia.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya uongozi na ushiriki wa wanawake kwenye nafasi mbalimbali za uongozi zikiwemo kamati na bodi mbalimbali ngazi za vijiji na kata, yaliyoandaliwa na shirika la Helvetas-Tanzania, chini ya mradi wa Wanawake katika uzalishaji wa ukijani, mjini Singida, Dendego amesema kwamba ni lazima wanawake wajitokeze kuomba nafasi za uongozi katika maeneo yote zaidi ya siasa ili waweze kulinda uoto wa asili, mazingira na kuboresha usalama wa chakula.
“ Tunapokuwa na wanawake kwenye nafasi za uongozi jamii
inakuwa salama, na sio kwamba wanaume wamefanya makosa au hawafanyi kazi
vizuri, wametuongoza siku nyingi tangu
uhuru na mambo mazuri yametokea, lakini
sasa wanahitaji tuwasaidie pia ili tuungane nao katika kujenga taifa hili na
kuleta maendeleo ambayo ni shirikishi.”alisema Dendego.
Kwa upande wake, Meneja Mradi wa Ukijani, kutoka Shirika la
Helvetas- Tanzania, Shoma Nangale, alisema kwamba mradi unalenga kujenga uelewa wa washiriki, kupata
ujuzi na stadi za kuwezesha kujiandaa na kuwania nafasi za maamuzi na uongozi
za kuteuliwa, kuchaguliwa ama kugombea ili waweze kusimamia miradi ya
maendeleo, na kuhakikisha masuala ya wanawake yanapata kipaumbele hasa katika sekta ya mazingira, usalama wa
chakula na ulinzi wa rasilimali asilia.
Mradi wa Ukijani unatekelezwa katika Halmashauri tatu za Mkoa
wa Singida ambazo ni Manyoni, Iramba na Ikungi na kwa Mkoa wa Simiyu ni Halmashauri
za Bariadi Mji, Bariadi DC na Meatu ambapo Zaidi ya wanawake 3,000 wananufaika
moja kwa moja na mradi huo.
No comments:
Post a Comment