Sunday, October 22, 2023

TGNP kushiriki wiki ya CSO Arusha, kuonesha ubunifu wa wasichana wa DIT

 

Na Mwandishi Wetu, Arusha

Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) inashiriki maadhimisho ya wiki ya Asasi za Kiraia (CSO) inayofanyika Jijini Arusha kwa kutoa elimu juu ya umuhimu ya wajamii kushiriki kwenye ubunifu wa kisayansi na Kiteknolojia kwa kuzingatia usawa wa Kijinsia kwa maendeleo Endelevu.

Mkutano wa wahandishi wa Habari na Kamati ya Maandalizi ya Wiki ya CSOs uliofanyika leo jijini Arusha

Maadhimisho ya Wiki ya CSOs yanayotarajiwa kuanza kesho Oktoba 23, 2023 Jijini Arusha yatahusisha asasi za kiraia Zaidi ya 500, kutoka  mikoa yote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na nchi jirani, huku kukiwa na mada mbalimbali ambapo mada kuu inalenga ushiriki wa asasi za kiraia katika Teknolojia katika kufanikisha shughuli zake za kitoa huduma kwa jamii nchini,  na Zaidi kutafakari mafanikio ya nyuma, ya sasa na ya baadaye  sambamba na changamoto zake.

Akizungumza Mwakilishi wa TGNP katika Mkutano na wandishi wa Habari leo uliowahusisha wakurugenzi wa mashirika mbalimbali na kamati ya kitaifa ya uandaaji wa maadhimisho hayo, Deogratius Temba, alisema kwamba, pamoja na TGNP kushiriki kwenye shughuli zote, kwa kushirikiana na mashirika mengine, pia wataendesha warsha na majadiliano ambayo yataangazia Ubunifu na uvumbuzi  wa kiteknolojia kama chachu ya usawa wa Kijinsia.

Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Lilian Liundi na  Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) Prof. Preksedis Ndomba, katika hafla ya makubaliano ya kushirikiana kukifanya chuo hicho kuwa Kitovu cha Jinsia, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wasichana wanapewa kipaumbele katika ubunivu katika Teknolojia (Picha na maktaba)


Temba ameeleza kwamba, mada hiyo itawahusisha wadau mbalimbali, mashirika, wanazuoni na wataalamu wanawake  na wasichana walio kwenye Ubunifu na uvumbuzi wa kiteknolojia katika kuondoa changanmoto zinazoikumba jamii hasa wanawake na watoto.

“Tutakuwa na wanafunzi wasichana kutoka DIT ambao ni wavumbuzi wa kiteknolojia, wanaolenga kuondoa changamoto za kijamii katika taifa letu. TGNP tumejenga uwezo kwa jamii na taasisi mbalimbali kubomoa mifumo kandamizi na mitazamo hasi juu ya uwezo na ushiriki wa wanawake hasa wasichana katika Sayansi, Teknolojia, na Hisabati, sasa wapo wasichana wanaofanya vizuri kwenye ngazi ya vyuo vikuu kama Taasisi ya Teknolojia Dar es salaam (DIT), wamefanya vizuri sana,” alisema Temba na kuongeza:

“Ukiangalia kwa hapa tulipofikia kama nchi, tumepiga hatua, vifaa vipo,lakini bado kuna pengo la usawa wa kijinsia na ushiriki au ujumishwaji wa makundi yote, tunachofanya kwa kushirikiana na Taasisi mbalimbali ni kubadilisha mitazamo hasi, lakini pia kushaiwshi serikali kutenga bajeti ya kutosha kwenye TEHAMA hasa mashuleni, na kuondoa au kuunguza kodi kwa vifaa hivyo ili watoto waweze kujifunza na kuonesha ubunifu wao” alisema Temba.        

Aidha, amesema kwamba, Nchi kama Tanzania zinaweza kufaidika sana na kuendeleza sera na mipango inayowezesha ushiriki wa wanawake katika sekta ya teknolojia na kuhakikisha kwamba teknolojia inatumika kwa njia inayolinda usawa wa kijinsia. Hii inaweza kuchangia katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi na kuboresha hali ya maisha kwa wanawake na wanaume kwa usawa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi  ya wiki ya CSO Niensia Mahenge alisema kwamba, Teknolojia inatoa  fursa kwa wasichana na wanawake kupata elimu na kukuza ujuzi. Majukwaa ya kujifunza mtandaoni, programu za elimu, na rasilimali za kidijitali huwezesha kujifunza kwa umbali na kujifunza bila shinikizo la muda, kupunguza vikwazo vya kuingia.

“Teknolojia inaweza kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wanawake, hasa katika maeneo yasiyopewa kipaumbele. Huduma za tiba kwa njia ya mtandao na programu za afya za simu hutoa zana kwa wanawake kudhibiti afya na ustawi wao, ikiwa ni pamoja na huduma za ujauzito, uzazi wa mpango, na usaidizi wa changamoto za kiafya” alisema Mahenge.

Hata hivyo, wadau wameshauri kwamba  ni muhimu kuzingatia kuwa teknolojia na uvumbuzi pia yanaweza kuwa na athari hasi kwa usawa wa kijinsia ikiwa haitazingatia changamoto za kijinsia na inaweza kuongeza pengo la kidijitali. Kwa mfano, wanawake wengi katika nchi za dunia ya tatu wanaweza kukosa upatikanaji wa vifaa vya teknolojia au elimu ya kutosha ya kidijitali. Kwa hiyo, juhudi zinahitajika ili kuhakikisha kwamba teknolojia na uvumbuzi unawafikia wanawake na wanaume sawa na kuchangia katika kuboresha usawa wa kijinsia.

 

 

No comments:

Post a Comment