Wanafunzi wa shule ya sekondari ya Zirai, Wilayani Muheza mkoani Tanga, wakiwa na Mwandishi wa Makala hii wakati alipotembelea shuleni hapo.
Na deogratius temba, Muheza
Mwongozo
wa serikali juu ya Maji, Afya na Usafi wa mazingira wa mwaka 2016, unatoa maelekezo
kwamba wadau katika ngazi mbalimbali
watahusika kusimamia utekelezaji wake ikiwepo kuhakikisha kuwa ujenzi wa
miundombinu ya hedhi salama katika shule unakuwa na tija. Serikali kupitia
wmongozo huo ulioandaliwa na Wizara ya elimu, sayansi na Mafunzo ya Ufundi, inazotaka
kila Halmashauri kusimamia utekelezaji wa mwongozo huo ikiwa ni pamoja na
kutenga bajeti kwa kila mwaka wa fedha kwenye mapato yake ya ndani ili kutatua
changamoto zinazotokana na kukosekana kwa huduma nzuri kwenye eneo la Maji,
afya na usafi wa mazingira (SWASH) na
kusababisha kiwago cha elimu kushuka.
Kama
sehemu ya utekelezaji wa mwongozo huu wa serikali, Mtandao wa Jinsia (TGNP),
kwa kushirikiana na Shirika la ONGAWA na Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, wanatekeleza
mradi wa Maji, afya na usafi wa mazingira (WASH) katika ngazi ya kaya na
shuleni, ambapo suala la Hedhi salama shuleni linapewa msukumo wa kipekee ili
kuwezesha wasichana kushiriki kikamilifu masomo shuleni wanapokuwa kwenye hedhi.
Utafiti wa awali kuhusu hali ya SWASH
uliofaywa na serikali mwaka (2009) katika shule za msingi na sekondari
iliyofanyika katika wilaya 16 Tanzania umeoneshasha kwamba hali ya Maji, Usafi
wa mazingira katika shule ilikuwa chini. Ni asilimia 11 ya shule zilizofayiwa
utafiti ndizo zilikuwa zimefikia hitaji la kisera la uwiano wa matundu ya vyoo
wa Tundu moja kwa wasichana 20, na tundu moja kwa wavulana 25. Zaidi ya
asilimia 20 ya shule zilikuwa na uwiano wa wanafunzi 100 na zaidi kwa tundu
moja la choo. Wakati utafiti ulionesha kuwa asilimia 6 ya shule zilikuwa hazina
kabisa matundu ya vyoo.
Picha
halisi inaonesha kuwa utafiti huu wa Maji, Afya na usafi wa mazingira shuleni
(SWASH), shule nyingi hazina miundombinu ya kutosha ya usambazaji wa maji,
miundombinu hafifu ya usafi wa mazingira, hakuna kabisa mfumo wa kunawa mikono,
baadhi ya vifaa vya usafi ni vibovu au
vimevunjwa.
Vifaa
vya Maji, afya na usafi mazingira shuleni (SWASH) kama matundu ya vyoo, kwa
shule nyingi hayalengi mahitaji ya wasichana wanapokuwa kwenye hedhi, watoto
wadogo na wanafunzi wenye ulemavu, maeneo mengi yana mahudhurio hafifu kwa
wasichana wanapokuwa kwenye hedhi kutokana na kukosekana kwa vifaa vya hedhi salama
na usiri wa kujisitiri wakiwa kwenye hedhi.
Hivi
karibuni, wasichana wa shule ya sekondari ya Zirai iliyoko katika Tarafa ya Amani
-wilaya ya Muheza, walitoa sauti zao kushukuru wadau kwa kusaidia upatikanaji
wa chumba maalum cha kujisitiri wanapokuwa kwenye hedhi, upatikanaji wa pedi za
bure shuleni, maji safi na salama chooni, elimu na malezi bora ya makuzi
yanayotolewa na waalimu wa kike shuleni hapo. Wanafunzi wamesema kwamba, sasa
wanawea kusoma bila tatizo kutokana na kupata huduma za hedhi salama shuleni na wengi waliokuwa hawafiki shuleni
wakati wa hedhi.
