Friday, May 19, 2023

Wadau wakutana na TAMISEMI , watoa maoni juu ya mikopo ya 10%

Wadau wakutana na TAMISEMI kujadili mfumo wa utoaji mikopo ya asilimia 10 Na Deogratius Temba, Dodoma KIKOSI kazi cha Asasi za Kiraia (Azaki), wamekutana na Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuwasilisha maoni na mapendekezo yao kwenye mfumo wa utoaji wa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya Halmashauri kwa Wanawake, Vijana na watu wenye ulemavu.
Kikosi kazi hicho chini ya uenyekiti wa UNA-Tanzania, kimewakilishwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), ANSAF, WAjibu- Institute of Public Accountability, Policy forum na IDPC, na kuwasilisha maoni ya Azaki juu ya muundo gani utakaowezesha makundi lengwa kunufaika na fedha hizo. Awali akiwasilisha, Mkuu wa Programu kutoka UNA-Tanzania, Lucas Kifyasi alisema kwamba kikosi kazi kimefika Tamisemi kwa lengo la kuwasilisha maoni na mapendekezo ya haraka mara baada ya kusitishwa kwa muda mfumo wa sasa unaotumika kutoa mikopo kwa makundi maalum ili kusubiria muundo na mfumo mpya. Pamoja na mengine, suala kutumia benki kupitisha mikopo hiyo, ambapo wadau walipendekeza kuwepo na Banki ya serikali za Mitaa ambayo itaweza kulenga kuwafikia walengwa kiurahisi, kuliko kuzitumia benki za kibiashara ambazo makundi maalum yamekuwa yakipata changamoto kufikia huduma za kibenki. Kaimu Mkurugenzi Utawala Bora na Maendeleo ya jamii kutoka TAMISEMI , Stephen Motambi, alishukuru Azaki, kwa kuona umuhimu wa kuwasiliana na wizara kabla mchakato haujafika mbali. Aidha, aliwashauri wadau kuandaa wasilisho litakalo onesha muundo ambao wadau wa Azaki wanapendekeza na kuwasilisha Tamisemi ili mikopo hiyo iweze kuwanufaisha walengwa wengi na kuhakikisha changamoto zilizojitokeza huko nyuma hazitajirudia.

No comments:

Post a Comment