Tuesday, December 19, 2023

Haya hapa mapendekezo 11 ya wakazi wa Kibaha kwa Halmashauri


Na Deogratius Temba, Kibaha

Wananchi kutoka kata ya Pangani, Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Mji, wanaoshiriki utafiti wa kiraghibish unaofanywa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), wametoa mapendekezo yao 11, yanayotokana na changamoto zilizoibuliwa wakati wa zoezi hilo lililoanza mapema mwezi huu

Picha ya pamoja ya washiriki wa kikao kazi cha mrejesho wa utafiti raghibish ngazi ya  Halmashauri, uliofanywa na TGNP , katika Halmashauri ya Kibaha Mji

Kikao kazi hicho cha mrejesho ngazi ya Halmashauri ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa “ Uimarishaji wa Sauti za wanawake, wasichana na watu wenye ulemavu katika uongozi na haki ya kumiliki rasilimali” unaofadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya wanawake (UNwomen).

Washiriki hao, wakiwasilisha mapendekezo yao kwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Charles Marwa, wamesema kwamba, pamoja na mapendekezo hayo, pia wameandaa mpango kazi ambao watautekeleza sambamba na viongozi wao. Kikao kazi hicho kilichoandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa kushirikiana na Idara ya Maendeleo ya Jamii wilayani hapo, pia kimehudhuria na wakuu wa Idara na Vitengo wa Halmashauri hiyo.

“Kutokana na hayo hapo juu, kutokana na changamoto kubwa zilizoibuliwa ambazo ni Uongozi usiowajibika na usiozingatia uwakilishi wa Kijinsia, Mila na desturi kandamizi, umiliki wa ardhi na rasilimali nyingine na Ukatili wa kijinsia hasa mimba za utotoni.  Biashara haramu ya ngono inachochea mmomonyoko wa maadili,  na kuongeza matukio ya Ubakaji kwa wanawake hasa wasichana, kuongezeka kwa uporaji na migogoro mikubwa ya ndoa ambayo inaadhiri kwa kiasi kikubwa watoto” amesema mwasilishaji wa mapendekezo hayo”alisema mwasilishaji. 

 

Tunapendekeza yafuatayo kwa ujumla wake yafanyiwe kazi.

 

  1. Kutokana na suala la uongozi usiowajibika kuibuka, na kukosekana kwa uwakilishi wa Kijinsia katika uongozi, na kupelekea kukosekana kwa sauti za wanawake, wasichana na watu wenye ulemavu kwenye maamuzi. Elimu ya usawa wa kijinsia itolewe kwa viongozi walioko madarakani, viongozi wa vyama vya siasa kuanzia ngazi za chini hadi wilaya.
  2. Viongozi walioko madarakani katika mitaa, wajengewe uwezo ili kujua mipaka ya kiutendaji, uwajibikaji, uandaaji wa miradi ya maendeleo kwa kuzingatia vipaumbele vyenye mtazamo wa Kijinsia, ushiriki wa wananchi kwenye mchakato wa O&OD
  3. Halmashauri isimamie mchakato wa uandaaji wa bajeti uwe shirikishi kuanzia ngazi za mitaa ili kuwepo kwa bajeti yenye mrengo wa Kijinsia itakayogusa mahitaji ya kila kundi na kuwezesha wanawake kumiliki rasilima.
  4. Halmashauri kwa kushirikiana na TARURA izipe kipaumbele barabara zinazounganisha Kata ya Pangani na Mji wa Kibaha ili kurahisisha usafiri na kupunguza kiwango cha umasikini kwa jamii  na kupunguza vifo vya mama na mtoto.
  5. Mwaka wa fedha 2024/25, Halmashauri itenge bajeti kwenye mapato yake ya ndani, kwaajili ya kugharamikia urasimishaji wa ardhi na mipango miji ili kupunguza mzigo wa gharama kubwa za upimaji kwa wananchi hasa wanawake na watu wenye ulemavu, lakini pia fedha hizo zitarudi kupitia kodi itakayolipwa baada ya kumilikishwa.
  6. Kuhuisha kamati za Ulinzi wa Mama na Mtoto (MTAKUWWA) katika kata na Mitaa yote, zitambue majukumu yake na mfumo wa uwajibikaji yaani ziwe na taarifa zake za utekelezaji.
  7. Bado tuna kundi la wanawake wasiojua kusoma na kuandika katika kata ya pangani.Tunashauri kuondoa tatizo hili  mwongozo wa kuwarudisha  wanafunzi walioacha masomo kwa sababu mbalimbali uanze kutumika ndani ya Kata ya Pangani. Mratibu Elimu Kata (MEK) aanze kuwabaini wasichana walioko mitaani na kuwarudisha shuleni kwa mujibu wa mwongozo au waraka wa Elimu namba 1 wa mwaka 2022.
  8. Halmashauri isaidie usimamizi  na utekelezaji wa sheria ndogo ambazo zitathibiti watoto wa shule kuzurura hovyo mitaani, kila shule itoe huduma ya chakula kwa wanafunzi, watoto kutokushiriki ngoma na mikesha ya usiku ya ngoma, kufunga sehemu zote zenye ‘ubanda’ panapofanyika biashara haramu ya ngono na mabanda mengine ya kuonyesha video yadhibitiewe watoto wasiingie.  
  9. Sheria kali zichukuliwe dhidi ya kutokomeza Mimba na ndoa za utotoni. Maafisa Ustawi wa jamii na Maendeleo ya jamii washirikiane na dawati la Jinsia na Mtoto-Polisi, kuharakisha kesi za ubakaji na wanaobainika wahukumiwe kwa mujibu wa sheri zetu.
  10. Kutenga bajeti kwaajili ya kupeleka maji kwa mitaa sita (6) kati ya Minane (8), ya Kata ya Pangani ambayo haina maji kabisa, hii inapelekea kuongezeka kwa vitendo vya Ukatili wa Kijinsia
  11. Katika uibuaji, kulijitokeza tatizo la kukidhiri kwa rushwa ya pesa na rushwa ya ngono ili kupata huduma, hasa urasimishaji wa ardhi. Tunashauri, viongozi wa serikali za Mitaa wajengewe uwezo ili wazingatie uadilifu, maadili ya uongozi na utawala bora.











 

No comments:

Post a Comment