Na Mwandishi Wetu, Kondoa
Halmashauri ya wilaya ya kondoa, mkoani Dodoma, kwa mwaka wa
fedha 2023/2024, imeandaa bajeti yenye mtazamo wa Kijinsia kwa kujenga
miundombinu ya vyoo vya shule vyenye kukidhi mahitaji ya wasichana wanapokuwa
kwenye hedhi.
![]() |
Washiriki wa Uchambuzi wa Bajeti kwa mtazamo wa Kijinsia wakiwa katika Picha ya Pamoja na wataalamu wa halmashauri ya wilaya ya Kondoa |
Hayo yalibainishwa na Afisa Mipango wa Halmashauri, Joshua
Mnyang’ali, alipokuwa akijibu taarifa ya uchambuzi wa Bajeti ya Halmashauri kwa
mtazamo wa Kijinsia iliyofanywa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa
kushirikiana na Vituo vya Taarifa na Maarifa Kata ya Haubi.
“Choo tulichojenga shule ya Msingi Mwisanga na shule mpya ya
sekondari ya Ntomoko, vina vyumba maalumu ya kujisitiri wasichana wanapokuwa
kwenye hedhi, kichomea taka kwaajili ya kuteketeza taulo za kike ambazo
zimetumika. Pia katika vyoo tunavojenga sasa, tunaweka sehemu ya haja ndogo kwa
wavulana, lengo ni kupunguza msongamano kwenye vyoo, ili wanafunzi wafurahie
kuwepo shuleni. Kwa kufanya hivyo tunapunguza pia utoro na kuongeza ufaulu”
alisema Mnang’ali.
Aidha naye mganga
mkuu wa halmashauri, Dkt Nelson Kimolo, amesema kwamba, Halmashauri hiyo kwa mwaka wa
fedha 2023/24, imedhamiria kupunguza kabisa au ikiwezekana kutokomeza vifo vya
mama na mtoto, kwa kutenga bajeti Zaidi ya shilingi Milioni 44 kwaajili ya
kuwalipa madereva wa ngazi ya jamii watakaotumika kuwasafirisha Mama wajawazito
kutoka zahanati kwenda Hospitali kubwa ili kurahisisha mfumo wa rufaa.
“Huu ni mradi unaojulikana kama M-MAMA ambao umeleta
mabadiliko makubwa, unasaidia sana kuondoa tatizo la usafiri, magari tuliyo
nayo ya kubeba wagonjwa hayatoshelezi, tumeona afadhal kuwa na utaratibu huu
mpya wa kuingia mikataba na madereva waliko kwenye jamii, wahudumu wa Hospitali
wawasilane nao muda wowote ili kuhakikisha Mama mjamzito anapata huduma ya
haraka na kukokoa maisha yake” alisema Dkt.Kimolo
Awali akiwasilisha mapendekezo ya Jumla mwezeshaji wa
Uchambuzi wa Bajaeti kutoka TGNP, Deogratius Temba, alisema kwamba, pamoja na
halmashauri kuwa na vyanzo vichache vya mapato ya ndani, bado wamejitahidi kuangalia
eneo la afya na elimu.
Temba, ameongeza kwamba, bado kuna mapengo ya kijinsia
kwenye Bajeti ya Halmashauri hasa katka eneo la ustawi wa Jamii ambapo Bajeti
ya kuzuia na kutokomeza Ukatili wa Kijinsia imetengwa kidogo, sambamba na Idara
ya Maendeleo ya Jamii inayotakiwa kuwajibika katika uhamasishaji wa jamii
kushiriki katika shughuli na maendeleo kutengewa fedha kidogo sana.
“eneo la Ukatili wa Kijinsia, ni muhimu
kuliangalia,tukiwekeza kwenye miundombinu ya elimu, alafu tusipoweka mikakati
ya kuwalinda watoto wa kike na kiume wasifanyiwe ukatili wa Kijinsia na
udhalilishaji wakingono, hatutapata matokeo mazuri”alisema Temba.
Pia, aneo linguine lenye mapungufu ambalo Halmashauri
imeshauriwa kuboresha na kuongeza msisistizo kwa viongozi wa vijiji na kata
kuwashirikisha wananchi kwenye mchakato wa kuandaa bajeti ili waweze kuibua
fursa na vikwazo katika maendeleo (O&OD) ili waweze kushiriki vizuri katika
kuisimamia na kuitekeleza miradi ya maendeleo.
Halmashauri kwa mwaka wa fedha 2023/24 imepanga kutumia
kiasi cha shs.milion 440 kuboresha vyanzo vya maji, sh. Million 3, kujenga
vichomea taka katika zahanati, sh. Million 23 kujenga mashimo ya taka mbichi
(placenta pit) katika zahanati na vituo vya afya, ambapo Kituo cha afya mnenia
kimetengewa bajeti ya sh. Million 35 kwaajili ya kujenga kichomea taka na vyoo.
Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), inatekeleza miradi
mbalimbali katika halmashauri ya Kondoa, inayolenga kujenga uwezo wa kwa jamii
kupitia Kituo cha taarifa na Maarifa, kupata uwezo wa kuchambua masuala ya
Kijinsia na kushawishi kuingzwa kwa masuala ya Kijinsia katika sera, mipango na
miongozo. Sambamba na kuwajengea uwezo viongozi mbalimbali wa Halmashauri
kuhusu masuala ya Usawa wa Kijinsia na Uongozi bora na ushiriki wa wanawake
katika uongozi.