![]() |
'Kalamu' ikiwa nchini wakati mwandishi akiendelea na mazungumzo na mfanyabiashara huyo |
Na Deogratius Temba,
KALAMU sio kitu kipya kwa watu wote, unaposikia neno ‘Kalamu’
kinachokujia kichwani ni ile inayotumika kuandikia kwenye karatasi au sehemu
nyingine.
Huko Kibosho Moshi,mkoani Kilimanjaro, wanawake
wafanyabiashara wadogo wa ndizi mbivu, wanaotokea maeneo ya Kibosho Kirima ,
kwao kalamu ni aina ya Kibox ambacho
hutumika kubeba ndizi mbivu, kilichotengenezwa kwa ustadi mkubwa na fundi
seremala kwaajili ya kumwezesha kujitwisha kichwani na kusafiri nachO hadi Moshi
mjini kwaajili ya kuuza ndizi. Kalamu hutumika kutunza usalama wa mikungu ya
ndizi siziharibike.
![]() |
Mwandishi akiinyanyua 'Kalamu'tayari kwaajili ya kumtwisha ili aendelee na mizunguko |
Hivi karibuni, wakati wa mapumziko ya sikukuu za Noeli
(Krismas), nikakutana na Mama anayeitwa Maria Modest, ambaye ni mwenyeji wa
Kibosho - Kirima masoka ambaye anaitumia ‘kalamu’ kuuzia ndizi zake.
Nilimuuliza, ni kwanini hii inaitwa ‘kalamu’? akasema “kwani
hujui? Hii ilitumika tangu zamani sana, Bibi zetu ndio walikibatiza hiki kibox
jina hilo” akasema Maria akifikiri kwamba mwandishi ni mgeni sana eneo hilo.
![]() |
Mwandishi akimtwisha mfanyabiashara huyo 'kalamu' |
Mwandishi: kwanini hao kina Bibi wa zamani, wajasiriamali
walikiita jina hilo? Maria akajibu: “ahaaaa,
sasa ni kuambie, hao kina Bibi, walitusimulia kwamba walikiita hivyo kwa sababu
walifanya biashara hii ya ndizi kwa kubeba kichwani na wakafanikiwa kuwasomesha
watoto wao hadi wakafika vyuo vikuu”
Mwandishi: ehheee! Hadi
Vyuo vikuu kabisa? Ada inapatikana kwa hii biashara?
Maria: “ mhhhh, yaani mwanangu nikuambie, hata mimi ni
shahidi, nimesomesha watoto wangu shule nzuri, wapo wawili, mmoja ameshamaliza
Chuo Kikuu, na sasa amepata kazi, huyo mdogo wake yupo Chuo kikuu kingine,
ninalipa ada shilingi 1,600,000 kwa biashara yangu hii, na mimi nina pata
mahitaji yangu yote na matibabu” anaeleza maria kwa kujiamini.
Lakini maria anaeleza kwamba, wanawake wengi hapo awali hawakuamini kwamba biashara ile ya
kubeba ndizi kichwani itawakomboa, lakini kwa kuona wanawake wa Kibosho –Kirima
Boro waliofanikiwa waliamua kuiga na sehemu nyingine.
Anaeleza kwamba, wakiwa wanashangaa wale wanaotokea maeneo
ya Boro wanavyofanikiwa, wale wanaotokea maeneo ya Kirima Masoka, walikuja
kuiga biashara hiyo na sasa wamefanikiwa sana.
“Mimi ninazaliwa kule Boro, lakini nimeolewa Masoka, kule
Boro biashara hii ipo sana, wanawake karibia wote wenye afya nzuri wanafanya
biashara hizi, upatikanaji wa ndizi mbichi kwaajili ya kufundika ni wa shida,
lakini huku masoka ndizi zipo maana awali hakukuwa na ushindani mkubwa wa
wanawake anaozifundika” anasema Maria.
Jitihada za wanawake wengi kufanya biashara kwa lengo la
kujikombia kiuchumi zinafanikiwa kwa jinsi wao wenyewe wanavyoweka mtazamo
chanya juu ya kile wanachokifanya wakiamini kwamba kitaleta tija. Suala muhimu
ni serikali kuweka mifumo rafiki ya kuwawezesha kufanya biashara na kukutana na
wateja wao bila kusukumwa, kunyang’anywa biashara zao na mgambo, au maafisa
wengine.
No comments:
Post a Comment