Kwa upande
wake Afisa Elimu Kata ya Zirai, Mwalimu Mohamed Mmole, anazungumzia mafanikio
ambayo shule yake ya kata ya Zirai imeyapata kutokana na uwepo wa vyumba maalum
vya kujisitiri kwa wasichana wakati wa hedhi pamoja na upatikanaji wa pedi
shuleni. Anasema kwamba uongozi wa shule ulikubaliana kuwa suala la hedhi
salama lipewe kipaumbele. Pamoja na
changamoto ya ukosefu wa rasilimali fedha za kununua pedi na vifaa vingine,
walikubaliana kutumia fedha kidogo za ruzuku ya elimu kwa wanafunzi
(capitation) inayotolewa kwaajili ya afya shuleni na kununua vifaa hivyo.
“…….
inawezekana kabisa kusimamia vizuri utekelezaji wa mwongozo huu wa serikali wa
Afya, Maji na usafi wa mazingira wa mwaka 2016, wadau wametujengea matundu ya
vyoo na chumba maalum cha kujisitiri, sisi hapa shuleni tumeamua kuunga mkono
juhudi hizi za wadau kwa kuhakikisha hizi pedi hazikosekani, dawa za kutuliza
maumivu kwa kwaajili ya wasichana nazo hazikosekani” anasema Mwalimu Mmole.
Mwalimu
Mmole anasema kwamba, pamoja na changamoto ya miundombinu ya usafiri katika
kata, ukosefu wa maduka karibu na wananchi, uwepo wa huduma muhimu za kiafya
kwa wanafunzi kunaongeza ushiriki wa wanafunzi hasa wasichana kwenye masomo,
ikiwepo ongezeko la mahudhurio darasani.
Mwalimu
mlezi wa wasichana shule ya sekondari Zirai, Rehema Matuga, anaeleza: “ Sisi kama waalimu tunashukuru sana, tunapoona
wasichana wana utulivu hapa shuleni, awali kabla ya miradi hii ya hedhi salama haijaanzishwa hapa kwetu, suala
la hedhi kwa wasichana hatukulipa kipaumbele, watoto wa kike walikuwa
wakijiamulia kutokufika shuleni, lakini kwa sasa wanafika shuleni hata wakiwa
kwenye hedhi na wanajua tutawasaidia vifaa na mazingira ya shule ni salama.
Tunaishukuru sana TGNP na ONGAWA, shule yetu kwa sasa imekuwa mfano wa kuigwa”.
Laya
Christopher, mwanafunzi wa kidato cha nne, shule ya sekondari Zirai anaeleza
kwamba tangu huduma za hedhi salama zimeboreshwa shuleni hapo na kuwepo kw a chumba
maalum cha kujisitiri, kuna mabadiliko makubwa ya ushiriki wa wasichana
darasani.
“Utaona
tu kila msichana anauhuru, anatabasamu muda wote, Kwa kweli sisi wanafunzi wa
kike katika shule ya sekondari Zirai, tunashukuru sana, kwa sasa hapa shuleni
tunaona na mahali salama kwetu, baadhi yetu hata hizo pedi huko nyumbani
zilikuwa hazipo, lakini sasa hivi zipo shuleni, ukiwa kwenye hedhi, unaona ni
bora kuwepo shuleni hautachafuka, utakuwa salama na hautapata aibu, ukienda
nyumbani utajua la kufanya, lakini jambo la msingi hapa shuleni umeshashiriki
vizuri vipindi vya masomo na kujisitiri vizuri”. Anaeleza Laya
Kwa
upande wake Amina Ayubu wa Kidato cha kwanza, anaeleza mtazamo wake kwamba yeye
ametokea shule ya msingi mwaka jana 2020, ambako hakuwahi kuona au kusikia
suala la hedhi likipewa kipaumbele au kujadiliwa kama ilivyo kwa shule hiyo ya
Zirai.
