Monday, October 2, 2023

TGNP yawezesha viongozi wanawake na wenza wao kusimulia hadhithi za mafanikio

 TGNP yawezesha viongozi wanawake na wenza wao kusimulia hadhithi za mafanikio

Na Mwandishi Wetu

Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa kushirikiana na Aghakan Foundation (AKF-T), wameendesha warsha ya Masimulizi ya hadithi za mafanikio kwa viongozi wanawake na wenza wao ili kujadili changamoto wanazokumbana nazo katika kutekeleza majukumu yao ya kiuongozi.  

Picha ya pamoja ya viongozi wanawake na wenza wao baada ya warsha iliyofanyika katika Ukumbi wa Riverside, mjini Kondoa


Warsha hiyo iliwahusisha Madiwani wanawake na wenza wao, viongozi wa Kata, vijiji na Vitongoji katika Halmashauri ya wilaya ya Kondoa, Mkoani Dodoma.

Akizungumza Mwezeshaji kutoka TGNP, Deogratius Temba, alisema kwamba Mradi huo unalenga kujenga na kuimarisha mahusiano kati ya wenza wa viongozi wenyewe lakini  pia kuangalia changamoto ambazo wanawake viongozi wanapitia hadi kufikia maendeleo.


“Kila kiongozi aliyepo hapa anayo mafanikio, mafanikio haya yamekuja kwa kupitia changamoto pia, kufikia hali nzuri kuna watu wamekuwezesha kufika hapo, labda ni Mwenza wako, jirani, mwalimu, kiongozi wa Chama chako, mwajiri, kiongozi wa dini au yeyote. Lakini pia hadithi yako itajenga uelewa kwa wengine na kuwatia moyo…’ alisema Temba


Washiriki wakiwa tayari kwa kusikiliza masimulizi ya hadithi za safari ya uongozi kutoka kwa viongozi wanawake


Ameongeza kwamba, kupitia masimulizi ya hadithi, madiwani watawapa moyo viongozi wanawake wanaotoka ngazi za chini vitongoji na vijiji ili wasonge mbele zaidi kwani huko ndiko wanakumbana na vikwazo vikubwa vya mila, desturi, mitazamo hasi, lakini pia majukumu ya kazi ambazo hazina malipo (unpaid care work)  yanawaelemea sana wanawake sana wanawake viongozi na kupelekea kushindwa kutekeleza vizuri majukumu ya kiuongozi.

Akitoa hadithi ya kukwama na kufanikiwa katika safari ya uongozi, Fatuma Iddi Issa Diwani wa Viti maalum, Halmashauri ya Kondoa Mji, alisema kwamba, pamoja na kuanza mapema safari ya kisiasa akiwa na umri wa miaka 20, hakufanikiwa  kufikia lengo lake kwa wakati kutokana na kukwamishwa na watu wa karibu.

Mhe. Fatma Said Idd, Diwani wa Viti Maalum, Kondoa Mji


“Nilitakiwa kuwa mbali sana, kama nisingekwamishwa, leo nilitakiwa kuwa Mbunge na sio Diwani tena, lakini nilipoteza mwelekeo  hapo katikati, sijakata tamaa, nasonga mbele kwa ujasiri “ alisema Fatuma.

Kupitia mjadala na masimulizi ya hadithi, wenza wa viongozi wanawake nao walisimulia safari za uongozi za wenza wao na jinsi ambavyo wamewawezesha kutimiza majukumu ya kiuongozi kwa kuwasaidia baadhi ya kazi za nyumbani kama kulea watoto, kuandaa chakula, kuvua, kusafisha shamba na kutunza mifugo.

Mwezeshaji kutoka TGNP, Deogratius Temba


Katika simulizi za safari ya uongozi kwa viongozi wanawake waliohudhuria, wenza wao walitoa ushuhuda jinsi ambavyo walichangia wake zao kufikia hatua hiyo, ikiwepo, kuwashawishi, kuwawezesha kifedha, rasilimali nyigine lakini pia kuwapa muda wa kutekeleza majukumu. 

No comments:

Post a Comment