Monday, January 27, 2025

“upatikanaji wa huduma za hedhi salama, ulivyo tejesha tabasamu kwa wasichana shuleni ”


Wanafunzi wa shule ya sekondari ya Zirai, Wilayani Muheza mkoani Tanga, wakiwa na Mwandishi wa Makala hii wakati alipotembelea shuleni hapo.

Na deogratius temba, Muheza

Mwongozo wa serikali juu ya Maji, Afya na Usafi wa mazingira wa mwaka 2016, unatoa maelekezo kwamba wadau  katika ngazi mbalimbali watahusika kusimamia utekelezaji wake ikiwepo kuhakikisha kuwa ujenzi wa miundombinu ya hedhi salama katika shule unakuwa na tija. Serikali kupitia wmongozo huo ulioandaliwa na Wizara ya elimu, sayansi na Mafunzo ya Ufundi, inazotaka kila Halmashauri kusimamia utekelezaji wa mwongozo huo ikiwa ni pamoja na kutenga bajeti kwa kila mwaka wa fedha kwenye mapato yake ya ndani ili kutatua changamoto zinazotokana na kukosekana kwa huduma nzuri kwenye eneo la Maji, afya na usafi wa mazingira (SWASH)  na kusababisha kiwago cha elimu kushuka.

Kama sehemu ya utekelezaji wa mwongozo huu wa serikali, Mtandao wa Jinsia (TGNP), kwa kushirikiana na Shirika la ONGAWA na  Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, wanatekeleza mradi wa Maji, afya na usafi wa mazingira (WASH) katika ngazi ya kaya na shuleni, ambapo suala la Hedhi salama shuleni linapewa msukumo wa kipekee ili kuwezesha wasichana kushiriki kikamilifu masomo shuleni wanapokuwa kwenye hedhi.  Utafiti wa awali kuhusu hali ya SWASH uliofaywa na serikali mwaka (2009) katika shule za msingi na sekondari iliyofanyika katika wilaya 16 Tanzania umeoneshasha kwamba hali ya Maji, Usafi wa mazingira katika shule ilikuwa chini. Ni asilimia 11 ya shule zilizofayiwa utafiti ndizo zilikuwa zimefikia hitaji la kisera la uwiano wa matundu ya vyoo wa Tundu moja kwa wasichana 20, na tundu moja kwa wavulana 25. Zaidi ya asilimia 20 ya shule zilikuwa na uwiano wa wanafunzi 100 na zaidi kwa tundu moja la choo. Wakati utafiti ulionesha kuwa asilimia 6 ya shule zilikuwa hazina kabisa matundu ya vyoo.

 

Picha halisi inaonesha kuwa utafiti huu wa Maji, Afya na usafi wa mazingira shuleni (SWASH), shule nyingi hazina miundombinu ya kutosha ya usambazaji wa maji, miundombinu hafifu ya usafi wa mazingira, hakuna kabisa mfumo wa kunawa mikono, baadhi ya vifaa vya usafi  ni vibovu au vimevunjwa.

Vifaa vya Maji, afya na usafi mazingira shuleni (SWASH) kama matundu ya vyoo, kwa shule nyingi hayalengi mahitaji ya wasichana wanapokuwa kwenye hedhi, watoto wadogo na wanafunzi wenye ulemavu, maeneo mengi yana mahudhurio hafifu kwa wasichana wanapokuwa kwenye hedhi kutokana na kukosekana kwa vifaa vya hedhi salama na usiri wa kujisitiri wakiwa kwenye hedhi.

Hivi karibuni, wasichana wa shule ya sekondari ya Zirai iliyoko katika Tarafa ya Amani -wilaya ya Muheza, walitoa sauti zao kushukuru wadau kwa kusaidia upatikanaji wa chumba maalum cha kujisitiri wanapokuwa kwenye hedhi, upatikanaji wa pedi za bure shuleni, maji safi na salama chooni, elimu na malezi bora ya makuzi yanayotolewa na waalimu wa kike shuleni hapo. Wanafunzi wamesema kwamba, sasa wanawea kusoma bila tatizo kutokana na kupata huduma za hedhi salama  shuleni na wengi waliokuwa hawafiki shuleni wakati wa hedhi.

Kwa upande wake Afisa Elimu Kata ya Zirai, Mwalimu Mohamed Mmole, anazungumzia mafanikio ambayo shule yake ya kata ya Zirai imeyapata kutokana na uwepo wa vyumba maalum vya kujisitiri kwa wasichana wakati wa hedhi pamoja na upatikanaji wa pedi shuleni. Anasema kwamba uongozi wa shule ulikubaliana kuwa suala la hedhi salama lipewe kipaumbele.  Pamoja na changamoto ya ukosefu wa rasilimali fedha za kununua pedi na vifaa vingine, walikubaliana kutumia fedha kidogo za ruzuku ya elimu kwa wanafunzi (capitation) inayotolewa kwaajili ya afya shuleni na kununua vifaa hivyo.

“……. inawezekana kabisa kusimamia vizuri utekelezaji wa mwongozo huu wa serikali wa Afya, Maji na usafi wa mazingira wa mwaka 2016, wadau wametujengea matundu ya vyoo na chumba maalum cha kujisitiri, sisi hapa shuleni tumeamua kuunga mkono juhudi hizi za wadau kwa kuhakikisha hizi pedi hazikosekani, dawa za kutuliza maumivu kwa kwaajili ya wasichana nazo hazikosekani” anasema Mwalimu Mmole.

Mwalimu Mmole anasema kwamba, pamoja na changamoto ya miundombinu ya usafiri katika kata, ukosefu wa maduka karibu na wananchi, uwepo wa huduma muhimu za kiafya kwa wanafunzi kunaongeza ushiriki wa wanafunzi hasa wasichana kwenye masomo, ikiwepo ongezeko la mahudhurio darasani.