“nilipofika
hapa kuanza kidato cha kwanza, nimefurahi sana, nilijisikia vizuri kuona waalimu
wanazungumzia suala la hedhi na kuteuelekeza nini cha kufanya tukiingia kwenye
hedhi, tumesaidiwa ushauri na waalimu na pedi tunapatiwa hapa shuleni, kwa
kweli sina hofu tena juu ya hedhi, ninajua nikiwa hapa Zirai nitasoma vizuri na
nitafaulu..”alisema Amina.
Kwa
upande wake Afisa Programu kutoka ONGAWA, Leonia Andrew anasema kwamba lengo la
ONGAWA kuboresha mazingira ya utoaji elimu kwa watoto wa kike ni kuongeza
kiwango cha elimu kwa wasichana na kuwafanya wahitimue elimu yao ya sekondari
wakiwa kama wavulana.
“…Tunategemea
viongozi wetu ambao wamefanyiwa mafunzo ya umuhimu wa kuboresha miundombinu ya
hedhi salama, maji, afya na usafi wa
mazingira watasaidia kuhakikisha wanalipa kipaumbele, pia kwenye bajeti zetu tulipe
kipaumbele. Sisi wadau tunachoomba ni kwamba suala hili liwe na utashi wa
wananchi wa hapa na serikali yao, hata kama miradi inafikia ukomo, haya mambo
yote yanatakiwa kuendelea hapa kwa manufaa ya watu wa Zirai” alisema Leonia.
Kaimu
afisa Mtendaji kata ya Zirai, Florence Mosha anasema kwamba, kila kijiji
kinatakiwa kuchukua hatua za dhati za kutekeleza mpango kazi na vipaumbele
tulivyokubaliana hapa, ili tuweze kuwa na kata ambayo inazingatia usawa wa
kijinsia. “……Kila kitongoji mkafanye kikao na kurejesha kwa wananchi masuala
haya ya bajeti yenye mrengo wa kijinsia na kuweka mbele masuala ya hedhi salama
kwa wasichana katika shule zetu”.alisema
Mosha
Shule ya
secondary ya Zirai ina wasichana zaidi ya 150, ambao kwa sasa wanatumia pedi
boxi 10 kwa mwezi. Pedi hizo zimekuwa zikichangiwa na wadau mbalimbali, shule
kununua kutoka kwenye bajeti yake ya capitation na Kituo cha Taarifa na Maarifa
Zirai ambao wamekuwa wakichangishana na kutafuta wadau mbalimbali.
Wakati
wa mafunzo ya uandaaji wa bajeti kwa mrengo wa kijinsia kwa kuzingatia uboreshaji
wa miundombinu ya hedhi salama kwa viongozi wa kata ya zirai yaliyofanywa na
TGNP na ONGAWA, wenyeviti wa vijiji
vitatu vinavyounda kata hiyo, Kwalumbizi, Zirai na Kizerui, walisema
kwamba kila kijiji kimeweka kipaumbele cha kuhakikisha shule za msingi zina
miundombinu ya hedhi salama ikiwepo vyumba maalum vya kujisitiri pindi wakiwa
kwenye hedhi na kutenga bajeti ya kununua pedi kwaajili ya wanafunzo shuleni.
Pamoja
na vyumba maalum, kipaumbele kinawekwa pia kwenye kuhakikisha kila shule ya
msingi ina sehemu ya kuchomea taka mbichi na kavu (incinerator) ili kuhakikisha
pedi zilizotumika shuleni zinateketezwa na wanafunzo mara baada ya kutumika.
Mwisho
No comments:
Post a Comment