Monday, July 29, 2024

MAELEKEZO 7 YA SERIKALI KUHUSU UKATILI WA KIJINSIA




Serikali imetoa maelekezo saba yanayaotakiwa kufaanyiwa kazi kwa dharura nchi nzima ili kuzuia vitendo vya Ukatili wa Kijinsia. 

 Maelekezo hayo yametolewa wakati wa  ziara ya Mawaziri wa kisekta kufuatilia uhai wa Kamati za Kutokomeza Ukatili wa Kijinsia na kwa Watoto, Mtaa kwa Mtaa (MTAKUWWA), iliyofanyika Manispaa ya Temeke, Jijini Dar es salaam, Julai 27, mwaka huu.

maelekezo hayo ni haya yaliyopo hapa chini:-

1. Kamati za MTAKUWWA ngazi zote zikae vikao vya dharura ndani ya wiki 2 kuanzia tarehe 1 Agosti, 2024 zijadili mikakati.

2. Wajumbe wa Kamati watangazwe wajulikane.

3. Viongozi pacha wachaguliwe Ili ikitokea  mwingiliano wa majukumu kazi za kamati ziendelee. 

4. Taarifa ya mipango na mikakati ya kamati imilikiwe na vikao vyote rasmi ngazi zote.

5. Kila tukio linaloripotiwa, Kamati ifanye kikao cha dharura cha tathmini ya kubaini wapi kulikuwa na mianya Ili wadhibiti.

6. Mikakati ya kuamsha uelewa wa watoto kuhusu kujilinda iandaliwe ikiwemo kwa kutumia michezo, hadith, sanaa, sinema nk.

7. Mijadala ya kijamii ifanyike kwa uratibu wa Dawati la Maendeleo ya Jamii.

Friday, July 19, 2024

RC Singida awafunda wanawake viongozi

 RC Singida awafunda wanawake viongozi

Washiriki wa mafunzo kutoka Mikoa ya Simiyu na Singida, wakishangilia wakati wa Kumpokea Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego. 


Na Deogratius Koyanga, Singida

 MKUU  Mkoa wa Singida, Halima Dendego amewataka wanawake viongozi wanaotoka kwenye vikundi vya kijamii vya uzalishaji na wakulima kujitokeza kwenye kugombea uongozi katika ngazi mbalimbali ili kuchangia kuboresha bajeti na mipango ya serikali za mitaa iweze kuzingatia mahitaji ya kijinsia.

 Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya uongozi na ushiriki wa wanawake kwenye nafasi mbalimbali za uongozi zikiwemo kamati na bodi mbalimbali ngazi za vijiji na kata, yaliyoandaliwa na shirika la Helvetas-Tanzania, chini ya mradi wa Wanawake katika uzalishaji wa ukijani, mjini Singida, Dendego amesema kwamba ni lazima wanawake wajitokeze kuomba nafasi za uongozi katika maeneo yote zaidi ya siasa ili waweze kulinda uoto wa asili, mazingira na kuboresha usalama wa chakula.

 







“ Tunapokuwa na wanawake kwenye nafasi za uongozi jamii inakuwa salama, na sio kwamba wanaume wamefanya makosa au hawafanyi kazi vizuri,  wametuongoza siku nyingi tangu uhuru na mambo mazuri yametokea,  lakini sasa wanahitaji tuwasaidie pia ili  tuungane nao katika kujenga taifa hili na kuleta maendeleo ambayo ni shirikishi.”alisema Dendego.

 

Kwa upande wake, Meneja Mradi wa Ukijani, kutoka Shirika la Helvetas- Tanzania, Shoma Nangale, alisema kwamba   mradi unalenga kujenga uelewa wa washiriki, kupata ujuzi na stadi za kuwezesha kujiandaa na kuwania nafasi za maamuzi na uongozi za kuteuliwa, kuchaguliwa ama kugombea ili waweze kusimamia miradi ya maendeleo, na kuhakikisha masuala ya wanawake yanapata kipaumbele  hasa katika sekta ya mazingira, usalama wa chakula na ulinzi wa rasilimali asilia.

 

Mradi wa Ukijani  unatekelezwa katika Halmashauri tatu za Mkoa wa Singida ambazo ni Manyoni, Iramba na Ikungi na kwa Mkoa wa Simiyu ni Halmashauri za Bariadi Mji, Bariadi DC na Meatu ambapo Zaidi ya wanawake 3,000 wananufaika moja kwa moja na mradi huo. 

