Thursday, January 26, 2023
Wadau wagoma wanaume kuwa sehemu ya wahanga wa Ukatili wa kijinsia
Na Mwandishi Wetu, JmaiiVoice
Mashirika yanayofanya utetezi wa haki za wanawake na watoto nchini Tanzania, yametoa mapendekezo juu ya rasimu ya kwanza ya Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili wa Kijinsia kwa wanawake na watoto (MTAKUWWA) kuwa wanaume wasitajwe kuwa ni sehemu ya kundi lililoko hatarini kuathiriwa na Ukatili wa Kijinsia.
Wakizungumza na wandishi wa Habari, jijini Dar es salaam, wadau hao wa masuala ya Ukatili wa Kijinsia, Haki za watoto na wanawake, walisema kwamba;
“ ….tumesikitishwa sana na pendekezo lililotolewa la kujumuisha wanaume kama kundi linalokabiliwa na vitendo vya ukatili, sawa na wanawake na watoto kwenye Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili na tungependa kuweka wazi msimamo wetu wa kutokubaliana na pendekezo hili” ilisema sehemu ya taarifa yao.
Pendekezo hili linalopingwa na wadau hao, limeainishwa kwenye rasimu ya mpango kazi kama inavyosomeka “ Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake, Watoto na Wanaume 2023 - 2027”
Ikumbukwe kuwa MTAKUWWA 2017/18 - 2021/22 ilitengenezwa kwa kufuata maazimio ya kitaifa na kikanda yaliyoongozwa na takwimu kuhusu aina mbalimbali za ukatili na makundi yanayopitia ukatili zaidi katika jamii yetu. Maazimio haya yalijikita katika kuongeza jitihada za kuzuia ukatili hasa kwa wanawake na watoto, ili kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu ya mwaka 2030 (hasa lengo 5.2 na 16.2), Ajenda ya Afrika Tuitakayo ya mwaka 2063 na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025 ikilenga maisha bora, utawala bora na utawala wa sheria.
Taarifa hiyo imeelza kwamba, Katika jamii ya Tanzania, ukatili ni hali halisi ya kila siku kwa idadi kubwa ya wanawake na watoto kama ilivyo sehemu nyingi duniani. Kulingana na Ripoti ya Kimataifa ya Maendeleo ya Binadamu ya 2015, 35% ya wanawake ulimwenguni wamepitia ukatili wa kimwili au wa kingono kutoka kwa wenzi wao ambao huathiri ustawi wa wanawake.
Hapa Tanzania, karibu wanawake wanne kati ya kumi wamepitia ukatili wa kimwili, na mwanamke mmoja kati ya watano amepitia ukatili wa kingono katika kipindi cha maisha yake. Ukatili wa kingono na kimwili kwa wanawake ndani ya ndoa umekuwa zaidi kwa 44%.
Vilevile, baadhi ya mila na desturi za kitanzania zimekuwa zikishikilia mfumo dume ambao umeendelea kuwakandamiza wanawake na watoto huku wanaume wakionekana kuwa bora zaidi, jambo ambalo limefanya wanawake na watoto kuendelea kuwa kundi lililo hatarini zaidi katika kuathirika na vitendo vya ukatili.
Wadau hao, wamehitimisha kwa kutoa msimamo wao juu ya suala hilo, ambao ni:
• Rasimu ya Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili, itoe neno wanaume, na isomeke, Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili kwa Wanawake na Watoto 2023 - 2027.
• Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili, uendelee kuwatambua wanawake na watoto kama kundi linaloathirika zaidi na ukatili wa kijinsia katika jamii na linalohitaji kuwekewa mifumo wezeshi ili kuwalinda dhidi ya vitendo hivyo. Kwa kuwatambua wanaume kama focus ya mpango kazi, mpango kazi wa kitaifa unakuwa umepoteza lengo lake.
• Wanaume waendelee kushiriki katika mapambano dhidi ya ukatili kwa wanawake na watoto kama mabalozi,na sio kutambulika kama kundi linalokandamizwa.
• Wanaume wanaweza kuendelea kuripoti vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi yao kwa kutumia mifumo mingine ya kisheria bila kuingilia jitihada ambazo zimekua zikifanyika kuwakomboa wanawake na watoto ambao ndio waathirika wakubwa.
• Utengenezwaji wa Mpango Kazi mpya uzingatie na kuongozwa na takwimu kuhusu hali halisi ya ukatili katika nchi yetu. Jitihada zaidi ziwekwe kwenye kuboresha mifumo ya kuzuia na kushughulikia matukio ya ukatili, kuimarisha uratibu na kuongeza rasilimali fedha kwenye afua zinazolenga kutokomeza ukatili kwa wanawake na watoto.
Subscribe to:
Posts (Atom)