Mwalimu mlezi wa wasichana shule ya sekondari Zirai,  Rehema Matuga, anaeleza:  “ Sisi kama waalimu tunashukuru sana, tunapoona wasichana wana utulivu hapa shuleni, awali kabla ya miradi hii ya  hedhi salama haijaanzishwa hapa kwetu, suala la hedhi kwa wasichana hatukulipa kipaumbele, watoto wa kike walikuwa wakijiamulia kutokufika shuleni, lakini kwa sasa wanafika shuleni hata wakiwa kwenye hedhi na wanajua tutawasaidia vifaa na mazingira ya shule ni salama. Tunaishukuru sana TGNP na ONGAWA, shule yetu kwa sasa imekuwa mfano wa kuigwa”.

Laya Christopher, mwanafunzi wa kidato cha nne, shule ya sekondari Zirai anaeleza kwamba tangu huduma za hedhi salama zimeboreshwa shuleni hapo na kuwepo kw a chumba maalum cha kujisitiri, kuna mabadiliko makubwa ya ushiriki wa wasichana darasani.

“Utaona tu kila msichana anauhuru, anatabasamu muda wote, Kwa kweli sisi wanafunzi wa kike katika shule ya sekondari Zirai, tunashukuru sana, kwa sasa hapa shuleni tunaona na mahali salama kwetu, baadhi yetu hata hizo pedi huko nyumbani zilikuwa hazipo, lakini sasa hivi zipo shuleni, ukiwa kwenye hedhi, unaona ni bora kuwepo shuleni hautachafuka, utakuwa salama na hautapata aibu, ukienda nyumbani utajua la kufanya, lakini jambo la msingi hapa shuleni umeshashiriki vizuri vipindi vya masomo na kujisitiri vizuri”. Anaeleza Laya

 

Kwa upande wake Amina Ayubu wa Kidato cha kwanza, anaeleza mtazamo wake kwamba yeye ametokea shule ya msingi mwaka jana 2020, ambako hakuwahi kuona au kusikia suala la hedhi likipewa kipaumbele au kujadiliwa kama ilivyo kwa shule hiyo ya Zirai.

“nilipofika hapa kuanza kidato cha kwanza, nimefurahi sana, nilijisikia vizuri kuona waalimu wanazungumzia suala la hedhi na kuteuelekeza nini cha kufanya tukiingia kwenye hedhi, tumesaidiwa ushauri na waalimu na pedi tunapatiwa hapa shuleni, kwa kweli sina hofu tena juu ya hedhi, ninajua nikiwa hapa Zirai nitasoma vizuri na nitafaulu..”alisema Amina.

Kwa upande wake Afisa Programu kutoka ONGAWA, Leonia Andrew anasema kwamba lengo la ONGAWA kuboresha mazingira ya utoaji elimu kwa watoto wa kike ni kuongeza kiwango cha elimu kwa wasichana na kuwafanya wahitimue elimu yao ya sekondari wakiwa kama wavulana.

“…Tunategemea viongozi wetu ambao wamefanyiwa mafunzo ya umuhimu wa kuboresha miundombinu ya hedhi  salama, maji, afya na usafi wa mazingira watasaidia kuhakikisha wanalipa kipaumbele, pia kwenye bajeti zetu tulipe kipaumbele. Sisi wadau tunachoomba ni kwamba suala hili liwe na utashi wa wananchi wa hapa na serikali yao, hata kama miradi inafikia ukomo, haya mambo yote yanatakiwa kuendelea hapa kwa manufaa ya watu wa Zirai” alisema Leonia.

Kaimu afisa Mtendaji kata ya Zirai, Florence Mosha anasema kwamba, kila kijiji kinatakiwa kuchukua hatua za dhati za kutekeleza mpango kazi na vipaumbele tulivyokubaliana hapa, ili tuweze kuwa na kata ambayo inazingatia usawa wa kijinsia. “……Kila kitongoji mkafanye kikao na kurejesha kwa wananchi masuala haya ya bajeti yenye mrengo wa kijinsia na kuweka mbele masuala ya hedhi salama kwa wasichana  katika shule zetu”.alisema Mosha

Shule ya secondary ya Zirai ina wasichana zaidi ya 150, ambao kwa sasa wanatumia pedi boxi 10 kwa mwezi. Pedi hizo zimekuwa zikichangiwa na wadau mbalimbali, shule kununua kutoka kwenye bajeti yake ya capitation na Kituo cha Taarifa na Maarifa Zirai ambao wamekuwa wakichangishana na kutafuta wadau mbalimbali.

Wakati wa mafunzo ya uandaaji wa bajeti kwa mrengo wa kijinsia kwa kuzingatia uboreshaji wa miundombinu ya hedhi salama kwa viongozi wa kata ya zirai yaliyofanywa na TGNP na ONGAWA, wenyeviti wa vijiji  vitatu vinavyounda kata hiyo, Kwalumbizi, Zirai na Kizerui, walisema kwamba kila kijiji kimeweka kipaumbele cha kuhakikisha shule za msingi zina miundombinu ya hedhi salama ikiwepo vyumba maalum vya kujisitiri pindi wakiwa kwenye hedhi na kutenga bajeti ya kununua pedi kwaajili ya wanafunzo shuleni.

Pamoja na vyumba maalum, kipaumbele kinawekwa pia kwenye kuhakikisha kila shule ya msingi ina sehemu ya kuchomea taka mbichi na kavu (incinerator) ili kuhakikisha pedi zilizotumika shuleni zinateketezwa na wanafunzo mara baada ya kutumika.

Mwisho