Monday, July 1, 2024

Unyago, jando vyachangia utoro shuleni

 Unyago, jando vyachangia utoro shuleni



Na Deogratius Koyanga, Nachingwea

Vitendo vya kupeleka watoto wa kiume na kike kwenye shughuli za jando na unyago vinavyofanywa  na jamii ya Mkoa wa Lindi na viunga vyake vinachangia kwa kiasi kikubwa utoro wa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

Hayo yamebainishwa katika mdahalo wa jamii uliowashirikisha wananchi kutoka katika vikundi vya kijamii, wazee wa mila, mangariba na viongozi wa dini katika kata ya Mtuwa, halmashauri ya wilaya ya Nachingwea, mkoani Lindi.

Imebainishwa kwamba, vitendo hivyo vinatokana na jamii kutokufuata ratiba ya kufunga na kufungua shule na kuwaingiza watoto wadogo wa shule za msingi kwenye shughuli za kimila za jando na unyago wakati shule zikiendelea na ratiba zake na kupelekea mamia ya wanafunzi kukosa masomo hadi zitakapofanyika sherehe za kuwatoa ndani,

Mdahalo huo, unawashirikisha wananchi  na wadau mbalimbali kama sehemu ya kutekeleza mradi wa uwezeshaji wanawake kushiriki kwenye nafasi za uongozi  na maamuzi na haki ya uchumi, unaotekelezwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa ufadhili wa Unwomen Tanzania,

Akizungumza wakati wa mjadala huo, mchungaji wa kanisa la wadiventista wasabato, kata ya Mtuwa,Samwel Mang’ati, alisema kwamba wao kama viongozi wa dini wanashauri utaratibu wa kuheshimu ratiba za watoto wa shule ufuatwe ili watoto wote wapate haki ya kupata elimu sambamba na maadili lakini akaonya kuhusu mila hizo kuzingatia maadili na heshima kwa kutumia lugha nzuri zenye staha, kuepuka matusi, kuepuka kufundisha vitu vilivyo nje ya umri wa watoto hao ili kukuza jamii yenye maadili mazuri.

“sisi kama viongozi wa dini tunashauri kuwepo kwa watu maalum, hawa wanaoitwa “warombo” wawe na elimu, wawe ni watu wazima,  walioandaliwa na wawe na elimu maalum ya kufanya kazi hiyo” alisema MchungajI Samwel

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kigango cha Kanisa Katoliki cha Mtuha,Emelius Mkwawa, Alisema kwamba anashauri, utaratibu wa kundesha unyago na jando, uzingatie ratiba za shule ili kutokuwakosesha watoto wa kike na kiume haki ya kupata elimu.

“nashauri, mara tu shule zinapofungwa, hizi shughuli za kimila zianzie hapo hapo, hiyo wiki ya kwanza, shule zinapofunguliwa tuhakikishe hakuna mtoto anabaki kwenye jando au unyago. Wote wawe huru waende shule”alisema na kuongeza:-

“Ninashauri wazazi waache hii tabia kuingia gharama kubwa na kutumia fedha nyingi kwenye sherehe za jando na unyago  lakini kushindwa kuwanunulia watoto hao sare za shule na vifaa vya shule mara shule zinapofunguliwa, unakuta mzazi ananunua nguo za gharama kubwa kwaajili ya shughuli ya unyago au jando, lakini sare za shule hakuna,viatu”

Alisema kwamba, ni vizuri wazazi kuwekeza kwenye elimu, na wanaotoa zawadi kwa watoto wanunue madaftari , kalamu,mabegi ya shule, sare za shule ili kuwafanya watoto walioingia jando kuipenda elimu.

Kwa upande wake Ngariba wa muda mrefu mzee Thomas Ndimbo,  alismea kwamba, taratibu za kutoa vibali vya kuendesha  jando na unyago zinajieleza wazi kwamba, watoto waende jando na unyago wakiwa likizo na wasiwepo kwenye shughuli hizo wakati shule zimefunguliwa na huu ni utaratibu wa mkoa mzima wa Lindi, lakini jamii imekiuka kwa kupanga shughuli hizo wakati mwingine.

“Labda sisi mangariba tukutane, tufanye kikao pamoja na viongozi wa serikali za vijiji vyetu sambamba na jamii ili tukubaliane tena. Asiwepo ngariba anayekubali kupeleka watoto uwanjani, wakati wa shule au wengine akiwa sshuleni” alisema Ndimbo.