WaterAid, TGNP na TAWASANET wajenga uwezo kwa wanawake Hanang’
Picha ya pamoja ya washiriki wa mafunzo ya wanawake viongozi wa Halmashauri za vijiji na kamati mbalimbali wilayani Hanang' Mkoa wa Manyara
Na Deogratius Koyanga, Manyara
Taasisi ya WaterAid Tanzania, Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), na Mtandao
wa Asasi za Kiraia zinazoshughulikia Maji, na Usafi wa Mazingira Tanzania (TAWASANET),
wamefanya mafunzo ya kujenga uwezo kwa wanawake viongozi kutoka vijiji nane (8)
katika Halmashauri ya Wilaya ya Hanang, Mkoani Manyara.
Mafunzo hayo yanalenga kujenga uwezo kwa viongozi wanawake wanaohudumu
kwenye Kamati za zahanati na Vituo vya afya, shule za msingi, Bodi za Sekondari
na kamati za Huduma za jamii kwenye Halmashauri za vijiji ili waweze kuweka
kipaumbele cha upatikanaji wa rasilimali ili kutatua changamoto za maji na
Usafi wa mazingira (WASH) katika maeneo yao.
WaterAid, TGNP na TAWASANET
wanatekeleza kampeni ya Afya ya Mwanamke Sasa ambayo inalenga kujenga
uwezo kwa wanawake na wanaume ili kuondoa changamoto za Kijinsia kwa kuzipa
kipaumbele wakati wa mipango na bajeti sambamba na kuondoa changamoto za
kijinsia ambazo zina wakabili zaidi wanawake.
Akiungungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkuu wa
Ushawishi, na Uchechemuzi wa sera kutoka
WaterAid, Christina Mhando, alisema kwamba suala la ukosefu wa maji ni suala la
wanawake, na ni suala la kijinsia, kwahiyo wanawake wanapaswa kulipa kipaumbele
katika majadiliano, au maamuzi ya kupanga vipaumbele vya bajeti. “ …. Hata yanapoibuka
magonjwa, waathirika wakubwa ni wanawake ndio maana tunashirikiana na wenzetu
hawa kujenga uelewa wa jamii jinsi
ambavyo masuala ya maji, afya na usafi wa mazingira unavyoweza kuathiri
wanawake, watoto wa kike na wazee
sambamba kurasimisha masuala ya kijinsia katika sera, bajeti na mipango
yote ya serikali za Mitaa” alisema Mhando.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Hanang, Theresia
Irafy, wakati wa kufungua mafunzo hayo alisema kwamba, mafunzo hayo ni muhimu
kwa wakati huu ukizingatia kwamba wanawake ndio wahitaji na watumiaji wakubwa wa huduma za maji na
endapo watapata uelewa na kusimamia vizuri rasilimali za umma sambamba na
miradi iliyojengwa italeta tija na kuwezesha kumtua mwanamke ndoo kichwani.
“Ninashukuru wadau hawa kwa kuja Hanang, tunahitaji sana
wadau wanaofanya kazi ya kujenga uelewa kwa jamii na kubadilisha mitazamo hasi
kuhusu masuala ya kijinsia, mtawezesha kubadilisha mitazamo ya jamii, lakini
pia wanawake wanatakiwa kuwa viongozi wazuri wa kusimamia miradi hii sambamba
na kuibua na kuweka vipaumbele vya
bajeti vyenye mtazamo wa kijinsia” alisema
Mafunzo hayo pia, yamefungwa na Mwenyekiti wa Halmashauri,
Bi. Rose Kamili ambaye alisema kwamba suala la maji na usafi wa mazingira ni suala la
kijinsia na linatakiwa kuwekewa mkazo kwa wanawake kulielewa na kulisimamia
wenyewe kwasababu ndio kundi
linaloathirika zaidi endapo huduma za maji na usafi wa mazingira zitakosekana.
“Sisi Halmashauri, tunaendelea kupambana kuhakikisha
tunatatua changamoto za ukosefu wa maji kwa baadhi ya maeneo, lakini tuendelee
kuwashukuru wadau wetu WaterAid kwa kuwezesha upatikanaji wa maji safi na
salama kwa baadhi ya vijiji hasa kwenye taasisi kama zahanati ambako wanawake
wanapata huduma zaidi. WaterAid mmekuwa msaada mkubwa kwa wanawake wa Hanang,
tunawashukuru sana…” alisema Kamili.
Mafunzo hayo yamewahusisha wanawake kutoka vijiji nane
ambavyo ni Gidamula, Gawidu, Muungano, Dajameda, Laghanga, Wareta, Getak na Bashang, ambapo washiriki wamekubaliana kuhakikisha wanahamasisha
wanawake kujitokeza kugombea uongozi katika serikali za Mitaa mwaka huu 2024
ili waweze kuwa kwenye nafasi za maamuzi hasa kuibua miradi ya maendeleo
itakayotatua changamoto za Maji, afya na usafi wa mazingira (WASH) katika
jamii.
Picha ya pamoja kati ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang' Mhe. Rose Kamili na wawezeshaji kutoka TGNP, TAWSANET na WaterAid, baada ya kufunga mafunzo ya wanawake viongozi mjini Hanang' |
No comments:
Post a Comment