Wednesday, August 30, 2023

TGNP yafanya zoezi la SAM kwa mtazamo wa Kijinsia sekta ya Afya

 

·        *  Watumishi wa afya wanaoishi kwenye wodi ya wazazi kuhamishwa

·       *  Changamoto ya maji kwenye zahanti yaibuliwa

·         *Uongozi wa Vijiji kusimamia vichomea taka zahanati

Na Deogratius Temba, Kondoa

WATUMISHI  wa zahanati ya Kijiji cha Mafai,Kata ya Haubi, Wilaya ya Kondoa  wanaoishi katika wodi zilizojengwa kwa ajili ya huduma ya mama na mtoto, wametakiwa kutafuta nyumba za kuishi ili kupisha wodi hizo kutumika kwa lengo husika.

Akizungumza wakati wa kujibu hoja zilizoibuliwa kwenye zoezi la Uwajibikaji na Ufuatiliaji wa Jamii (SAM) kwa mtazamo wa Kijinsia, lililoendeshwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP),  katika sekta ya afya, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa,Mashauri Visenti, alisema kwamba watumishi wa zahanti ya Mafai, ambao wanaishi kwenye wodi za Mama na Mtoto wanapaswa kuhamia kwenye nyumba za kupanga kijijini ili kupisha huduma ya mama na mtoto kuendelea katika vyumba hivyo kwa ufanisi zaidi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha usalama wa vifaa vilivyopo kwenye zahanati hiyo.

Timu ya SAM ikiwa nje ya Jengo la zahanati ya Mafai, ilipotembelea kuona ubora wa utoaji wa huduma za afya

“kwa sababu sasa tumeshatimiza mwaka mmoja tangu kuanza kazi kwa zahanati hii, tunashauri, wapishe zile wodi ili kuboresha Zaidi huduma ya mama na mtoto katika zahanati yetu ile..” alisema Mashauri.

Timu ya SAM ikiendelea na uchambuzi na mapitio ya nyaraka mbalimbali za Halmashauri ya Kondoa DC kwa muda wa siku tatu


Awali akizungumzia jambo hilo, Katibu wa Afya wilaya ya Kondoa, alisema kwamba, awali watumishi hao walikuwa wapya, na ndio walipelekwa kwa ajili ya kuanzisha zahanati hiyo mpya, wakaomba kuishi kwenye vyumba hivyo vya zahanati ili waweze kuzoea mazingira na kutafuta vyumba katika kijiji hicho.

“sasa wamezoea, mazingira, na wameshakaa Zaidi ya mwaka, awali tuliwaruhusu kwa sababu ndio walikuwa wanaenda kuanza kazi katika kijiji kile, tutawa andikia barua ya kuwataka kutafuta nyumba kijijini ili waweze kupisha huduma ziendelee pale. Pia sio salama kiafya kwa wahudumu kuishi ndani ya Hospitali au vyumba vya matibabu.” Alisema Mbaga.

Awali akiwasilisha matokeo ya SAM kwa wadau wa Halmashauri pamoja na Menejimenti, Mwezeshaji wa SAM kutoka Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) Deogratius Temba alisema kwamba, pamoja na changamoto ambazo zilioonekana za kibajeti, na utoaji wa huduma za afya kwa kuzingatia usawa wa Kijinsia, Halmashauri ya wilaya ya Kondoa imejitahidi kutenga bajeti ya afya kwa mrengo wa kijinsia ikiwa ni pamoja na kupata hati safi kwa mujibu wa ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2021/2022.

Mwezeshaji Deogratius Temba, kutoka TGNP akitoa mafunzo mafupi maana ya SAM kwa mrengo wa Kijinsia, umuhimu wake  na maeneo Muhimu ya Kijinsia ya kufuatilia

Temba aliishauri halmasahuri kuweka uzito na umuhimu katika maeneo ambapo kuna vifaa tiba vya mama na mtoto vitumike  na kutunzwa. Mfano, zahanati ya Mafai, wahudumu wanatumia vyumba vya wodi ya mama na mtoto kwa malazi, chumba kinachotumika kwa sasa kama wodi na chumba cha kujifungulia (labor Room) kipo eneo la wazi  karibu na ukumbi wa OPD. Hakuna usiri wala faragha Kwa mama anayejifungua.

“ ..Kutokana na kutokutumika kwa wadi ya mama na mtoto iliyonjengwa kwa kazi hiyo, uhifadhi  na utunzaji wa vifaa tiba na mashine za kisasa zilizonunuliwa kwa ajili  mama na mtoto unakuwa dhaifu.  Mfano mashine nzuri za Oxygen, kuvuta uchafu kwenye pua za watoto wachanga (suction machine) na sterilizer ya kisasa vilikutwa chini kwenye sakafu” alisema temba na Kuongeza:

“ Hatukuona bajeti  kwa ajili ya Zahanati ili kuhakikisha zinapata maji safi na salama kwa ajii ya mahitaji ya kina mama wanaojifungua. Hata tulipoitembelea Zahanati ya Mafai kisima kilichopo jirani hakijaanza kutumika, lakini pia kina mama wanaojifungulia zahanati hawana huduma ya maji….” Alisema Temba

Aidha timu ya SAM kwa mrengo wa Kijinsia iliishauri Halmashauri kutenga  bajeti kwa ajili ya nyumba za watumishi kwani kuna maboma ya nyumba za watumishi wa kada ya afya ambazo zimejengwa na jamii kwa nguvu zao, lakini zipo hatua ya lenta muda mrefu. Mwaka wa fedha 2021/2022 hakuna bajeti iliyotengwa kwa ajili ya nyumba za watumishi wa afya huko vijijini, Mfano jengo  nyumba ya watumishi Zahanati ya Mafai ambalo limejengwa na wananchi hadi hatua ya lenta tangu mwaka 2014, sasa limeanza kuharibika.

Zoezi la SAM na mafunzo yake liliendeshwa kwa njia shirikishi za kiraghibishi ili kujenga uelewa wa pamoja

Naye Diwani wa Kata ya Haubi,Paulo Irovya,  ambapo zahanati hiyo, ipo alisema kwamba ataitisha Kikao cha Kamati ya Maendeleo ya Kata (WDC) ili kuweka mikakati ya kukabiliana na changamoto zilizo onekana katika zahanati hiyo, hasa zilizo ndani ya uwezo wao badala ya kusubiria bajeti ya Halmashauri ambayo wakati mwingine haitoshi kutatua changamoto zote za jamii.

Katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mafai, Mursal Juma Doiyya, aliahidi  kuitisha mkutano wa kijiji na kuwahamasisha wanakijiji kujenga kichomea taka katika zahanati hiyo, sambamba na kuendeleza ujenzi wa nyumba ya wahudumu ambayo imeishia hatua ya lenta ambayo inauwezo wa kutumika na familia mbili. 

Vifaa vya Kisasa kwa ajili ya Huduma ya Mama na Mtoto vilivyowekwa katika zahanati hiyo, zikiwepo Mashine ya kuvuta uchafu puani kwa watoto waliozaliwa na matatizo na mashine ya oxygen zikiwa chini sakafuni, ndani ya chumba cha kujifungulia



Mashine maalum ya kuchemshia vifaa tiba, ikiwa chini sakafuni kwenye chumba cha kujifungulia



No comments:

Post a Comment