Sunday, July 9, 2023

KADINALI MTEULE RUGAMBWA NI NANI?


Kadinali Mteule, Mwadhama Protas Rugambwa

Na Mwandishi wetu

Baba Mtakatifu Francisco amemteua Mhasham Askofu Mkuu, Protas Rugambwa, kuwa Kadinali.

Ni kwa mara nyingine taifa la Tanzania, linapata baraka za kupewa kadinali wa tatu mzawa, akiwa ametanguliwa na Marehemu Laurian Kadinali Rugambwa na Policarp Kadinali Pengo.

Askofu Mkuu Rugambwa alizaliwa Mei 13, 1960 huko Bunena - Bukoba, nchini Tanzania, akapata Daraja Takatifu la Upadri kutoka mikononi mwa Mtakatifu Yohane wa Pili alipotembelea Tanzania Septemba 2, 1990 na kuwa Padri wa Jimbo Katoliki Rulenge - Ngara.
Kuanzia mwaka 2002 hadi mwaka 2008 alifanya utume wake kwenye Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu mjini Vatican.
Baba Mtakatifu Benedikto XVI, Januari 18, 2008 alimteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Kigoma, na Juni 26, 2012 aliteuliwa kuwa Katibu Mwambata wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu na Rais wa Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari na wakati huo huo kumpandisha hadhi na kuwa ni Askofu Mkuu.
Aidha, Novemba 9, 2017 Baba Mtakatifu Francisko alimteuwa kuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu baada ya kulitumikia Baraza kwa vipindi viwili na muda wake ulipogota ukomo, kadiri ya Katiba mpya ya Kitume inayojulikana kama “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” Juu ya Sekretarieti Kuu “Curia Romana” na Huduma Yake kwa Kanisa na kwa Ulimwengu” Aprili 13, 2023,

Baba Mtakatifu alimteuwa Askofu Mkuu Protase Rugambwa kuwa Askofu Mkuu wenye haki ya kurithi Jimbo kuu la Tabora, Tanzania.
Leo Julai 9, 2023, kwa neema za Kanisa na watu wa Mungu nchini Tanzania, ameteuliwa kuwa Mwanafalme wa Kanisa "Prince" yaani Kadinali. au Mwenye adhama (mwadhama) katika familia ya Mungu nchini.

Taifa la Tanzania linapata kiongozi, Baba wa kiroho na mshauri wa Papa kwa wakati mwingine, Watu wa Mungu wanamuombea matashi mema Katika utume wake nchini na Duniani.
Mtangulizi, Kadinali wa Kwanza Mwafrika na Mtazania, Marehemu Mwadhama Laurian Rugambwa


KADINAL WA PILI TANZANIA

Kadinal wa Pili Mtanzania kwa Taifa la Tanzania, na Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu la Dar es saalam, Mwadhama Policarp Kadinal Pengo. 


KARDINALI NI NANI?

Kardinali ni cheo kimojawapo cha juu katika Kanisa Katoliki, hasa Kanisa la Kilatini, lakini si daraja takatifu Ndio wanaomchagua Papa (Baba Mtakatifu)

Mkutano wa makardinali ndio humchagua Papa mpya ambaye ni mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani ambalo ndilo dhehebu la Ukristo kubwa kuliko yote. Uchaguzi hutokea baada ya Papa aliyetangulia kufariki au kung'atuka. Kwa mara ya kwanza kwa historia ya Kanisa, Marehemu Papa Benedict ndiye aliomba kustaafu katika kiti na kumwachia Papa Francis.  Lakini kardinali aliyefikia umri wa miaka 80 hashiriki tena katika uchaguzi wa Papa.

Kati ya kifo cha Papa na uchaguzi wa mwandamizi wake ni mkutano wa makardinali unaoongoza Kanisa lote kwa muda.

Uteuzi wa kardinali mpya

Kwa kawaida kardinali huteuliwa kati ya maaskofu, lakini kuna pia makasisi wachache wanaoteuliwa na Papa kuwa kardinali bila kupewa uaskofu.

Mwenye kuteua makardinali ni Papa peke yake, naye ana haki ya kumteua kardinali hata bila kutangaza jina lake hadharani (yaani anakuwa kardinali kwa siri).  Kardinali ya aina hiyo huitwa kwa Kilatini "in pectore" (yaani "moyoni"). Hii inaweza kutokea hasa kama ni kardinali kutoka nchi pasipo uhuru wa dini au nchi ambayo haina uhusiano mzuri na Kanisa Katoliki

Wajibu wa makardinalI

Wajibu mkubwa ni kumchagua mwandamizi wa Papa, lakini pia ni kazi yao kumshauri katika kuongoza Kanisa lote.

Kwa kawaida viongozi wa idara kadhaa za Kanisa wanapewa kofia ya kardinali.

Pia kwa sababu hiyo kuna idadi ya makardinali wanaoishi Vatikani au katika mitaa mingine ya jiji la Roma maana yake hawana majimbo au hawapo majimboni kama alivyokuwa Mwadhama Pengo.

Hata hivyo kwa sasa wengine wengi wanaishi katika nchi mbalimbali, wakiongoza majimbo. Hiyo haina maana kwamba wao ni wakuu wa maaskofu wenzao wa nchi hiyo au kwamba wana mamlaka yoyote juu ya Kanisa la nchi hizo.

Idadi ya makardinali

Hakuna idadi maalumu ya makardinali na mnamo 7 Novemba 2021 walifikuwa 215.

Papa Paulo VI aliunda utaratibu kuwa wasiwepo zaidi ya makardinali 120 wenye haki ya kupiga kura. Wale waliofikia umri wa miaka 80 hawashiriki tena katika uchaguzi wa Papa mpya. Lakini kardinali hajiuzulu wala kustaafu: anaendelea na cheo na pia na haki ya kushiriki katika mkutano wa makardinali hadi kifo. Kardinali aliyestaafu kuwa Askofu Jimbo au kuachia kiti cha Uaskofu Jimbo, anaendelea na majukumu kama Askofu Mstaafu-Jimbo (Bishop Emeritus). Anaweza kuendelea kupangiwa majukumu kadiri ya uwezo wake na Askofu Jimbo mahalia.

Kwa sababu ya uhusiano wao na Kanisa la Roma, kimapokeo makardinali wengi ni Waitalia, hata Mapapa walikuwa Waitalia watupu kwa karne nne mfululizo hadi alipochaguliwa Papa Yohane Paulo IIMpolandi.

Lakini asilimia ya makardinali Waitalia imepungua: kabla ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia zaidi ya nusu walikuwa Waitalia, siku hizi hawafikii asilimia 25.

MAKALA HII IMEUNGANISHWA KUTOKA VYANZO MBALIMBALI NA KUHARIRIWA NA

Deogratius Temba, kwa msaada wa Mitandao.

0784686575