Na Deogratius Temba, MOROGORO
UMOJA wa Klabu za Waandishi wa habari Tanzania (UTPC),umejenga uwezo na kuunda timu ya Waandishi wa Habari vinara wa Jinsia (Gender Champions) watakaokuwa chachu ya kuongeza dhana ya uandishi wa Habari za Kijinsia nchini.
Mkurugenzi Mtendaji, UTPC, Kenneth Simbaya, akifungua mafunzo hayo mjini Morogoro |
Mafunzo kwa waandishi wa Habari Vinara wa Usawa wa Kijinsia yamefanyika kwa muda wa siku mbili kujenga uwezo Zaidi kwa washiriki namna ya kuandika habari zenye mrengo wa Kijinsia katika sekta mbalimbali kwa ufadhili wa Ubalozi wa Sweden.
Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa (UTPC) Kenneth Simbaya,akifungua mafunzo hayo amesema lengo ni kuwajengea uwezo waandishi wa habari, namna ya kuripoti habari za jinsia, pamoja na kujifunza namna ya kuandika au kuibua habari za kijinsia ambazo zimekuwa haziandikwi mara nyingi ili kuchoechea maendeleo endelevu kwa jamii yote kwa ujumla.
Afisa Programme, Kutoka UTPC, Bi. Hilda Kileo akizungumza |
"Hakuna Maendeleo bila usawa wa kijinsia, Nchi yetu inatekeleza malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) tunataka kuona wanahabari wakielimisha jamii itambue haya malengo vizuri, jamii itambue namna ya kuhusisha maendeleo na SDGs" alisema Simbaya.
Aidha, amewataka pia waandishi wa habari kujikita katika kuandika habari za jinsia (Specialize), pamoja na kuandika habari kina zaidi na zenye kuleta uwajibikaji, na kubadilisha mitazamo hasi ndani ya jamii juu ya usawa wa kijinsia.
Mwakilishi wa Ubalozi wa Sweden Nchini Tanzania, Bi. Nasieku Kisambu akizungumza |
Naye Ofisa Program kutoka UTPC Hilda Kileo, amesema mafunzo hayo pia yamelenga kufanikisha malengo endelevu ya Maendeleo (SDGs) lengo namba 5 Usawa wa Kijinsia na kuyahusisha na Mikakati na mipango ya ndani ya nchi kama dira ya maendeleo ya Taifa ya Miaka mitano (Vision 2025), Mpango wa maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (FYDP), Sera ya Taifa ya Jinsia na Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili wa Kijinsia kwa Wanawake na watoto (MTAKUWWA).
“… kama ilivyoainishwa katika lengo namba 5 la SDGs tunataka kuona wanahabari wa habari za Kijinsia wakiwa na uwezo wa kuunganisha utekelezaji wa mipango ya ndani ya nchi, huduma za Jamii na usawa wa Kijinsia. Lakini pia kutoa elimu kwa jamii ili itambue kuwa nchi yetu inatekelezaje SDGs zote 17 kwa mrengo wa kijinsia” alisema Hilda
Washiriki wa Mafunzo wakifuatilia mada |
Mwakilishi kutoka Ubalozi wa Sweden Tanzania Nasieku Kisambu, amesema wamefadhili mafunzo hayo wakiamini kwamba vyombo vya habari zinauwezo mkubwa wa kuleta mabadiliko ndani ya jamii kuhusu masuala mazima ya usawa wa kijinsia, na kuahidi kuendelea kushirikiana na UTPC na wanahabari kuhakikisha usawa wa kijinsia unazingatiwa kaatika Nyanja zote.
Nao baadhi ya waandishi wa habari wamesema mafunzo hayo yamewaongezea uwezo katika kuandika habari za usawa wa kijinsia.
Mwezeshaji wa Mafunzo, Mtaalamu wa Masuala ya Usawa wa Kijinsia, Deogratius Temba, akitoa mada |
Waandishi wa habari vinara wa Jinsia wataendelea kuwa chachu ya mabadiliko katika uandishi wa habari za kijinsia, wakilenga kutoa elimu kwa jamii kubadili mitazamo hasa mila na desturi zinazokuza mfumo kandamizi, kusukuma mabadiliko ya kisheria na kisera ili kuweka mazingira salama kwa wanawake, watoto na makundi mengine yaliyoko pembezoni
No comments:
Post a Comment